27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UVUVI SEKTA YENYE FURSA ILIYOSAHAULIKA

Na LEONARD MANG’OHA


PAMOJA na kuwa na utajiri wa eneo kubwa la maji lenye fursa kubwa ya uvuvi, Tanzania bado haijaweza kutumia ipasavyo fursa hii.

Hii inatokana na sekta hiyo kuendelea kutegemea wavuvi wadogo wanaotumia dhana duni ambazo ni vigumu kwenda katika maeneo ya kina kirefu.

Pamoja na kuwa na ukanda wa pwani ya bahari wenye urefu wa kilomita 1,424 wenye eneo la maji ya kitaifa (Territorial Sea) lenye ukubwa wa kilomita za mraba 64,000 na eneo la Bahari  Kuu lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000 kushindwa kuwa na viwanda vikubwa vya uchakataji na usindikaji wa samaki na mazao yake.

Kwa uvuvi wa maji baridi, Tanzania ina maziwa makubwa matatu ambayo ni Victoria, Tanganyika na Nyasa ambayo kwa ujumla yana kilomita za mraba 54,277 na maziwa ya kati na madogo yapatayo 29 mito na maeneo oevu 9.

Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka 2013/2014, kulikuwa na wavuvi wadogo 183,341 wakiongezeka kutoka 182,741 mwaka uliotangulia, huku wananchi zaidi ya milioni nne wakitegemea shughuli za uvuvi ikiwemo biashara ya samaki, uchakataji wa mazao ya uvuvi, utengenezaji wa zana na vyombo vya uvuvi na kujipatia kipato.

Miongoni mwa changamoto ambazo mara kadhaa zimekuwa zikitajwa kukwamisha ukuaji wa sekta hiyo ni pamoja na kutopata fedha za kutosha na kwa wakati ili kutekeleza majukumu yanayoainishwa kwenye mpango kazi wa Wizara, uwekezaji mdogo katika sekta hiyo.

Kutopatikana kwa mikopo ya kutosha na yenye masharti nafuu kwa wafugaji na wavuvi, gharama kubwa za zana za uvuvi, uhaba wa maofisa ugani wa uvuvi ikilinganishwa na mahitaji, ni baadhi ya changamoto katika sekta ya uvuvi.

Changamoto nyingine ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika la mazao ya uvuvi, ushiriki mdogo wa wadau katika kudhibiti uvuvi na biashara haramu ya samaki na mazao ya uvuvi pamoja na elimu duni ya ufugaji bora na wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia katika shughuli za uvuvi.

Kuwapo kwa changamoto nyingi katika sekta hii kunaleta umuhimu wa Serikali kuweka sera madhubuti itakayoleta mageuzi makubwa ya uvuvi ili kulipatia Taifa mapato ya kutosha na kuchangia kulingana ukubwa wa sekta husika.

Kuimarishwa uvuvi kutasaidia kujenga jamii yenye afya njema kwa kuhakikisha upatikanaji wa kitoweo cha samaki ambacho ni miongoni mwa vyakula bora na vinavyojenga afya ya mwili na akili.

Kuimarishwa kwa uvuvi kutaongeza ajira kwa wananchi kwa kuwaajiri moja kwa moja na na wengine kujiajiri kupitia fursa zitakazojitokeza kupitia sekta hiyo.

Ikiwa shughuli za uvuvi zitaimarika, ni wazi kuwa itafunua fursa na usafirishaji kwenda kuchukua samaki na kuwapeleka viwandani hivyo kutoa ajira kwa madereva na wale watakaoajiriwa katika viwanda vya uchakataji na usindikaji minofu ya samaki.

Dk. Berno Mnembuka ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA). Anasema kama jamii inavyoamini kuwa ardhi ni hazina na inapaswa kuwa hivyo kwenye maji hivyo watawala hawana budi kuhakikisha vyanzo vya maji vinatumika kikamilifu kukuza uchumi wa nchi.

Anasema bado kiwango cha uvuvi ni kidogo ukilinganisha na vyanzo vya maji vilivyopo ambavyo ukubwa wake ni zaidi ya kilomita 343,000 za mraba  vikijumuisha eneo la bahari, maziwa, mito na maeneo oevu.

Kwa mtazamo wake, anaamini wavuvi wanapaswa kuwezeshwa kwa kupewa ruzuku kama ilivyo kwenye sekta ya kilimo cha mazao ambapo wakulima hupata ruzuku katika pembejeo.

Anasema wavuvi wakiwezeshwa wataweza kufika katika maeneo ya maji marefu ambako wanaweza kupata mazao makubwa ya samaki na kuepukana na uvuvi haramu ambao hufanywa ili kujikimu kimaisha.

“Uvuvi haramu lazima upigwe vita kisayansi si kwa kutumia nguvu. Kwa sababu sasa hivi nyenzo za uvuvi bei yake iko juu sana, wanapaswa wakopeshwe kwa vikundi na wapewe ruzuku,” anasema Dk. Mnembuka.

Anasema hakuna mwananchi ambaye atapinga au kuendelea na uvuvi haramu ikiwa zitawekwa taratibu zitakazomwezesha kuvua huku akilinda rasilimali hiyo kwani itakuwa ni faida kwao ambapo wataweza kuvua kwa muda mrefu zaidi.

Dk. Mnembuka anasema umefika wakati wa kuhama kutegemea vyanzo vya asili kuvua na badala yake kuanzishwa mfumo wa ufugaji wa samaki ambao utaleta tija zaidi kwa wafugaji wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Anasema sera ya matumizi ya maji inapaswa kufanyiwa mabadiliko kuruhusu watu kutumia maji hayo kufuga samaki, sekta anayoeleza kuwa inaweza kuwa na manufaa makubwa endapo itapewa nafasi.

Anatolea mfano nchi ya Norway ambayo licha ya kuwa inachimba mafuta, pia imepata mafanikio kupitia ufugaji samaki na Denmark ambayo pia imepata mafanikio makubwa baada ya kuamua kukuza ufugaji samaki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles