|Hadija omary, Lindi
Licha ya serikali mkoani Lindi kuweka sheria ya kuwataka wanunuzi wa zao la ufuta kutoa ufuta wao ndani ya siku saba baada ya kununua, bado wanunuzi hao wameendelea kuweka ufuta wao katika maghala ya vyama vya msigi.
Hatua hiyo imesababisha kuwapo kwa mlundikano mkubwa wa ufuta katika vyama hivyo.
Akizungumza katika mnada wa zao hilo uliofanyika katika kijiji cha Kipelele, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani hapa, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Kipelele, Abasi Abdalah amesema kuwapo kwa ufuta huo kwa muda mrefu katika vyama vyao kunaweza kusababisha hasara kwa vyama hivyo pindi ufuta huo utakapoibiwa.
“Mimi naamini huu mnada kuna matajiri wa zao hili wanataka watajirike kupitia vyama vya ushirika kwa kutotoa mizigo yao mapema kwenye maghala.
“Hii pia inaweza kuwafanya kula njama na wezi wakaja kuiba ufuta ule na baadaye wakarudi kupita katika vyama vyetu jambo hili ni hatari sana kwa vyama vya msingi tusipoangalia tutaingia madeni yasiyotarajiwa,” amesema Abdallah.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Runali, kinachojumuisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa , Nachingwea na Liwale, Hassani Mpako amesema iko haja kwa serikali kufanya marekebisho katika msimu wa mwaka 2019 ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeka katika msimu uliopita.