KUNA baadhi ya nchi duniani zinastaajabisha kutokana na namna zinavyoendesha sera za utawala wa Serikali zao, kwa mujibu wa katiba inayosimamia nyanja mbalimbali kutegemeana na mtazamo wa chama kinachotawala na kiongozi wao mkuu.
Mojawapo ya nchi ambayo nimewahi kuiandika mara kadhaa katika safu hii ni Taifa la Uturuki, lenye siasa zilizojaa hamkani na mgawanyiko mkubwa unaochagizwa na Rais Recep Tayyip Erdogan na chama chake cha AKP kwa kuwa kila baada ya muda lazima kitaibuka kioja kipya nchini humo kutokana na sera shaghalabaghala zilizokosa mwelekeo.
Limeibuka jambo jipya ambalo limezua taharuki ya maandamano ya kupinga Muswada uliopendekezwa uliopigiwa kura katika Bunge lao.
Songombingo mpya katika mfululizo wa hamkani zinazolikumba Taifa hilo imesababishwa na Muswada uliopendekeza kuwa wanaume waliowaingilia kimwili wasichana walio chini ya umri unaotambulika kisheria kuridhia kujamiiana, hawatachukuliwa hatua za kisheria endapo watawaoa wasichana hao waliowabaka kwa mapendekezo ya Serikali inayodai kuwa imewasilisha Muswada huo ili kukabiliana na wimbi la ndoa za wasichana wadogo, lakini wanaopinga Muswada huo wanadai ni uhalalishaji wa ubakaji.
Waandamanaji walioingia mitaani katika miji ya Istanbul, Izmir na Trabzon wamekuja juu na kuapa kuwa hawakubaliani na Muswada huo na kwamba wataendelea kuupinga vikali hadi uondolewe kwani kupitishwa kwake kutawaachia huru wanaume wengine ambao tayari wanatumikia vifungo kama wakikubali kuwaoa waliowabaka.
Wanachopinga kwa mujibu wao ni kwamba ubakaji hauwezi kuhalalishwa wakikituhumu chama tawala kwa kuandamana na kupaza sauti: “AKP achilia mwili wangu!” Kwa mujibu wa sheria za Uturuki msichana aliye na umri chini ya miaka 18 ni mtoto ambaye haruhusiwi kujihusisha wala kushawishiwa kujamiiana kwa kuwa bado hana utashi wa kuamua juu ya jambo hilo.
Muswada huo umeligawa Taifa la Uturuki katika makundi mawili huku wazazi wengi hususani kinamama, wakiupinga kwa kuwa wanahisi ni uingiliaji wa malezi yao kwa binti zao na kupokwa haki ya kuwalea ipasavyo.
Si wazazi tu lakini hata jumuiya ya kimataifa imeoneshwa kukerwa na Muswada huo uliojaa utata kwani imemlazimu Waziri wa haki wa Uturuki Bekir Bozdag, kufafanua katika mkutano wa NATO ambao ni washirika muhimu wa usalama wa Taifa hilo kwamba Muswada huo hautawasamehe wabakaji ila umedhamiria kutatua tatizo la ndoa za utotoni zilizokubuhu hususani katika maeneo mengi ya vijijini, ambako baadhi ya wazazi wanaelekea kuufurahia mkakati huo unaopingwa vikali katika maeneo mengi ya mijini.
Wapinzani wa kisiasa wa AKP nao wamekuja juu na kumlazimu Waziri Mkuu Binali Yildirim kukiagiza chama cha AKP kufanya mazungumzo nao ili kufikia maridhiano kuhusiana na Muswada huo tatanishi wa sheria ya ubakaji. Inawezekana wakafikia maridhiano ya ndani lakini watakuwa na kazi kubwa kuridhisha jumuiya na mashirika ya kimataifa yanayosimamia haki za watoto ikiwamo UNICEF, iliyotatizwa na muswada huo kwa mantiki kuwa watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili kwa kuwaadhibu wanaowatendea uhalifu kwa kuwanyanyapaa kijinsia.
Lakini utata kamili uliosababisha sakata hilo ulianza miezi mitano iliyopita ambapo mahakama ya juu ya kikatiba ya Taifa hilo ilirekebisha kifungu kilichotamka kuwa kila tendo la kujamiiana na mtoto chini ya miaka 15 ni unyanyasaji wa kijinsia na kutaka kila kesi iangaliwe kwa jinsi ilivyo. Lakini kwa mujibu wa takwimu Uturuki ni mojawapo ya nchi zenye matukio mengi ya unyanyasaji wa kijnsia, kwa muda wa muongo mmoja uliopita asilimia 40 ya wanawake wamelalamikia kunyanyaswa kijinsia ikiwamo kubakwa huku kukiwa na ongezeko kubwa la idadi ya waliouawa baada ya kutendewa ukatili huo.
Licha ya Serikali kudai Muswada haudhamirii kuwasamehe waliobaka bali kutoa fursa kwa wasichana waliojamiiana chini ya miaka 18 kuhalalisha uhusiano wao na wenza wao ili kuzuia unyanyapaa wa kutengwa na jamii zao, ikitarajia kuungwa mkono maeneo ya vijijini ambako ndoa za utotoni ni nyingi lakini inavyoelekea wananchi wengi hawakubaliani na mtazamo huo licha ya Serikali kudai kuwa mbakaji anapofungwa mbakwaji anaachiwa mzigo wa malezi ya mtoto aliyezaliwa kutokana na uhalifu huo kwa kutopata malezi stahiki kutoka kwa baba.
Inawezekana Muswada wenyewe unapingwa zaidi kutokana na walioupendekeza kwani Rais Erdogan anayetoka katika chama cha AKP, anafahamika kwa historia ya misimamo yenye kauli tata.
Aliwahi kukaririwa akisema kuwa kamwe kwa asili huwezi kuwalinganisha wanawake na wanaume, akatamka tena kuwa mwanamke jasiri ni ambaye walau amezaa watoto watatu kwa njia ya kawaida ya uzazi na sio upasuaji, kisha akatamka tena kwamba mwanamke mjamzito anapwaya zaidi katika kutenda kazi ofisini ukichukulia kuwa kwa hulka wanawake ni legelege kuliko wanaume kutokana na jinsi walivyoumbwa, kwamba itawasaidia zaidi wakidai kuheshimiwa sawa na wanaume kuliko kudai usawa walionyimwa tangu kuumbwa kwa dunia.
Rais Erdogan ana hulka ya kutoa kauli tatanishi si tu kwa masuala ya kijinsia bali mambo mengine mengi kwani aliwahi kukaririwa akidai kuwa Waislamu walilivumbua Bara la America miaka 300 kabla ya madai ya Columbus kuvumbua Bara hilo.