25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE ILIYOJENGWA KWA TOPE YABOMOLEWA, WANAFUNZI SASA WASOMEA CHINI YA MTI

NA FLORENCE SANAWA – MTWARA


BAADA ya picha ya madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa makuti ya Shule ya Msingi, Mitambo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani hapa kusambaa katika mitandao ya kijamii, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Omary Kipanga, ameagiza yabomolewe na sasa wanafunzi waliokuwa wakiyatumia wanasomea chini ya miti ya mikorosho.

Akizungumzia hali hiyo, Kipanga alisema majengo hayo yalijengwa kwa utashi wa wananchi bila kushirikisha halmashauri hiyo.

“Kile kilichokuwa kimejengwa sio kwa maagizo ya ofisi yangu, Oktoba nilipita kwenye shule zote kukagua, lakini sikuona majengo kama yale, kama ni kujenga wamejenga wananchi, tena kama sio Novemba itakuwa Desemba.

“Hata mwongozo wa Wizara ya Elimu hausemi tujenge darasa kama lile, hata jiko hatukuambiwa tujenge mfano ule, hatukuagizwa, yale si madarasa, hata ingekuwa ya muda yale sio madarasa, ule ni uchafu, sio mahala pake ndio maana nimeagiza yabomolewe.

“Niliwaambia kuwa nyie mmejenga kwa utashi wenu, hamkunijulisha. Hivyo lazima wabomoe, nikawaambia mlichoelekezwa ni kujenga maboma sio ule uchafu, hata ukiangalia vizuri katika eneo la shule, misingi imeshaanza kuchimbwa ili kuanza ujenzi wa madarasa mazuri.

“Tunazo shule 10 zinahitaji ujenzi na ukarabati wa hali ya juu, hivi sasa katika Shule ya Msingi Mitambo tutajenga madarasa matatu ili yawe sita. Kwa darasa moja tutajenga kwa Sh milioni 20 huku tukitenga Sh milioni 40 kwa nyumba za walimu, lakini wananchi pia watajenga, hivyo kutakuwa na madarasa manne,” alisema Kipanga.

Nae Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rashid Chalido,  alisema baada ya kikao cha wazazi na walimu kilichofanyika mwaka jana mwishoni, walikubaliana kujenga madarasa hayo ili kuwanusuru watoto na kero za mvua zinazokuwa zinawakabili.

“Mwaka jana tulifanya kikao, tuliona tatizo ni kubwa na watoto wanaathiriwa na mvua shuleni, ndiyo maana tuliamua kujenga madarasa ya muda ili watoto wapate pa kujishikiza, lakini tumepata agizo kutoka uongozi wa juu likitutaka tuvunje hayo madarasa ili kuanza ujenzi wa madarasa manne ambao unaanza mara moja,” alisema Chalido.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mitambo, Salum Akola, alisema kutokana na wazazi kuona adha waliyokuwa wakipata watoto shuleni hapo, walilazimika kujenga madarasa ya muda ili kuwasaidia watoto hao.

“Kwakweli sisi tulikwama, hata ukiangalia wanafunzi wengi wamekuwa wakitapakaa hovyo nje, hali ambayo inamfanya mwalimu kushindwa kuwadhibiti kutokana na uhaba wa madarasa, hivyo kufanya utoro kuongezeka nyakati za masomo,” alisema Akola.

Katibu Msaidizi Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Wilaya ya Mtwara (MTWANGONET), Fidea Luanda, alisema katika mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya elimu,  walitembelea shule sita na kubaini uwepo wa hali mbaya ya mazingira ya shule hizo ikiwamo Mitambo.

Alisema kuwa mbali na shule hiyo kuwa na madarasa matano yaliyojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti, bado mlundikano wa wanafunzi katika madarasa hayo ulikuwa mkubwa zaidi kutokana na kuchanganyishwa kwa madarasa mawili.

“Yaani kutokana na uhaba wa madarasa, walimu wanafundisha darasa la saba huku darasa la sita wako darasani, na ukifuatilia utaona kuwa zipo shule zina madarasa mawili,  watoto wapo wa awali hadi darasa la saba, niambie watasoma vipindi vingapi kwa siku, ndiyo maana utoro umekuwa mkubwa, watoto wanasoma kwa kupishana, hii ni hatari,” alisema Luanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles