Na ANDREW MSECHU
WABUNGE 27 wa Chama cha Wananchi ( CUF), waliokuwa wakimuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wamejikuta njiapanda, kuondoka au kubadili upepo, waungane na uongozi mpya wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba aliwapa muda wabunge hao hadi jana Machi 31 wawe wametoa msimamo wao, kuwa upande wake au la.
Wabunge hao ambao baadhi yao walizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, walisema wataendelea kubaki ndani ya chama hicho kwa kuwa hadi sasa wanatambulika kuwa ni wabunge wa CUF.
Wabunge 28 wa CUF walikuwa wakimuunga mkono Maalim Seif.
Hatua hiyo inaleta sintofahamu baina ya wabunge waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif katika mgogoro wa ndani wa chama hicho uliodumu kwa miaka mitatu, uliomalizika baada ya Maalim Seif kuhamia ACT-Wazalendo wiki mbili zilizopita.
Mmoja wa wabunge hao, Hamidu Bobali alitangaza hadharani kupitia mkutano wa Lipumba kuwa ameamua kurejea upande wa mwenyekiti huyo baada ya uamuzi wa mahakama uliomhalalisha.
Wabunge 27 waliobaki wameendela kuwa na kigugumizi hata baada ya siku ya mwisho kuweka msimamo wao kuhusu hatima yao iliyotolewa na Lipumba, ambayo ilikuwa jana, Machi 31.
Mbunge Alli Saleh, Malindi alisema kwa sasa wameamua kwa kauli moja, kutozungumzia suala hilo kwa kuwa ubunge wao si suala la kujadiliwa, bali ni suala la uamuzi wao ikizingatiwa ndio waliochaguliwa na wananchi.
“Kwa sasa sisi ni wabunge, hatuko tayari kuanza kuzungumzia mambo mengine, hatuzungumzii habari hiyo ya kuhama au kubaki kwa sasa,” alisema.
Mbunge wa CUF Mgogoni, Ally Yusuph Suleiman alisema hana taarifa yoyote kuhusu muda uliotolewa na Profesa Lipumba na kwamba ni suala ambalo bado hajalitolea uamuzi.
“Kuhusu msimamo wangu katika hilo, sina taarifa ya muda huo wa mwisho uliotolewa, ila mtapata habari, kuweni na subira,” alisema.
Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara (Bwege) alisema anachojua ni kwamba yeye ni mbunge wa chama hicho hadi sasa kwa hiyo si suala la kuhoji.
“Mimi kwa upande wangu, hadi sasa mimi ni mbunge kupitia CUF, sijasema naenda kokote. Nadhani umenielewa,” alisema.
Alipotafutwa, Mbunge wa Chake Chake, Yusuph Makame aliomba atumiwe ujumbe wa maneno kwa kuwa simu yake haisikiki vizuri, lakini alipotumiwa ujumbe huo kuhusu kueleza msimamo wake hakutuma majibu.
Katika Uchaguzi wa 2015, CUF ilipata wabunge 42, kati yao wa majimbo ya Tanzania Bara na Zanzibar walikuwa 32 na viti maalumu 10. Hata hivyo, wabunge watatu wa Bara walihamia CCM.
Wabunge 28 wa majimbo kati yao 22 kutoka Zanzibar na wanne wa Bara na mmoja wa viti maalumu walionekana kuwa upande wa Maalim Seif, huku wabunge watatu wa majimbo ya Bara na tisa viti maalumu wakionekana kuwa upande wa Lipumba.
Tayari Profesa Lipumba na wenzake wamebadili Katiba ambayo sasa inampa mwenyekiti mamlaka ya kuteua katibu mkuu, ambaye sasa ni Khalifa Suleiman Khalifa.