Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, asili yake na wazazi wake kisiasa ni Chama cha ASP na hajawahi kufikiria kuunga mkono upinzani kama ambavyo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, anavyompakazia na kumchafua kisiasa.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, kutokana na matamshi ya Maalim Seif akiwa ziarani Mkoa wa Mjini Magharibi na kudai kuwa Samia anaunga mkono upinzani.
Shaka alisema si jambo la kutarajiwa kwa Maalim Seif ajivike joho la uzushi na uongo na kutoa madai yasiyokuwa na mashiko.
Alisema madai yake kuwa Makunduchi si eneo la ASP na kwa asili ni upinzani si kweli, kwa sababu katika uchaguzi wa mwisho mwaka 1963, Sheikh Idris Abdul Wakil wa ASP, alimshinda Sheikh Ameir Tajo wa ZPP katika kiti cha uwakilishi katika Bunge la Legco.
“Samia ni mzaliwa wa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na aliwahi kuwa mwakilishi wa jimbo hilo katika Baraza la Wawakilishi, Zanzibar. Maalim Seif amejaribu kupandikiza chuki na kuwagawa Wazanzibari lakini ameshindwa. Ametaka urais tangu mwaka 1984 hadi 2015 ameukosa,” alisema.
Shaka alisema anaelewa Maalim Seif anawachukia wananchi wa Makunduchi kutokana na kuwania urais na Mzee Wakil akamshinda, akamvua cheo cha Waziri Kiongozi kisha Serikali yake ikamuweka kuzuizini kwa muda wa miaka mitatu.
“Anatapatapa na kutaka kueneza siasa za mgawanyiko ili akubalike Makunduchi. Wananchi wa Mkoa wa Kusini hawajasahau dhihaka ya kuitwa ng’ombe kwa ushabiki wa Maalim Seif aliyemchafua hayati Mzee Wakil,” alisema.
Pia alimtaka asimpakazie Samia kuwa anataka kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2020 wakati sasa hivi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Alifukuzwa mwaka 1987 kwa jaribio la kuipasua CCM. Mwalimu Julius Nyerere alimbeba Maalim Seif, lakini aliambiwa huyo ni mzito humuwezi akabisha, mwishowe alimfukuza,” alisema.
Shaka alisema hata Rais wa zamani wa Zanzibar, Aboud Jumbe, alipoaswa na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Ramadhani Haji Faki, asimteue alibisha na matokeo yake Maalim Seif alimgeuka na kusababisha akavuliwa nyadhifa zote mwaka 1984.
“Maalim Seif ni mgeni Zanzibar hata uraia wake bado una utata, aliwahi kutakiwa ashiriki mdahalo wa asili yake akaukimbia, hatutaki kusema ila tukisema na kutaja historia yake atakimbia, asijilinganishe na Mama Samia ni zao la ASP na atafia CCM hata yeye ni CUF upepo, lakini ni CCM masilahi ndiyo maana tangu alipofukuzwa hajarudisha kadi yetu,” alisema.