Kulwa Mzee – Dar Es Salaam
VIGOGO sita wa Kampuni ya Viettel Tanzania, akiwemo Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46), wanaokabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya zaidi ya Sh bilioni 78 wanaendelea kusota rumande hadi Mei 4 mwaka huu.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa njia ya Mahakama Mtandao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kesi hiyo inatajwa na upelelezi haujakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 4 mwaka huu kwa kutajwa na washtakiwa wanaendelea kuwa rumande.
Mbali na Nguyen washtakiwa wengine ni Nguyen Minh (40) na Vu Tiep wote ni mameneja wa Halotel, Ha Than (39) ambaye Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Halotel, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel.
Awali waliposomewa mashtaka Machi 27, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ilishawahi washtakiwa hao kati ya Juni 8,2017 na Machi 26,2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida.
Inadaiwa kati ya Juni 8,2017 na Machi 26,2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi kwa pamoja walitumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.
Pia inadai kati ya Julai 7,2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.
Katika mashtaka ya nne, inadaiwa washtakiwa hao walikwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Viettel Tanzania na Vietnam kinyume na sheria.
Inadaiwa Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo hayo kwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA walisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 75.
Pia wanadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh bilioni 3.03.
Katika mashtaka ya saba washitakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.
Kampuni ya Viettel Tanzania inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu ilitakatisha Sh bilioni 3.03 na mashtaka ya tisa na 10, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 75 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.