25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YA 27 AFRIKA MATUKIO YA KUJINYONGA- WHO

Na MWANDISHI WETU


RIPOTI ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imeitaja Tanzania kushikilia nafasi ya 27 barani Afrika kwa vifo vinavyotokana na watu kujiua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye kurasa 34, Tanzania inashikilia nafasi  ya nne kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa wingi wa vifo vinavyotokana na watu kujiua.

Katika ukanda huo, Rwanda inaongoza kwa kuwa na asilimia 8.5 ya vifo vya kujiua ikifuatiwa na Burundi yenye asilimia 8.0. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Uganda kwa kuwa na asilimia 7.1 huku Tanzania ikishikilia nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia 7.0.

Nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni pamoja na Kenya ambayo inashikilia nafasi ya tano kwa kuwa na asilimia 6.5 na ya sita ni Sudani Kusini yenye asilimia 6.4.

Kwa bara la Afrika, Equatorial Guines inaongoza kwa wingi wa vifo vinavyotokana na watu kujiua kwa kuwa na asilimi 22.6 ikifuatiwa na Angola yenye asilimia 20.5 na ya tatu ni Ivory Coast yenye asilimia 18.1.

Duniani, Sri Lanka inashikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa asilimia 35.3 ikifuatiwa na Lithunia yenye asilimia 32.7 na ya tatu ni Jamuhuri ya Korea yenye asilimia 26.3.

Antigua na Barbuda ni nchi pekee duniani katika ripoti hiyo ambayo haina tukio lolote la watu kujiua.

Takwimu hizo za WHO, zimetolewa kutokana na viashiria vya Maendeleo Endelevu ya Melenia (SDG) kwenye sekta ya afya.

Ripoti tofauti ya WHO kuhusu vifo vinavyotokana na kujiua  iliyotolewa mwaka 2014 , ilionesha  Tanzania kushikilia nafasi ya nane kwa vifo vya aina hiyo ikirekodi vifo 25  kwa kila vifo 100,000 sawa nan chi ya Nepali.

Ripoti hiyo inataja kunywa sumu, kujinyonga na matumizi ya silaha za moto kama baadhi ya mbinu ambazo hutumiwa na watu wanaojiua au kujaribu kujiua na kuongeza kuwa kuweka masharti makali ya upatikanaji wa nyenzo hizi kunaweza kusaidia kupunguza matukio ya kujiua.

Kwa mujibu WHO, karibu watu 800, 000  hufariki dunia kutokana na kujiua kila mwaka ikiwa ni wastani wa vifo vya watu 40 kwa kila dakika moja.

Shirika hilo la afya linasema, vifo vinavyotokana na kujiua hutokea katika kipindi chote cha maisha ya binadamu na kwamba ndiyo chanzo namba mbili cha vifo kwa watu wenye umri kati ya miaka 15-29 duniani.

“Vifo vinavyotokana na kujiua vimekuwa vikiongezeka duniani. Asilimia 78 ya vifo hivi vimetokea kwenye nchi zenye uchumi wa chini na wa kati kwa mwaka 2015,” inasomeka sehemu ya taarifa iliyopo kwenye tovuti ya WHO.

Zaidi, WHO inasema vifo vinavyotokana na kujiua vinafanya asilimia 1.4 ya vifo vyote duniani na kufanya kuwa chanzo kikubwa cha vifo namba 17 duniani kwa kipindi cha mwaka 2015.

WHO inashauri tatizo hilo kupewa uzito wa kutosha na kusisitiza jitihada mbali mbali zifanyike katika ngazi za jamii na kwa ngazi ya mtu kwa mmoja mmoja ili kuzuia vifo vinavyotokana na kujiua pamoja na majaribio ya kutaka kujiua duniani.

Jitihada mbali mbali zimekuwa zikifanyika kukabiliana na tatizo hili ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Vifo Vinavyotokana na Kujiua (WSPD) ambayo huadhimishwa duniani kila tarehe Septemba, 10.

WHO imekuwa mmoja wa wadhamini wa siku hiyo ambayo imekuwa ikilenga kuelimisha umma sehemu mbali mbali duniani kwamba, vifo vinavyotokana na kujiua vinaweza kuzuilika.

Wanasaikolojia

Akizungumzia ongezeko la idadi ya watu kujinyonga nchini, mwanasaikojia Daniel Marandu alisema hali hiyo inasababishwa na mfumo mzima wa maisha kubadilika ikiwemo upatikanaji wa fedha, ajira na mengineyo.

“Unakuta mtu zamani watoto wake walikuwa wanasoma shule za gharama lakini kutokana na hali ilivyo sasa anashindwa kumudu na kukata tamaa,”alisema.

Alisema hivi sasa watu wengi wanaachishwa kazi kwa kupunguzwa katika makampuni mbalimbali pamoja na wenye vyeti feki hivyo inawafanya kukataa tamaa ya maisha.

“Utakuta mtu amefanya kazi kwa miaka 55, lakini leo anakuja kutumbuliwa kwa cheti feki, hivyo anajiona hapati hata yale mafao yake ya miaka yote hiyo na mbele haoni ‘future’ hivyo anaona bora ajinyonge,”alisema Marandu.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni msongo wa mawazo unaosababishwa na mahusiano ya mapenzi, kwa sababu siku hizi wengi wanachanganya mapenzi na fedha.

“Stress ya mahusiano ya kimapenzi imekuwa ni chachu kubwa ya watu kujinyonga, hii ni kwa sababu wengi wamereplace mapenzi na pesa hivyo wengine wanashindwa kujizuia pale anaposikia mpenzi wake au mke/mume ana mahusiano na mtu mwingine.

“Hii stress (msongo wa mawazo) ni mbaya zaidi bora ya kufiwa na mzazi unaweza kulia siku mbili ukasahau, lakini ya mapenzi ni tofauti wengi wao wanajikatia tamaa na kujinyonga,”alisema.

Aliwashauri watu wanaokutana na matukio ya aina hiyo, kutafuta mtu wa karibu au wataalamu ambao wataweza kuwashauri.

“Watu wasitafute solution (ufumbuzi) ya kudumu kwa tatizo ambalo ni temporary, kuachwa katika mapenzi ni safari tu kwa sababu atakuja mwingine hivyo watu wanapaswa kuwa wavumilivu.

“Ukizidiwa tafuta mtu mwelezee kwa sababu unavyomwelezea mtu unatema zile sumu,”alisema Marandu.

Kwa upande wake mwanasaikolojia na Mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Christian Bwaya alisema wengi wanafikia hatua hiyo pale wanapokuwa na matarajio makubwa.

“Pale unapokuwa na matarajio makubwa halafu hufakiwi wengi wanakata tamaa na kuamua kujinyonga. Pia mtindo wa maisha umebadilika wengi muda mwingi wako kazini hawana mawasiliano au mahusiano ya karibu na watu.

“Huna marafiki wa karibu, muda mwingi tunatumia kazini lakini unapokuwa na mtu wa karibu inakuondolea stress.

“Ushauri wangu kwa watu wa aina hiyo; kuhakikisha pamoja na kwamba una mambo mengi uhusiano na familia na marafiki ni muhimu.

“Tafuta rafiki ambaye mnafahamiana umwelezee na matukio haya yakifika kiwango fulani mtafute mtaalamu ambaye atayabeba matatizo yako, itakusaidia,” alisema Bwaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles