Francis Godwin, Iringa
VIFAA mbali mbali vyenye thamani ya Sh bilioni 1.2 vimetolewa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Iringa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili katika hifadhi hiyo.
Mratibu wa mradi wa mradi wa Kuendeleza Utalii Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (REGROW), Saanya Saenea, alisema juzi wakati wa hafla ya kuzindua vifaa hivyo iliyofanyika katika ofisi za hifadhi ya Ruaha mkoani hapa alisema ifaa hivyo vimetolewa kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ulinzi kwenye hifadhi hiyo.
Alisema mradi huo wa Regrow umeanza kazi kwa kasi na kupitia vitendea kazi mbali mbali vya ulinzi ambavyo vimetolewa wanauhakika ulinzi utaimarishwa zaidi kwenye hifadhi hiyo .
Pia alisema kupitia mradi huo watahakikisha wanaweka mikakati ya kunusuru kukauka kwa mto Ruaha mkuu ambao ni mto tegemeo kubwa kwa wanyama hivyo wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo watajengewa mabwawa na elimu ya umwagiliaji wenye tija itatolewa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda alisema wizara yake imejiwekea kipaumbele cha kuboresha miundo mbinu ya hifadhi za ukanda wa kusini na zile mpya zilizoanzishwa hivi karibuni na kuzitangaza ulimwenguni kote.
Alisema uimarishaji wa miundo mbinu katika hifadhi utaongeza kasi kubwa ya watalii nchini na kuwa kazi kubwa ni kuona hifadhi hizo zinaendelea kutangazwa zaidi ndani na nje na utangazaji wake uwe ni ule wenye tija .
Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA ) Kanda ya Kusini, Dk.Christopher Timbuka , alisema ujio wa mradi wa REGROW umetokana na changamoto ambazo hifadhi za kusini zilikuwa zikikabiliwa nazo .
Alisema miundombinu kuwa mibovu na watalii kushindwa kufika katika hifadhi hivyo mradi huo utawezesha kufungua utalii nyanda za kusini .
Alisema ujio wa mradi huo ambao unaanza kazi utasaidia kuongeza idadi ya watalii na kuongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 400 vilivyopo na kuongezeka zaidi ili watalii kuweza kupata maeneo ya kufikia .
Alisema kupitia mradi huo ulinzi ulinzi didhi ya ujangili kwenye hifadhi utapungua zaidi kutokana na mradi huo kuwezesha vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi .