Na MWANDISHI WETU
UTAJIRI ni neno la kawaida, lakini lenye maana zaidi ya moja. Kimsingi utajiri ni neno mtambuka ambalo linategemea jamii gani na wakati gani linazungumzwa.
Utajiri si fedha mtu anazokusanya. Ni fedha ambazo huziweka zikafanya kazi. Tamaduni zetu tangu awali zimefanya jamii nyingi kuhifadhi fedha ndani kwenye vyungu, magodoro na hata vibubu. Njia hizi zimekuwa zikibadilika taratibu sawa na ukuaji wa elimu na teknolojia katika jamii.
Wawekaji akiba ambao hutaka kuwa wawekezaji, hufikiri juu ya kuchagua, kupanga na kutathmini juu ya uwekezaji wao.
Hapa Tanzania unaweza kuwekeza fedha katika masoko ya fedha na mitaji.
UTT AMIS ni Taasisi ya Serikali yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika usimamizi wa mali kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Shughuli za taasisi hii zinaratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania.
Ofisa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Rahim Mwanga, anasema: “Ukiwa na akiba ya fedha unatakiwa kuiwekeza. Uwekezaji ni dhana pana, kwa mfano, mwingine anataka kununua kiwanja, mwingine aanzishe biashara, mwingine ampeleke mtoto shule, mwingine akasome, lengo likiwa ni ile fedha ya akiba ilete matokeo chanya kwake.
Hata hivyo, inatakiwa ieleweke kwamba kuna muda kati ya kuweka akiba, kuwekeza na kutimiza lengo.
Kwa mfano, mtu anataka kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya mtoto wake mwenye mwaka mmoja sasa, hivyo kuna miaka miwili au mitatu baadaye aanze elimu ya awali.
Mkurugenzi huyo wa masoko anasema: "Tunapozungumzia masoko ya mitaji mfano wake ni Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika soko hili kuna kampuni zimejiorodhesha kutafuta mitaji kwa kuuza baadhi ya hisa, kwa hiyo ni sehemu mojawapo ambayo watu wanaweza kwenda kuwekeza.
Sehemu nyingine ni katika masoko ya fedha, hapa kuna akaunti za muda maalumu (fixed deposit accounts) na akaunti sizizo za muda maalumu (call deposit accounts).
Pia kuna dhamana za Serikali (treasury bills) na (treasury bonds). Hizi treasury bills ni dhamana za muda mfupi na treasury bonds ni dhamana za muda mrefu. Sehemu hizi mtu mmoja mmoja anaweza kwenda na kuwekeza, lakini kuna changamoto za kuweza kuyafikia hayo masoko kwa mtu mmoja mmoja.
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni fursa inayomwezesha mtu mmoja mmoja au taasisi, kampuni kuwekeza rasilimali fedha zao kupitia UTT AMIS ambao kazi yao kubwa ni kuwekeza kwa niaba yao.
Aidha, Mwanga anasema: "UTT AMIS inawekeza katika sehemu mbili kubwa ambazo ni masoko ya fedha na masoko ya mitaji. Faida inayopatikana katika kuwekeza masoko ndiyo inayogawanywa kwa kila aliyewekeza.
Katika hatua hiyo sehemu ya uwekezaji aliyonayo mwekezaji katika mfuko wa uwekezaji wa pamoja ndiyo inayoitwa kipande (unit). Moja ya faida kubwa ambayo watu wanaweza kuipata kwa kujiunga na mifuko ya uwekezaji wa pamoja badala ya kujiunga mmoja mmoja, ni kwamba faida ya ukuaji wa fedha inayopatikana ni faida shindani zaidi na nzuri kuliko mtu akienda mmoja mmoja katika masoko ya fedha na mitaji.
Kwa mwaka benki huwa zinatoa riba ya kuanzia asilimia tatu hadi saba kulingana na kiwango walichopanga, lakini kama ukiwekeza kiasi kikubwa katika benki, unakuwa katika nafasi ya kupata riba kubwa, kwa mfano kuanzia milioni 500 na kuendelea unaweza kupata riba ya kuanzia asilimia 7 hadi18, kulingana na kiwango cha fedha, hali ya kiuchumi ya wakati husika na mahitaji ya benki.
"Hapo ndipo inapokuja faida ya dhana ya uwekezaji wa pamoja, kwamba kila mtu kutokana na uwezo wake anaweza kupeleka fedha katika mfuko.
Kwa ujumla, UTT AMIS ina mifuko mitano ya uwekezaji wa pamoja. Kuna mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Watoto na Ukwasi. Mifuko hii ipo kwa ajili ya kukidhi mahitaji tofauti ya kijamii.
Mpango wa gawio
Katika mpango wa gawio, mfuko wa kujikimu unatoa gawio kila baada ya miezi mitatu au kila baada ya mwaka. Ili mwekezaji apate gawio kila baada ya miezi mitatu, kiwango cha chini kabisa cha kuwekeza ni Sh milioni mbili na ili apate gawio mara moja kwa mwaka, kiwango cha chini kabisa kuwekeza ni Sh milioni moja.