27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Pierre, Makonda waibua mjadala

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwatahadharisha watu wanaomuunga mkono na kumshabikia msanii wa vichekesho,   Pierre Gumbo, maarufu Pierre Liquid, mjadala mzito umeibuka.

Juzi, wakati wa harambee ya kuchangia elimu Wilaya ya Kisarawe iliyopewa kaulimbiu ya ‘Tokomeza Ziro Kisarawe’, Makonda alisema msanii huyo hapaswi kupewa kipaumbele.

 “Ningewasihi sana waandishi wa habari  kina mama wanaojituma na kuhangaika kwa ajili ya watoto wao ndiyo wapewe kipaumbele, si hao walevi walevi,  kina sijui, Pierre.

“Unakuwa na taifa ambalo watu wa ovyo ndiyo wanapewa umaarufu halafu watu wa maana hawajulikani hata walipo…hauwezi kuwa na taifa lina – promote watu wa ovyo halafu unategemea watoto wetu watafika kwenye mafanikio,” alisema Makonda.  

Hata hivyo kauli hiyo imeibua mjadala baada ya watu mbalimbali kutofautiana naye huku wakimtetea msanii huyo.

Dk. Kigwangalla

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, katika ukurasa wake wa twitter aliandika kuwa nchi haiwezi kujengwa na watu wanaofanya mambo magumu pekee na kwamba kila mmoja ana sehemu yake.

“It’s ok kwa Pierre Liquid kufanya anachofanya na kufurahisha wanaoona anachekesha. Pierre anatuchekesha na kutukumbusha kufurahia maisha tunapopata nafasi, hasa tunapotoka kufanya hayo mambo yetu magumu magumu.

“Jamani maisha ni magumu, yana mitihani mingi na ni mafupi sana, katika kuleta furaha na shangwe kwenye maisha ndiyo maana wachekeshaji wakapata ajira.

“Wengine tusome udaktari, uhandisi na tufanye uvumbuzi na utatuzi wa changamoto na wengine watutetemeshe, watuvuruge akili, watupe na furaha…watuchekeshe siku zisogee,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema Pierre ni mtu huru kwenye nchi yake na uhuru huo unapaswa kulindwa kama Katiba ya nchi inavyoelekeza, hivyo aachwe apate riziki yake.

“Mungu anajua zaidi kwa nini hatukumjua miaka mitano iliyopita na kwa nini sasa anazua mjadala. Hata kwa mimi binafsi, Mungu anajua zaidi kwa nini sikuwa waziri miaka mitano iliyopita na leo ni waziri.

“Mungu anatupangia maisha yetu, anatugawia mafungu yetu, pengine hii inaweza kuwa sababu ya Pierre kuwa mtu bora zaidi leo kuliko ile siku aliyopiga kelele na raha na kubembea pale Liquid. Pengine hii ndiyo nyota yake ya jaha…Pierre atabaki kuwa juu, Pierre atabaki kuwa kileleni,” aliandika Dk. Kigwangalla.

NIKKI wa PILI

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nikson Simon maarufu Nikki wa Pili alisema Pierre anajitambua na amekuwa akifanya mambo muhimu kama kuhamasisha uzalendo kwa timu ya taifa na kuchangia elimu.

“Somo la Piere kwa wanywaji wote, usinywe ukaenda nyumbani ukampiga mkeo, kunywa lakini changia maendeleo ya elimu, hamasisha michezo na uzalendo kwa timu yako.

“Ukiwa mnywaji wa namna hii utabaki juu ila ukinywa ukaharibu familia, ukachepuka, ukaharibu kazi, ukala mtaji wewe utabaki chini,” alisema msanii huyo.

DC JOKATE

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, alisema katika harambee aliyoiandaa, alialika wasanii na watu wengi akiwamo Pierre ambaye alichangia Sh 100,000.

“Katika dhifa niliyoiandaa jana (juzi) nilialika watu wengi, wanasiasa, taasisi za Serikali, mabalozi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wasanii, wadau wa burudani na wengine.

“Kipekee kabisa ninamshukuru Pierre, wako watu maarufu wengi mno tuliowaalika lakini hawakufika, ila wewe (Pierre) ulichukua muda wako kuhamasisha na kufika na zaidi ya hapo ukatoa mchango wa Sh 100,000. Hukuja kuuza sura tu, nasema ahsante sana,” alisema Jokate katika taarifa yake iliyosambaa kwenye mitandao ya  jamii.

  Jokate ambaye pia ni msanii wa mitindo alimkaribisha msanii huyo kwenda kuwekeza Kisarawe na kuahidi kumpatia eneo aanzishe hata mgahawa.

“Wana Kisarawe tunakupenda, tunasema samahani kwa kukwazika lakini zaidi ahsante kwa kushiriki. Nimesikia pia ni mtengenezaji mzuri wa furniture (samani), hii shule tunayoenda kujenga inahitaji madawati naomba tufanye kazi na wewe katika hii fursa,” alisema.

PIERRE AMWACHIA MUNGU

Katika ukurasa wake wa twitter jana, Pierre aliandika kuwa anayetoa riziki ni Mungu pekee na kuwashukuru Watanzania kwa kumthamini.

“Nashukuru sana kwa thamani mliyonipa Watanzania mmenisaidia nimepiga hatua kwenye maisha yangu. Nilikuwa ni mtu wa furaha nashukuru mmeniongezea sana furaha.

“Si kila mtu anapenda mafanikio yako, wengine huyachukia, lakini tukumbuke anayetoa riziki ni Mungu pekee, jaribu kuvuta picha maisha yako miaka 10 iliyopita hadi leo hii umefanikiwa.

“Wakati sijithamini Mungu alinipatia Watanzania kunipa uthamani, ni wachache sana wanakumbuka walipotoka   baada ya kupata mafanikio. Usimdharau mtu kutokana na madhaifu au kutokana na mafanikio yako,” alisema Pierre.

ALIVYOIBUKA

Msanii huyo almeibuka hivi karibuni na kuwa kivutio ndani na nje ya nchi kupitia matukio anayoyafanya.

Amekuwa akinywa pombe kisha kuonyesha vituko mbalimbali vya kuchekesha hatua iliyomwezesha kufahamika haraka na kuanza kupata kazi kupitia usanii huo huku akialikwa kwenye baa mbalimbali kuvutia wateja   kwa kulipwa fedha na wakati mwingine hufanya matangazo ya biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles