26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAZO KUCHANGAMKIA FURSA YA MRADI MPYA WA MAJI

Na MWANDISHI WETU


MIONGONI mwa viashiria vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuimarika kwa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji ambayo hutumika zaidi katika kusaidia uanzishaji na uendelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo viwanda.

Kwa sasa Tanzania inajielekeza kuwa Taifa la Viwanda. Ili kufanikisha azma hii,ni muhimu sekta ya maji kupewa uzito wa kipekee kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda.

Kwa kutambua umuhimu wake, Serikali imelazimika kubuni miradi mikubwa ya uimarishaji wa usambazaji maji katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa uboreshaji huduma ya majisafi katika eneo la Wazo jijini Dar es Salaam, mradi unaotegemewa utakapokamilika utawezesha kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Wakizungumzia mradi huu, baadhi ya wananchi wa eneo la Wazo wanasema mradi huo mpya mbali na kumaliza tatizo la maji, pia utasaidia kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kwani wananchi watatumia muda mwingi kufanya shughuli za kujiingizia kipato badala ya kutumia muda
mwingi kutafuta maji.

Mmoja wa wananchi hao, Nurdin Kambi,anasema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakisubiri mradi huo, hivyo uamuzi uliofanywa na Serikali umekuja wakati mwafaka na kutaka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Anasema shughuli za kuanzisha viwanda vidogo itafanikiwa kwa kuwa kutakuwepo na uhakika wa huduma ya maji ya kutosha na hivyo kuchochea uanzishaji wa miradi ya kiuchumi inayohitaji zaidi upatikanaji wa maji.

Mwananchi mwingine wa eneo hilo, Shufaa Adam, anasema kwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia pia kutekeleza kwa vitendo kampeni ya ‘Mama tua ndoo kichwani’, kwani wanawake wengi wataweza kuchota maji katika maeneo jirani na makazi yao tofauti na ilivyokuwa awali ambapo
walilazimika kutembelea umbali mrefu kutafuta maji.

Aidha, anasema wanawake wengi walikuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji, huku wakiacha kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji maji hivyo kwa hatua hiyo ya kuanza kwa mradi huo, ni wazi wataongeza ufanisi katika shughuli zao za ujasiriamali na kujiongezea zaidi kipato na
kukabiliana na ugumu wa maisha.

Shufaa anasema mradi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa eneo la Wazo hasa kutokana na eneo hilo kuwa na wakazi wengi, walianzisha makazi mapya hivyo kukosekana kwa maji pia ilikuwa changamoto kubwa katika harakati zao za kufanya shughuli za ujenzi.

Akizungumzia Mradi huo wa Uboreshaji huduma ya usambazaji maji eneo la Wazo, Mkurugenzi wa huduma za Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(Dawasa), Mhandisi Romanus Mwangi'ngo,  anasema mradi huo utajumuisha ujenzi wa tenki la maji la ardhini (sump) lenye
uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 1,140.

Pia kufanyika ujenzi wa jengo la kuhifadhi pampu na ufungaji wa pampu nne zenye nguvu ya ili kuweza kusukuma maji kutoka katika tenki la ardhini hadi katika tenki la kuhifadhi maji, ujenzi wa tenki jipya la
maji lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 6,000 (lita milioni sita).

Aidha, Mhandisi huyo anasema kazi nyingine itakayofanyika ni ulazaji wa bomba la chuma lenye kipenyo cha inchi 16 (DN400) lenye urefu wa kilomita 3, litakalosafirisha maji kutoka kwenye matoleo (offtake)
katika bomba kuu lililopo la inchi 54 (DN1350) hadi kwenye tenki jipya. Pia ubadilishaji na ukarabati wa mabomba katika matoleo (offtake) yaliyopo.

