21.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 6, 2022

MAKALA: Tundu Lissu afunguka wabunge Chadema kwenda CCM

NA, TUNDU LISSU, UBELGIJI


Kwako Wakili Mahinyila:

NAFIKIRI una tatizo moja kubwa: unaelekea kuamini kila tuhuma inayoelekezwa Chadema na wanachama wetu wa jana na juzi.

Sijakusikia ukijipa tahadhari ya kujiuliza swali moja rahisi: hivi kwa nini wahamaji wetu hawa wanagundua maovu ya ndani ya Chadema pale tu wanapoondoka na kuhamia CCM?

Lipo lingine ambalo nadhani pia ni swali muhimu la kujitahadharisha na maneno ya wahamaji hawa: ni kwa nini ‘wimbi’ hili la wahama chama lipo Chadema tu kwa sasa???

Nitaanza na swali la kwanza na mtaniwia radhi nikiwarudisha nyuma kidogo katika historia ya chama chetu. Tukifahamu historia ya masuala haya hatutayumbishwa na makelele ya akina Mwita Waitara wa sasa na wajao.

Katika wahama Chadema wa kwanza kabisa, Dr. Amani Walid Kabourou, Katibu Mkuu na baadaye Makamu Mwenyekiti wetu alikuwa ni maarufu zaidi.

Huyu alihama mwaka 2006, mara baada ya kupoteza ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005.

Dr. Kabourou alihama akiwa Makamu Mwenyekiti wetu, takribani miaka miwili baada ya timu ya Mheshimiwa  Mbowe na Dr. Slaa kuchukua uongozi wa Chadema.

Heshima pekee ya Dr. Kabourou, kwa kuzingatia haya ya waliofuata baadaye, ni kwamba yeye aliondoka bila kusema sana. Angalau mimi sikuwahi kumsikia akiyoyoma kama hawa wa baada yake.

Hizi tuhuma za ruzuku na ‘Uchaga’ dhidi yetu zilianza na Makamu Mwenyekiti wetu aliyerithi mikoba ya Dr. Kabourou, Marehemu Chacha Zakayo Wangwe.

Chacha alikuwa rafiki yangu mimi tangu tulipokutana kwa mara ya kwanza mwaka 2003, wakati wa harakati za kudai haki za wananchi wa Nyamongo dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara sasa. Nilimkuta akiwa diwani wa Kata ya Tarime Mjini kupitia NCCR-Mageuzi.

Tayari alikuwa na kesi kumi na moja za kubambikiziwa na Mgodi na maswahiba wao CCM, wakiongozwa na kaka yake mwenyewe Peter Wangwe ‘Keba’, wakati huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mwaka uliofuata Chacha alifungwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi minne. Nilijitolea kuwa wakili wake katika rufaa ya Mahakama Kuu Mwanza.

Kitu ambacho wengi hawakijui ni kwamba gharama zote za usafiri wa kwenda Mwanza na baadaye Tarime kumtetea kwenye kesi kumi zilizobaki zilitoka kwenye mifuko binafsi ya Mwenyekiti Mbowe.

Tulishinda rufaa na kupangua kesi nyingine zote kumi katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime.

Chacha hakuwahi kuchangia shilingi moja katika kesi zake zote, hata ya ubunge ya 2006. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005 mimi binafsi nilifanya kampeni sana Tarime.

Na baada ya kutatua tatizo la ubambikiziaji wananchi kesi za uongo, tuliwasambaratisha CCM na Chacha alichaguliwa kwa kura nyingi kuliko mbunge mwingine yeyote wa upinzani.

Kwa hiyo Chacha Zakayo Wangwe aliingia bungeni akiwa na umaarufu mkubwa ndani na nje ya chama. Kwangu binafsi tatizo lilianzia hapo. Kwanza alianzisha ugomvi mkubwa ndani ya Chama wilayani Tarime.

Ndani ya mwaka mmoja aligombana na viongozi karibu wote wa Chadema  Wilaya waliomsaidia kupata ubunge.

Ndani ya mwaka huo huo, alihama jimboni na kuhamia Dar es Salaam.

Chacha aliyenyanyaswa sana na Wazungu wa Nyamongo akawa anaenda jimboni Tarime kwa ‘lifti’ ya ndege za Wazungu wa Mgodi wa Nyamongo. Mengine sitayasema hapa.

Mwaka huo huo, kufuatia kukimbia kwa Makamu Mwenyekiti Kabourou, Chacha akawa Makamu Mwenyekiti wetu.  Mwaka huo huo wa 2006, Chacha akaanza kuwaambia wananchi wa Tarime waliokuwa wanamhoji sababu za kukimbia jimbo, kwamba si lazima agombee ubunge mwaka 2010 kwani atakuwa ana ‘majukumu makubwa ya kitaifa.’

Haukupita muda Chacha Zakayo Wangwe akatangaza kuwa anataka kugombea Uenyekiti wa chama Taifa ili kuondoa ‘Uchaga’ na kugawa ruzuku hadi wilayani badala ya kuliwa na watu wa Makao Makuu.

Hapo ndipo zilipoanzia tuhuma za ‘Uchaga wa Chadema’  na ‘ulaji wa ruzuku.’

Wakati huo tulikuwa na wabunge watano wa kuchaguliwa na Viti Maalumu sita na ruzuku haikuwa inafika hata milioni 50

Kuhusu ruzuku. Kitu cha kwanza cha kuelewa ni kwamba ruzuku yetu haijawahi kutosheleza hata mahitaji ya kawaida ya uendeshaji chama.

Kila inapotokea kuna uchaguzi wa marudio au Uchaguzi Mkuu wowote ule, matumizi yamekuwa ni makubwa kuliko mapato yetu ya ruzuku na michango ya wabunge.

Tunapowapiga sana wabunge wetu, tuwe tunakumbuka pia kwamba nje ya ruzuku, wabunge wetu wamekuwa ndio chanzo kikubwa cha mapato ya chama hasa nyakati za Uchaguzi Mkuu au uchaguzi wa marudio.

Kwa sababu ya upungufu huo wa mapato, hasa kila wakati wa Uchaguzi Mkuu, tumelazimika kukopa pesa kwa ajili ya kampeni kwa mapatano kwamba madeni hayo yatarudishwa baada ya Uchaguzi Mkuu.

Sasa ni vyema tujiulize, katika hali halisi ya Tanzania hii, ni kina nani hasa ambao wako na wamekuwa, tayari kukikopesha chama?

Ni wachache sana, kwa sababu za wazi kabisa: hofu ya kunyanyaswa na polisi au uhamiaji au TRA.

Nimekuwa naingia kwenye vikao vya Kamati Kuu tangu mwaka 2004 na ninaweza kusema kwa uhakika kabisa kwamba hakuna kikao cha Kamati Kuu kilichokaa kuzungumzia maandalizi ya

Uchaguzi Mkuu au uchaguzi wa marudio, ambacho hakikumwambia Mwenyekiti wetu atafute pesa za kampeni hata kwa kukopa, ili tuweze kununua vifaa vya kampeni au kulipia huduma zinazohitaji malipo.

Chopper, magari, pikipiki, bendera, mabango na kila aina ya vifaa vingine vya uchaguzi vinapopatikana kila Uchaguzi Mkuu au uchaguzi wa marudio, huwa hatuna utamaduni wa kuuliza au kujiuliza vifaa hivi vyote vitakuwa vimegharimu kiasi gani na pesa hiyo itakuwa imetoka wapi.

Hata hivyo, kila baada ya uchaguzi tunapoanza kulipa madeni ya waliotukopesha kwa maagizo ya Kamati Kuu ya chama, kunakuwa na kelele kubwa kwamba ruzuku ya chama inaliwa na viongozi wakuu, hasa Mwenyekiti.

Na kila anayehama chama na kukimbilia CCM anarudia rudia tuhuma hizo mpaka watu wetu wanaanza na wao kuzirudia rudia.

Na lengo kubwa la mashambulizi haya, miaka yote, ni Freeman Aikaeli Mbowe, huyo huyo ambaye kila uchaguzi ukifika tunamwomba atutafutie pesa za kampeni.

CCM wanajua wanachokitaka kwenye kampeni hii ya kumchafua Mwenyekiti wetu.

Wapambe wao, hasa wahamaji hawa, nao wanajua. Je, sisi wanachama wa Chadema  tunaozirudia rudia tuhuma hizi tunajua hii ngoma tunayoicheza? Naambiwa CAG naye amehoji juu ya matumizi ya ruzuku yetu.

Ni kweli. Lakini ni kweli pia kwamba CAG amezungumzia pesa za ruzuku ambazo hatujawahi kuzipata tangu tuanze kupata ruzuku.

Na kwenye suala la ruzuku, maafisa wa ofisi ya CAG wametuhumiwa kutoa taarifa yao bila kutupa sisi fursa ya kujibu ‘audit queries’ zao, kama inavyotakiwa na sheria na taratibu za ukaguzi wa hesabu.

Tunapaswa hapa kukumbuka kwamba CAG na maafisa wake ni wateule wa Jiwe na/au watumishi wa Serikali ambao, kwa mazingira ya sasa ya Tanzania ya Magufuli, wanashinikizwa sana kutafuta namna ya kuiumiza Chadema.

Kwahiyo, badala ya kumeza kila kinacholetwa kwa jina la CAG, tunahitaji angalau kujihadhari na taarifa hizo kwa kuuliza maswali muhimu juu ya usahihi wake.

Kumalizia hoja hii ya ruzuku. Tumeijibu tangu ilipoanza kuibuliwa na Marehemu Chacha Wangwe mwaka 2006/2007. Tumeijibu wakati tunashughulikia ‘Mkakati wa Mabadiliko’ wa kina Zitto na Kitilla Mkumbo.

Tumejieleza na kujieleza. Lakini CCM na wapambe wao wana malengo yao ya kutaka tuendelee kujadili ruzuku ya Chadema.

Inawauma kwamba tangu mwaka 2005 tulipoanza kuonesha aina mpya ya kampeni za kisiasa. Tangu wakati huo, mafanikio yetu yamekuwa makubwa zaidi.

Kutoka chama chenye wabunge watano mwaka 2000 hadi chama kikuu cha upinzani chenye wabunge 72 mwaka 2015 ni mafanikio makubwa.

Ruzuku yetu imeongezeka pia, hata kama bado haikidhi mahitaji yetu yote. Wakati najiunga Chadema mwaka 2004, ruzuku yetu ilikuwa Sh. milioni 5.6 kwa mwezi. Leo ni takribani Sh. milioni 250 kwa mwezi.

Haya ni mafanikio makubwa. CCM wanajua hivyo lakini hawawezi kusema hivyo hadharani.

Hawafurahishwi nayo. Ukitaka kujua wanatuonaje angalia mambo yote wanayotutendea. Mauaji, vipigo, vifungo vya kusingiziwa, ukiukwaji wa haki za kisiasa, propaganda chafu, nakadhalika. Kuhusu kifo cha Marehemu Chacha Zakayo Wangwe.

Hii pia ni propaganda chafu iliyoanzishwa na CCM. Ulizeni watu wetu wa Tarime kilichotokea mara baada ya kifo cha Marehemu Chacha.

Ghafla msiba ule ukawa wa kina Wassira na CCM wenzao. Ukweli ni kwamba tuhuma hizi zilianzishwa na Wassira na genge lake wakati wa msiba huo.

Vijana wa CCM walitolewa Bunda, Musoma na maeneo mengi nje ya Tarime na kuletwa kuja kumfanyia fujo Mwenyekiti wetu msibani.

Ndugu zake Chacha, wale wale waliokuwa wakimbambikizia kesi ili afungwe wakati wa uhai wake, wakawa sasa ndio wenye uchungu naye akiwa amekufa. Hata hivyo, wananchi wa Tarime walielewa kilichokuwa kinaendelea.

Ndio maana kwenye uchaguzi wa marudio baada ya kifo cha Marehemu Chacha, tuliwapiga vibaya.

Na ndio maana Tarime imeendelea kuwa ngome kubwa ya Chadema. Inatosha tu kujiuliza kama kweli tungekuwa tumemuua Chacha, hawa CCM kwa jinsi wanavyotuchukia wangetubakiza kwa hii miaka kumi?

Tunatakiwa kujielewa, tusije tukajikuta tunacheza ngoma ya maadui zetu wakubwa.

Nizungumzie swali langu la pili. Kwa miaka zaidi ya kumi sasa, Chadema ndio adui nambari moja wa CCM. Dhambi yetu kubwa ni ile ile iliyokuwa dhambi kubwa ya NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 1995 na 2000; na CUF kati ya 2000 na 2005.

Ni dhambi ya kuwa chama kikuu cha upinzani. Ni dhambi ya kuwa na mafanikio makubwa kwenye uchaguzi.

Ni dhambi ya kupendwa na kuungwa mkono na wananchi. Kwa sababu ya dhambi hiyo, ni lazima tushambuliwe na kuchafuliwa na kufanyiwa kila aina ya fujo na hila.

Tusipolielewa hilo ni rahisi sana kukatishwa tamaa na haya ya kina Waitara wa juzi, jana na wanaokuja mbeleni.

Ili tusibabaishwe na haya ya Magufuli na watu wake na hawa Yuda Iskariote, tukumbuke tu tulikotoka.

Tulikuwa na Amani Walid Kabourou kama Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Aliondoka na kujiunga na CCM. Tulisonga mbele.

Tulikuwa na Zitto Zuberi Kabwe, Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. Tulimwondoa na tukasonga mbele.

Tulikuwa na Mzee Saidi Arfi, Makamu Mwenyekiti na mrithi wa marehemu Chacha. Alitoroka na kujiunga nao, haikuwa mwisho wetu.

Tulikuwa na Dr. Wilbrod Peter Slaa, Katibu Mkuu na Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo. Alitukimbia katikati ya vita lakini hatuku-surrender. Tulisonga mbele.

Hawa wanaomkimbilia Jiwe, huyu anayetuogopa hadi kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa, wanatubabaishaje?

Mwisho, kwa yote ambayo nimeyasema hapa, sina maana sisi ni malaika tusiokuwa na doa lolote. Tuna mapungufu mengi ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi ili kuyaondoa.

Mengine ni ya kujitakia; mengine ni ya kutakiwa na maadui zetu.

Tupembue yapi ni ya kwetu wenyewe na yapi ni ya CCM. Yote tuyatafutie dawa.

Tundu Lissu ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria mkuu wa Chadema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,814FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles