Na PENDO FUNDISHA- MBEYA
WATENDAJI sita  wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi na kusomewa mashitaka matatu, likiwamo la uhujumu uchumi.
Miongoni mwa watendaji hao ni aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, Mkurugenzi wa halmashauri, Elizabeth Munuo na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji hilo, Samweli Razalo.
Wengine ni aliyekuwa mhasibu mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, James Jolojiki, Mhasibu Msaidizi Tumaini Msigwa na Mkuu wa Idara ya Ujenzi, Henry Maganga.
Akisoma mashitaka hayo, mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa, Michael Mteite, mwendesha mashitaka wa serikali kutoka makao makuu, Shadrack Matini, aliyataja mashitaka hayo kuwa ni kuisababishia mamlaka ya serikali hasara na uhujumu uchumi.
Alisema, makosa hayo ni kinyume cha kifungu kidogo cha sheria namba 10 (i)pamoja na kifungu namba 57(i) na namba 60(i) na (ii)Â Â cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 ya sheria za Tanzania iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika kosa la kwanza mwendesha mashitaka huyo alisema, Mshitakiwa Athanas Kapunga na Elizabeth Munuo, kati ya  mwezi Mei  na Desember 2008, katika Jiji na Mkoa wa Mbeya kwa nyakati tofauti kwa matendo yao ya kukusudia waliisababishia halmashauri  hasara ya Sh bilioni 3,360 423,611, kwa kusaini hati ya mkataba wa kukopa fedha benki ya CRDB na mkopo huo ukaanza kulipiwa riba kabla ya shughuli za ujenzi wa soko la Mwanjelwa kuanza.
Shitaka la pili linawahusu washitakiwa. Samweli Razalo, James Jolojiki, Tumaini Msigwa na Henry Maganga ambao waliisababishia serikali hasara.
Alisema washtakiwa wengine kwa tarehe tofauti kuanzia mwaka 2008 hadi 2013 katika Halmashauri ya jiji la Mbeya, kwa pamoja kwa kutokutekeleza majukumu yao katika njia sahihi waliisababishia halmashauri ya jiji hilo kupata hasara ya Sh milioni 304,470,500.
Alisema kiasi hicho cha fedha waliilipa Kandarasi ya ujenzi aliyejenga jengo la soko la Mwanjelwa kutoka Kampuni ya Danda Limited kwa kazi ambazo tayari zilishafanywa na mkandarasi mwingine Ms Tanzania Limited.
Shitaka la tatu linawahusu washitakiwa, Samweli Razalo, James Jolojiki, Tumaini Msigwa na Henry Maganga ambapo kwa tarehe tofauti kati ya 2008Â na 2013, waliisababishia halmashauri hasara ya kiasi cha Sh bilioni 1,140,228,750 kwa kuilipa kampuni iitwayo Tanzania Building Works kwa ajili ya ujenzi wa soko la Mwanjelwa kwa kazi ambazo hazikufanyika na hazikuwepo.
Awali, akitoa angalizo la kesi hiyo, Hakimu mfawidhi Michael Mteite, alisema mahakama hiyo inawasomea washitakiwa mashitaka hayo kwa mujibu wa sheria na itaandaa mashitaka yatakayowasilishwa mahakama kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.