Anasema pia kazi ya ulazaji wa mabomba ya ugawaji maji mitaani ya mpira mgumu (HDPE) yaliyo na ukubwa wa kati ya inch nane (DN200) na inchi tatu (DN 90) kwa umbali wa jumla ya kilomita nane ili kuweza kuunganisha mfumo wa maji uliopo na tenki jipya lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo elfu sita (lita milioni sita)

Pia kutafanyika kazi ya ufungaji wa mita kubwa ya kupima wingi na msukumo wa maji yanayoingia mitaani, ufungaji wa valvu za kudhibiti msukumo wa maji katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, mradi huo pia utahusisha ufungaji wa eneo maalumu kwa ajili ya kuhudumia magari ya zimamoto sambamba na ukarabati wa matoleo katika bomba kuu maeneo ya ugawaji maji (off take) na kufanya maunganisho kati ya tenki jipya na mtandao wa maji uliopo.

Ansema pia kazi nyingine itakayofanyika ni pamoja na ufungaji wa mtambo wa kisasa wa kusoma mita (wireless telemetry meter reading) na ufungaji wa kifaa maalumu cha kupokea taarifa za mita. Kifaa hicho
kitafungwa katika ofisi za Shirika la Majisafi na Majitaka Dar esSalaam (Dawasco)makao makuu.

Aidha, akizungumzia kwa ujumla wake kuhusu mradi wa uboreshaji wa huduma ya ugawaji maji katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, Mwangi'ngo anasema mradi huo ulianza rasmi Machi mwaka jana.

Pia mradi huu unahusisha uandaajiwa michoro, ujenzi wa matenki, ununuzi na ufungaji wa pampu kubwa za kusukuma maji, uagizaji naulazaji wa mabomba makubwa ya ugawaji maji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji mitaani.

Ameyataja maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni pamoja na Salasala, Goba, Goba, Bunju, Wazo, Makongo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo na ukanda maalumu wa EPZA ambayo kimsingi yanahudumiwa na mtambo wa Ruvun Chini.

Aidha, pamoja na utekelezaji katika maeneo yaliyotajwa, eneo jingine litakalonufaika na mradi ni lile lililopo kati ya Mbezi Luis na Kiluvya mkoani Pwani, ambalo huhudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu.

Hivyo, kutokana na kuwa baadhi ya maeneo chini ya mradi huu kuwa katika miinuko, matanki mapya yatajengwa sehemu za miinuko na pampu maalumuzilizo na nguvu zitafungwa ili kuweza kusukuma maji hadi katika maeneo ya miinuko, yatakapojengwa matanki.

Aidha, ili kuhakikisha kuwa pampu hizo zinapata umeme wa kutosha na zinafanya kazi kwa uwezo unaokusudiwa, Dawasa imekuwa ikifanya mawasilano ya karibu na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kwa upande wao, waweze kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha unapatikana. Tayari mafundi wa Tanesco wameshatembelea maeneo yote ambapo pampu zitafungwa na wameahidi kupeleka huduma stahiki katika maeneo husika.

Anasema mradi huo unaotekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia DAWASA na unajengwa na Kampuni kutoka nchini India ya Jain Irrigation chini ya usimamizi wa Kampuni ya ushauri ya WAPCOS kwa gharama ya Dola zaMarekani 32,927,222.45.

Ofisa Mahusiano na Jamii wa Mamlaka hiyo, Mecktridis Mdaku, anasema mradi huo kwa ujumla wake utakuwa na faida nyingi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wa kawaida na wenye viwanda na biashara katika eneo la mradi wanapata huduma ya maji bora zaidi hasa baada ya maji kuongezeka
baada ya upanuzi wa mitambo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Faida nyingine ni kuweka mitandao ya maji katika maeneo ambayo hayakuwa na mtandao rasmi wa maji; kwa kufanya hivi, mradi utawezesha maji yagawanywe kwa ufanisi zaidi. Chini ya mradi huu, miundombinu chakavu itakarabatiwa, hivyo kwa ujumla huduma ya maji itakuwa bora na
ya uhakika zaidi.

Mdaku anasema pia wananchi wataombwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi iweze kwenda kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa na kuwezesha kunufaika na mradi huo mkubwa ambao umeigharimu Serikali fedha nyingi.

Sehemu maalumu ambapo bomba kuu jipya kutoka Ruvu Chini lenye kipenyo
cha mita 1.8 limeunganishwa na bomba kuu la zamani la zege ambapo ni
sehemu ya mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles