30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UWEKEZAJI KWENYE MADINI WAZIDI KUKUA

Gari la kubeba makaa ya Mawe katika mgodi wa Ngaka likimwaga makaa sehemu maalum kutoka mgodini kabla ya kusagwa
Gari la kubeba makaa ya Mawe katika mgodi wa Ngaka likimwaga makaa sehemu maalum kutoka mgodini kabla ya kusagwa.

Na LEONARD MANG’OHA,


 

KUANZIA Septemba mwaka 2008 hadi 2009, dunia ilikumbwa na mtikisiko wa uchumi ambao ulisababisha baadhi ya mabenki kujiendesha kwa hasara, huku baadhi ya makampuni yakipunguza uzalishaji.

Baadhi ya kampuni zikiwamo za magari na nyinginezo zikilazimika kupunguza wafanyakazi ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha katika ulipaji wa mishahara na kupunguza gharama za uendeshaji.

Mtikisiko huo wa uchumi uliziathiri sekta nyingi za uchumi duniani kote ambapo pia ulishuhudiwa makampuni ya mafuta yakilazimika kushusha bei ya mafuta ili kuendana na hali halisi ya soko kwa wakati huo.

Miongoni mwa soko lililotikisika kutokana na mtikisiko huo wa uchumi wa dunia, ni lile la madini ambapo bei ya bidhaa hiyo iliporomoka kwa kasi ya ajabu.

Kushuka kwa bei ya madini, dunia ilishuhudia sekta ya madini hasa soko la dhahabu imeonekana kuzorota kiasi cha uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ikilinganishwa na hali ivyokuwa hapo awali.

Bei ya dhahabu inaelezwa kushuka kutoka Dola za Marekani kati ya 1,700 (zaidi ya Sh milioni 3.7) na 1,800 (Sh milioni 3.9) mwaka 2008 hadi Dola 1,300 (zaidi ya Sh milioni 2.8) kwa wakia moja (sawa na gramu 28.3).

Wakati hali ikiwa hivyo, katika soko la dunia bei ya bidhaa hiyo kwa sasa nchini ni Dola za Merekani 1,151.36 sawa zaidi ya Sh milioni 2.5 kwa wakia moja, huku madini aina ya fedha yakiuzwa kwa dola 16.44 (zaidi ya Sh 35,000) kwa kipimo hicho hicho.

Hivi karibuni, MTANZANIA lilizungumza na Kaimu Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini, Julius Sarota, ambapo anasema kuwa kushuka kwa bei hiyo kumesababishwa na mdororo wa uchumi ulioikumba dunia kati ya mwaka 2008 na 2009.

Sarota anasema hali hiyo imezikumba pia aina nyingine za madini ikiwamo almasi, shaba na madini mengine lakini Tanzania imepata mtikisiko mkubwa katika madini ya dhahabu kutokana na kuwa ndiyo yamekuwa yakizalishwa kwa wingi nchini ikilinganishwa na aina nyingine za madini.

“Kutokana na hali hiyo, wawekezaji wengi wameshindwa kuendelea na utafiti wa madini sehemu mbalimbali kutokana na mitaji yao kutegemea fedha kutokana na soko la bidhaa hizo za madini,” alisema.

Anasema kutokana na kushuka kwa bei ya madini, kumesababisha baadhi ya wawekezaji kusitisha shughuli zao kusubiri bei hiyo iimarike kabla ya kuendelea na shughuli za utafiti na uchimbaji madini.

Sarota anasema hadi wakati wa mdororo huo, tayari kulikuwa na makampuni kadhaa yaliyokuwa yamefikia hatua nzuri ambapo tayari yangekuwa yanaendelea na uzalishaji, lakini yameshindwa kwa kuhofia hasara.

Baadhi ya miradi iliyositishwa kuendelea na tafiti za madini ni pamoja na Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Nyakafuru (Geita) Ndutwa (Mwanza) sambamba na mradi wa machimbo ya madini aina ya Nikeli uliopo Kabanga, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Kusimama kwa miradi hiyo ni wazi  kuwa kumeleta athari za kiuchumi katika jamii, ikiwa ni pamoja na kukosa ajira ambazo zingetokana na miradi hiyo.

Mbali na miradi mikubwa ya Bulyanhulu, Geita, North Mara na Acacia, kwa sasa Tanzania imekuwa na baadhi ya miradi mipya ya kati ambayo iko katika hatua nzuri za ujenzi, huku baadhi ikiwa tayari imeanza uchimbaji.

Kwa mujibu wa Sarota, migodi iliyo katika hatua nzuri ni MGM ulioko Musoma, Mkoa wa Mara ambao uko katika hatua za ujenzi na unategemewa kuanza uchimbaji mwishoni mwa mwaka huu, lakini pia kuna migodi miwili ya dhahabu iliyoko Singida ambayo iko katika hatua nzuri.

“Mgodi ambao umeanza uzalishaji hadi sasa ni Cata mining ambao uko Musoma, lakini mwelekeo wa migodi hii yote pamoja na ile ya Singida si mbaya  na tunaamini itaanza uzalishaji mapema kabla mwaka huu haujakwisha,” alisema Sarota.

Kwa mujibu wa Idara ya Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, hadi sasa Tanzania ina leseni hai za wawekezaji wadogo 34,299, leseni za utafiti 2,758, huku wawekezaji wa kati na wakubwa ni 393.

Jumla ya leseni za wachimbaji wadogo zilizotolewa tangu Julai mosi mwaka jana ni 2,225, leseni za utafiti ni 193 na leseni zilizotolewa kwa wawekezaji wa kati na wakubwa ni sita.

Leseni zilizofutwa kati ya Julai mosi na Desemba 28, mwaka jana ni 1,705 za wawekezaji wadogo, leseni za utafiti zilizofutwa ni 72, huku leseni za wawekezaji wakubwa na wa kati hakuna iliyofutwa katika kipindi hicho.

[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles