33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS LULA AJISALIMISHA GEREZANI

BRASILIA, BRAZIL


RAIS wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva amejisalimisha katika gereza la Curitiba kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 baada ya awali kukwepa kufanya hivyo.

Siku ya Ijumaa Mahakama ilimhukumu kwa mashitaka ya ufisadi, lakini alikimbilia katika makao makuu ya muungano wa wafanyakazi wafua vyuma mjini Sao Paolo, ambako wafuasi wake walishinikiza kutojisalimisha.

Matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni nchini hapa yameonesha akiwasili kwa helikopta katika Makao Makuu ya Polisi katika mji wa Curibita, kusini mwa Brazil.

Katika hotuba iliyojaa hisia aliyoitoa mjini Sao Bernardo do Campo kabla ya kujisalimisha, Lula amejitaja kuwa raia aliyeghadhibishwa na mashitaka ya kutungwa ya ufisadi.

Alimshutumu Jaji Sergio Moro kuwa alidanganya kwamba alipewa jengo na kampuni moja ya ujenzi kama rushwa.

Helikopta iliyokuwa imembeba ilipotua, waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje walifyatua fataki, huku polisi nao wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Kabla ya kuwasili Curitiba, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 aliondoka Sao Paolo akiwa amezingirwa na walinzi.

Lula, ambaye alipenya katikati ya msitu wa wafuasi wake waliokuwa wanamzuia asiondoke na kuingia katika gari la polisi, anasisitiza kuwa mashitaka dhidi yake yalichochewa kisiasa.

Lula alikutwa na hatia ya kupokea rushwa kutoka kwenye kampuni kubwa ya ujenzi, ili iweze kupata mikataba ya serikali.

Makosa ya rushwa ni suala linaloweza kwa kiasi kikubwa kuhitimisha maisha yake kisiasa na kuondoa matumaini ya kurudi tena madarakani.

Licha ya kashfa zinazomkabili, Lula anaongoza kwa umaarufu kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya wapiga kura kuelekea uchaguzi wa rais unoatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Amejaribu kuchelewesha hukumu dhidi yake kwa kukataa rufaa mara kadhaa katika mahakama ya juu bila ya mafanikio.

Siku ya Ijumaa, jaji wa Mahakama Kuu alikuwa amemtaka Lula kujisalimisha kwa polisi ifikapo saa 11 jioni lakini alikiuka muda huo.

Jumamosi, maelfu ya wafuasi wake walimsihi asijisalimishe na kumzuia kuondoka kutoka majengo ya chama cha wafanyakazi wafua vyuma.

Baada ya kukamatwa na polisi, maandamano kutoka kwa wafuasi wake na sherehe kutoka kwa wanaompinga zilishuhudiwa katika miji ya Brasilia, Rio de Janeiro, Sao Paulo na miji mingine.

Wapinzani wake wanamuona kuwa ndiye anawajibika kwa misururu ya kashfa za ufisadi zinazoikabili siasa za Brazil.

Lakini wafuasi wake wamesononeka kwa kuondoka katika ulingo wa siasa wa kiongozi wanayemkumbuka kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka umasikini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles