24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

WASOMI WAICHAMBUA KAULI YA JAJI MKUU

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


BAADHI ya wasomi nchini wameichambua kauli ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma Ibrahim, ya kuwataka viongzi wa Serikali kujiepusha kuingilia muhimili wa mahakama, ambapo baadhi yao wameiunga mkono na wengine kutoa tahadhari.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema kumekuwa na tabia ya Serikali kuiingilia mihimili mingine ikiwamo Bunge na mahakama.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha Iringa, Profesa Gaundence Mpangala, alisema uamuzi huo ni hatua nzuri na anayoiunga mkono kwa kuwa itawezesha mahakama kutoa uamuzi wa haki.

Profesa Mpangala alisema licha ya mazingira ya kidemokrasia kutaka kila mhimili kuwa huru katika kutekeleza majukumu yake, nchi nyingi zenye demokrasia changa ikiwamo Tanzania Serikali imekuwa ikiliingilia mihimili ya Bunge na mahakama.

Alisema katika mazingira ya uhuru wa mihimili hiyo ndiyo maana mahakama ya juu nchini Kenya iliweza kusema uchaguzi haukuwa huru licha ya Rais aliyekuwa madarakani kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo ulifanyika Agosti 8 mwaka jana.

“Kama kungekuwa na kuingiliwa kwa mhimili wa mahakama wasingeweza kusema uchaguzi haukuwa huru, wakati aliyeshinda ni Rais alikuwa madarakani.

“Kutoingiliwa kwa uhuru wa mahakama ndiko kunawezesha mahakama kutoa uamzi wa haki. Kwa mfano hapa nchini Bunge linaingiliwa sana, lilitoa uhuru kwa vyombo vya habari kuingia bungeni kutoa habari kwa wananchi, lakini serikali ikaingilia na kuzuia kurushwa kwa matangazo ya moja kwa moja, huko ni kuingiliwa kwa mhimili mwingine” alisema Profesa Mpangala.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema japo katika serikali hii hakujakuwa na uingiliaji wa moja kwa moja wa mahakama kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Rais Mkapa bado yapo matukio machache ya kuingiliwa kwa mhilimi huo.

Alisema mahakama imekuwa ikiogopa kwa lengo la kuiridhisha Serikali hasa katika mambo yanayoihusisha Serikali dhidi ya viongozi wa upinzani.

Alisema viongozi wa upinzani wamekuwa wakikamatwa na kunyimwa dhamana kwa woga.

“Sina hakika sana kama Jaji Mkuu pia anaogopa ila hawa mahakimu wamekuwa wanaogopa hata kutoa dhamana. Hicho ni kitu kizuri kuwazuia wasiingilie mahakama.

“Lakini kama anataka wasiingiliwe ni lazima wao wasiiogope Serikali. Tangu Profesa Juma ameingia madarakani kushika nafasi ya Jaji Mkuu watendaji wamekosa umakini.

“Wanazo facilities nyingi kama vile magari ya kisasa, basi wafanye kazi ili professionalism yao tuione” alisema Profesa Safari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kauli ya Jaji Mkuu imetokana na mambo yanavyokwenda hapa nchini kwa sasa kwa sababu viongozi wanafanya chochote kinacho wajia kichwani bila kuangalia mipaka yao.

“Kuna matamko mengine yanatolewa kama watu anahukumiwa huko huko, lakini kikubwa ni pale ambapo mahakama imetoa hukumu au amri ile amri inadharauliwa unakuta watendaji wanafanya vitu ambavyo tayari kuna amri ya mahakama, hiyo kwa kweli kwa chombo cha mahakama ni kuikosea heshima.

“Mahakama inapotoa zuio au amri jambo fulani lisiendelee alafu lakini wanatokea watendaji wa Serikali au mamlaka zingine zinasema vinginevyo, unakuta mtu ana amri ya mahakama lakini kama ni jengo lake litavunjwa shughuli iliyokuwa imaembiwa isiendelee inaendelea kwa hiyo inakuwa ni kuidharau mahakama kwa sababu amri ya mahakama inatakiwa itekelezwe” alisema Dk. Helen.

Alisema pia viongozi wamekuwa wakitoa matamko ya kutaka watu kufungwa idadi fulani ya miaka  tofauti na mahakama ambayo inatakiwa kuangalia sheria kama inamfunga mtu au inamwachia huru.

Alise mtu mwenye mamlaka anapojitokeza na kusema mtu angefungwa maisha ni kuingilia uhuru wa mahakama, na kumfanya hakimu afikirie kuwa asipofanya hivyo anaweza kuwa anakwenda kinyume.

“Mhimili huo unaonekana unashindwa kuonekana unafanya kazi inavyostahiki kutokana mna hali za nchi zetu hizi wanafikiria wengi kuwa mwenye mamlaka kama ambavyo Rais aliwahi kusema kuwa yeye ndiye anayetoa bajeti kwa hiypo inaweza kuwa inawafanya wengine wanashindwa kusimamia kama tulivyoona kule Kenya jinsi ambavyo mahakama ya juu ilitoa amri juu ya Serikali bila kuwa na ukakasi hata kidogo.

“Wakati mwingine haieleweki hivyo wanakuwa na wasiwasi wanafikiria kuwa Serikali ni kubwa zaidi kuliko mahakama, inafika wakati mahakama inakuwa na kigugumizi, haieleweki , lakini ukweli ni kwamba wakisimamia zilivyo wao ni mhimili kama ulivyo mhimili wa Serikali au Bunge, wanatakiwa wafanye mambo yao kwa mujibu wa sheria inavyosema bila kujali.

“Maana kuna wakati unakumbuka mwaka jana wakati Lema amewekwa kizuizini, mahakama ya juu rufani ilipopelekwa iliitaka ile mahakama wasikubbali mihimili mingine isiwaingilie, hiyo ilionekana walikuwa wanamweka mtu ndani kwa force za nje na si kwa sababu kwa mujibu wa sheria.

“Nilichogundua Watanzania wengi ni waoga haijalishi wako wapi wanaweza kuwa wanaiogopa Serikali wanaogopa mamlaka nyingine wanafanya mambo kinyume cha sheria” alisema Dk. Helen.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Jaji Mkuu ni kutekeleza jukumu lake la kuwakumbusha viongozi na wananchi kuheshimu mhilili wa Mahakama.

“ Anatukumbusha kwa sababu watu wanatoa maamuzi magumu yanayoingilia uhuru wa mahakama, si serikali tu, hata wananchi wamekua wakiingilia uhuru wa mhimili huu utaona uamuzi unatolewa watu wanaupinga.

“Kwa hiyo anatukumbusha kuhusu kuheshimu mihimili iweze kuheshimiana na kuwe na section balance, watu wanatakiwa kuipa uhuru mahakama kama wanavyofanya kwa Serikali na Bunge” alisema Dk. Bana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles