Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
WAKATI leo ikiwa mwisho wa uwasilishaji fomu za tamko la mali na madeni viongozi mbalimbali wamepishana kuwasilisha taarifa zao katika ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika mikoa mbalimbali nchini.
Katika ofisi za Kanda ya Dar es Salaam Mtanzania iliwashuhudia viongozi kadhaa wakipishana wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi na madiwani ambao kila mmoja alikuwa akipota kuwasilisha fomu ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi, ambapo wanatakiwa kufanya hivyo hadi kufikia leo 31, 2019.
Ikiwa watabainika ambao watashindwa kufanya hivyo ni watakuwa wakikabiliana na makosa ya kimaadili.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekele, alisema kuwa licha ya kutokuwa na takwimu rasmi lakini mwitikio umekuwa mzuri katika ofisi zote za kanda na kwamba leo unatarajiwa kuwa mzuri zaidi.
“Kutowasilisha tamko ni kosa la kimaadili na sheria iko wazi kuwa kama mtu asipowasilisha kwa sababu zisizo za msingi, utaona kumbe sheria imeweka sababu za msingi ambazo mtu anaweza asiwasilishe tamko kwa wakati,” alisema Jaji Nsekela.
Alipoulizwa kuwa sheria imeelekeza lini kiongozi wa umma anapaswa kuwasilisha tamko hilo, Jaji Ndekela alisema kuwa kwa bahati mbaya sheria haijaweka wazi suala hilo na kwamba wao wanaona kuanzia Oktoba ni muda mzuri wa kufanya hivyo.
“Ujazaji wa tamko hili uko mara tatu, ukipewa wadhifa unajaza, unapostaafu unajaza kwaheri lakini kama hapo katikati, hujapewa wadhifa na hustaafu unatakiwa ujaze.
“Ukiniuliza kwanini hawajazi mapema sina jibu huenda ni hulka zetu kwa sababu wajibu wetu tunaujua kwa sababu tunapopewa wadhifa tunajaza tamko,” alisema Jaji Nsekela.
Akitoa wito kwa viongozi kuelekea mwakani ambapo kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani alisema kuwa licha ya kwamba bado ni mapema na kuna mamlaka zinazopaswa kulizungumzia hilo ikiwamo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lakini ni vema viongozi wakawa watu wenye maadili kwa sababu ndilo msingi wa kila kitu.
“Viongozi tusiwe na madoa madoa tuwe na maadili katika jamii,” alisema Jaji Nsekela.
JPM AREJESHA
Desemba 29, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli aliwasilisha tamko linalohusu mapato, rasilimali na madeni ya viongozi katika Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria na kikatiba.
Tamko hilo liliwasilishwa na Katibu wa Rais, Ngusa Samike ambaye alitumwa na Rais Magufuli ambaye yupo mapumzikoni wilayani Chato na limepokelewa na Kamishna wa Sektretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kupokea tamko hilo Jaji Nsekela, alisema kitendo alichokifanya Rais Magufuli, kimetekeleza takwa la kikatiba Ibara ya 132 (5) (D) linalowataka viongozi kuwasilisha taarifa za tamko la mapato, Rasilimali na madeni mara kwa mara lakini pia ametekeleza sheria no 13 ya mwaka 1995 kingu cha 9.
Kutokana na hali hiyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wengine kutumia siku 2 zilizobaki kufanya hivyo kabla ya leo Desemba 31, mwaka huu katika kutekeleza takwa hilo la kisheria na kikatiba.
WAJIBU WA SEKRETERIETI YA MAADILI
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais ambapo ilianza kazi zake rasmi Julai mwaka 1996.
Sekretarieti ya Maadili ilianzishwa ili kutekeleza Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Na. 13 ya mwaka 1995 kama ilivyo rekebishwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2001.
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitungwa na Bunge ili kutekeleza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ibara ya 132 (4) ambayo inasema kuwa Bunge litatunga Sheria itakayoainisha misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakayozingatiwa na watu wote wanaoshika nafasi za madaraka zitakazotajwa na Bunge.
Pia, katika Ibara 132 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ililipa Bunge mamlaka ya kuweka misingi ya Maadili ambayo:(a) Itafafanua nafasi za madaraka ambazo watu wenye kushika nafasi hizo watahusika nayo;(b) Itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao;(c) Itapiga marufuku mienendo na tabia inay opelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii.
Na kifungu (d) Itafafanua adhabu zinazoweza kutolewa kwa kuvunja misingi ya maadili;(e) Itaelekeza taratibu, madaraka na desturi zitakazofuatwa ili kuhakikisha utekelezaji wa maadili;(f ) Itaweka masharti mengine yoyote yanayofaa au ambayo ni muhimu kwa madhumuni ya kukuza na kudumisha ua minifu, uwazi, kutopendelea na uadilifu katika shughuli za umma na kwa ajili ya kulinda fedha na mali nyingi
Hata hivyo kayika kuleta ufanisi katiika kukuza uchumi wan chi inaelezwa ni muhimu kwa viongozi waliopewa jukumu la kuongoza umma, kuwa na maadili katika utendaji wao wa kazi za kila siku wanazozifanya kwa manufaa ya wananchi, lengo kuu ni kuwaongoza wananchi katika misingi ya haki na usawa katika kuwaletea maendeleo.