33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE 11 WASOTA KIZIMBANI

*Msigwa na wenzake wapandishwa kwa kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM

NA WAANDISHI WETU – MBEYA/IRINGA


WAKATI Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akipandishwa kizimbani jana, akidaiwa kuchoma nyumba aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM Iringa, wabunge wengine kumi, wanasota kizimbani kwa kesi mbalimbali zinazowakabili.

Kesi za watunga sheria hao, zipo kwenye mahakama tofauti nchini, huku baadhi yao wakiwa na zaidi ya kesi moja kwenye mahakama tofauti.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ambaye kwa sasa anatibiwa nje ya nchi, anakabiliwa na kesi za uchochezi zaidi ya moja kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), anakabiliwa na kesi ya uchochezi mkoani Arusha na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema) naye anakabiliwa na kesi ya uchochezi ambayo kwa sasa mashahidi wa upande wa mashtaka wanatoa ushahidi wao.

Wabunge wengine wa Chadema, Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero na Suzan Kiwanga wa Mlimba, wanakabiliwa na kesi ya uchochezi mkoani Morogoro.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), anakabiliwa na kesi ya kumshambulia mwili Mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM).

Wabunge wengine wa Chadema, Cecil Mwambe (Ndanda), Pascal Haonga (Mbozi) na Frank Mwakajoka (Tunduma) wote wanakabiliwa na kesi za uchochezi.

Naye Mbunge wa Donge, Sadifa Khamis Juma (CCM), anakabiliwa na kesi ya rushwa mkoani Dodoma.

 

MSIGWA KIZIMBANI

Jana, Msigwa na washtakiwa wengine 12, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, wakikabiliwa na kesi mbili, ikiwemo ya kuchoma nyumba ya Mary Tesha, aliyokuwa akiishi Katibu wa UVCCM Iringa Mjini, Alphonce Muyinga, na kuvunja nyumba ya aliyekuwa diwani wa Mwangata kupitia Chadema, Anjelius Mbogo, aliyejiuzulu na kujiunga CCM.

Washtakiwa hao kwa pamoja walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngunyale, huku Mchungaji Msigwa akiwa ni mtuhumiwa wa saba kwenye kesi zote mbili.

Msigwa alikamatwa na polisi siku ya Jumatatu baada ya  kuripoti kituo cha Polisi mjini Iringa kuwajulia hali washtakiwa wengine ambao tayari walishakamatwa.

Wakili wa Serikali, Felix Shakla, alidai kuwa kati ya Januari 5 na 14, mwaka huu,watuhumiwa kwa pamoja walipanga njama za kuharibu mali ya mtu kinyume na sheria za nchi.

Alidai pia kuwa Januari 15, mwaka huu, watuhumiwa waliharibu mali kwa kubomoa nyumba ya Anjelus Mbogo aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwangata, ambaye alijiuzulu udiwani kwa tiketi ya Chadema na kuhamia CCM.

Baadhi ya watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Iringa Mjini, Leonce Marto na Diwani Mteule Viti Maalumu, Rehema Mbeta.

Washtakiwa wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja ambao kila mmoja alipaswa kusaini ahadi ya dhamana ya Sh milioni  tatu.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa wote wanaotetewa na wakili mmoja, Antony Rutebuila, waliachiwa kwa dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Februari 14, mwaka  huu.

 

KESI YA SUGU

Mkoani Mbeya, upande wa utetezi katika kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli, inayomkabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Sugu na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda, Emmanuel Msonga, umesema unakusudia kuleta mashahidi saba na vielelezo vinane.

Uamuzi huo wa utetezi unafuatia kukamilika kwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, ambao ulileta mahakamani mashahidi watano na vielelezo viwili.

Wakili wa utetezi, Boniface Mwambukusi, alisema wapo tayari kuanza kuwasilisha utetezi wao leo kuanzia saa nne asubuhi ili waweze kupata muda wa kuwasiliana na wateja wao na kuwapa ushauri wa kisheria.

Awali, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Michael Mteite, alitupilia mbali ombi la mawakili wa utetezi la kutaka ushahidi wa sauti wa shahidi wa tano katika kesi hiyo, Inspekta Joram Magova, usipokewe mahakamani hapo kwa madai kuwa haukidhi matakwa ya kisheria.

Mteite alitaja baadhi ya sababu za kutupilia mbali pingamizi hilo kuwa mahakama imejiridhisha kuwa uhifadhi wa kifaa cha kurekodia sauti na aliyekitumia kurekodi hana masilahi yoyote na kesi hiyo.

Alisema pia mahakama imejiridhisha kwamba shahidi aliyeandaa taarifa ya sauti alikuwepo kwenye eneo husika, hivyo aliweza kurekodi, na kwamba kazi ya kutengeneza haimwondolei yeye uhalali wa kuwa shahidi.

Pia mahakama imesema kuwa sheria ya elektroniki imeeleza wazi shahidi ana haki ya kuchezesha mkanda kwa kusikilizwa mahakamani ili kuthibitisha kile anachokitolea ushahidi.

Kesi hiyo jana ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Mwakagenda.

Sugu  na Masonga wanadaiwa kuwa Desemba 30, mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, walitoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli.

 

Habari hii imeandaliwa na PENDO FUNDISHA (Mbeya) na FRANCIS GODWIN (Iringa)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles