29.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA AKWILINA YAJIPANGA KUTOA UAMUZI MZITO


Grace Shitundu na Upendo Mosha-DAR/K’NJARO  |  

FAMILIA ya mwanafunzi Akwilina Akwilini aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati Jeshi la Polisi likidhibiti maandamano ya wafuasi wa Chadema jijini Dar es Salaam, Februari 16 mwaka huu, imesema inasubiri matokeo ya uchunguzi ifanye uamuzi wa kudai fidia.

Kauli hiyo ya familia imekuja wakati ambao baadhi ya wanasheria waliozungumza na MTANZANIA Jumapili wakinukuu baadhi ya vifungu vya sheria vinavyotoa haki ya kudai fidia kwa atakayethibitika kuhusika na kifo hicho.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, ikiwa ni takribani wiki moja tangu mwanafunzi huyo azikwe kijijini kwao Marangu, Kilimanjaro, msemaji wa familia hiyo, Dismas Shirima, alisema kwa sasa hawajaamua kiasi cha fedha watakachodai kama fidia ya mauaji ya binti yao.

Alisema familia hiyo itadai fidia ya mtoto wao mara baada ya uchunguzi kukamilika na kwamba kwa sasa bado hawajajua watamdai nani.

“Kwanza Rais Dk. John Magufuli aliagiza uchunguzi ufanyike kwa haraka, sasa wakati uchunguzi ukiendelea, hatuwezi kusema tunadai fidia ya kifo cha mtoto wetu,

“Pili, hata hatujui tunamdai nani kwa sasa, ila uchunguzi ukikamilika tutakaa kikao cha familia na tutaamua ni kiasi gani cha fidia kinapaswa kulipwa,” alisema.

MTANZANIA Jumapili lilipotaka kufahamu uchunguzi ulipofikia, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliahidi jambo hilo kulizungumzia kwenye mikutano yake rasmi na waandishi wa habari ingawa hakueleza ni lini.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili lililotaka kufahamu haki ya fidia kisheria, baadhi ya wanansheria nchini walisema familia hiyo inaweza kuidai kwa kutumia Sheria ya Madhara.

Wakili wa kujitegemea, Isaack Zake, alisema sheria za madhara zipo kwa kulinda na kuhakikisha madhara yanapojitokeza mwathiriwa anapata fidia inayostahili.

Alisema yapo makosa mengi ya madhara na mengine yanaweza kuwa ya jinai na ya madhara pia.

Akizungumzia tukio la kifo cha Akwilina, Zake alisema zinaweza kufunguliwa kesi za aina mbili.

“Kwanza kuna mauaji, hivyo ni lazima ifunguliwe kesi ya jinai baada ya uchunguzi au upelelezi kukamilika na endapo mahakama itamtia hatiani mtu yeyote, familia ina haki ya kufungua kesi ya madai kwa kuzingatia sheria hiyo ya madhara,” alisema.

Alisema baadhi ya makosa yanayoweza kusababisha madhara na mwathirika kuwa na haki ya kuchukua hatua za kisheria kudai fidia, achilia mbali mchakato wa kijinai unaopaswa kuendeshwa na Jamhuri, ni pamoja na makosa yatokanayo na uzembe na kusababisha madhara kwa mtu.

Makosa mengine alisema ni ya kumshambulia mtu na kumkashifu.

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea, John Malya, alisema sheria inawapa haki familia kudai fidia endapo itathibitika mtu yeyote amesababisha kifo cha mwanafunzi huyo.

“Endapo mahakama itathibitisha iwe mtu wa Serikali, polisi au mtu yeyote, familia inayo haki ya kudai kwa kuzingatia ni namna gani wameathirika kwa kuondokewa na ndugu yao.

“Kuna baadhi ya kesi watu hupata madhara katika mwili, lakini wanakuwa hai, hivyo inategemea na mtu mwenyewe atadai nini.

“Kwa mfano kama amevunjika mguu atadai kutokana na yale anayoona anakosa baada ya yeye kuvunjika mguu, hivyo kwa kifo watakaodai ni familia kwani wao ndio wanajua mchango wa marehemu katika familia,” alisema Malya.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema madhara ni matokeo ya kosa ambalo limefanywa na mtu ambaye ameshindwa kutekeleza wajibu wake, na kosa hilo likasababisha mtu mwengine kuathiriwa kwa kupata maumivu kimwili, kisaikolojia au kibiashara, hivyo kuvunjiwa haki yake.

“Hivyo katika tukio la Akwilina, sheria ya madhara inaweza kutumika kama ilivyokuwa katika kesi ya mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, marehemu Luteni Jenerali Imran Kombe aliyeuawa na polisi wawili.

“Katika kesi ile, baada ya mahakama kuwatia hatiani askari polisi wawili, mke wa marehemu alifungua kesi ya madai kudai fidia, ambayo mahakama iliridhia alipwe,” alisema.

Wakati Kijo–Bisimba akikumbusha hilo, kumbukumbu zinaonyesha katika kesi hiyo, mke huyo wa marehemu, Rosseleen Kombe, alidai fidia ya shilingi milioni 690 kutokana na kile alichodai kuwa baada ya kuuawa mumewe miradi mingi ilizorota.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Roseeleen alilipwa shilingi milioni 300 baada ya madai yake kusikilizwa na kuamuriwa.

Ilielezwa kuwa kifo cha Luteni Jenerali Kombe kilisababishwa kwa bahati mbaya na maofisa wa polisi ambao waliagizwa kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi kufuatilia gari lililoibwa aina ya Nissan Patrol mali ya mfanyabiashara Ladwa.

Kwamba wakati wanafuatilia, walikutana na gari alilokuwa anaendesha Kombe ambalo kwa  bahati mbaya lilikuwa linafanana sana na lile lililoibwa.

Ilielezwa wakati polisi wanalifukuzia gari hilo, walipiga risasi kwenye tairi na hivyo likaserereka likaegama mahali.

Kombe ambaye alikuwa na mkewe Rosseleen, walitoka ndani ya gari na kujisalimisha, lakini maofisa wa polisi wakafyatua risasi iliyompata Kombe.

Tukio la kupigwa risasi Akwilina lilitokea wakati polisi wakiwazuia wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kutoka Uwanja wa Buibui Mwananyamala, ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kufungia kampeni za ubunge wa Kinondoni kuelekea Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles