24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

BARUA YA WAZI KWA DK. ALI MOHAMMED SHEIN

NA OMAR SAID SHAABAN


MHESHIMIWA Rais, kuna wakati wananchi wako tunapata taabu ya kujua ni njia gani sahihi ya kuwasiliana na wewe na kuhakikisha ujumbe tunaokusudia ukufike unakufika. Tabu hii inaongezeka hasa pale panapokuwa na jambo ambalo tunaamini utekelezaji wake au kwa namna unavyoliendesha na kulisimamia huwa linatokana na ushauri unaopewa na wasaidizi wako wakuu ndipo tunahisi hata tukiandika Barua za kuja hapo Ikulu ya Mnazi Mmoja(Vuga) uwezekano wa kuwekwa kapuni kabla ya kukufikia ni mkubwa sana. Hivyo njia pekee ya kufikisha ujumbe inakuwa ni hii ya barua ya wazi kama mhariri wa gazeti hatoamua kuacha kuichapisha.

Mheshimiwa Rais, hivi karibuni Serikali yako imepeleka Baraza la Wawakilishi Muswada wa Mafuta na Gesi ambao umepitishwa kwa kishindo na wajumbe wa baraza. Lengo la sheria hiyo kama ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi mbali mbali wa Serikali yako ni kuwa, hiyo ni hatua ya kuelekea kuipa mamlaka na uwezo Zanzibar wa kusimamia wenyewe rasilimali hii adimu ya mafuta na gesi.

Pia, viongozi mbali mbali ukiwamo na wewe mwenyewe Mheshimiwa Rais, mmekuwa mkiwaaminisha wananchi wa Zanzibar na wengi wenye maslahi na jambo hili kuwa uwezo na nguvu ya kutunga sheria hii unatokana kwanza na kile kinachoitwa “makubaliano ya viongozi wakuu wa Serikali mbili” kuliondoa suala la mafuta na gesi kwenye mambo ya Muungano, pili uwezo uliopewa Zanzibar na sheria namba 21 ya mwaka 2015 iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kifungu cha 2 kifungu kidogo cha 2 ambacho kwa mujibu wa tafsiri ya wasaidizi wako na yako mwenyewe inawezekana kuwa kinaelekeza na kuipa mamlaka Zanzibar kutunga sheria yake kuhusu usimamizi wa nishati ya mafuta na gesi.

Mheshimiwa Rais, kwanza nitangaze maslahi yangu kwenye jambo hili. Ya kwanza ni yale ya kisheria, nikiwa kama mwanasheria tena kiongozi kwenye kada hii ya sheria nina wajibu wa kikatiba, kimamlaka na kitaaluma kusimamia ulindwaji na usimamizi wa Katiba na sheria za nchi yetu.

Maslahi ya pili ni ya kizalendo, nikiwa kama mwananchi wa kawaida mwenye uchungu na Zanzibar yangu, napenda kuona Zanzibar ikisimamia rasilimali zake wenyewe hasa hii ya mafuta na gesi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na yale ya watu wake. Mimi ni mmoja ya Wazanzibari walio wengi tunaopenda kuona Zanzibar ikichimba na kunufaika na rasilimali hii hata kuanzia leo. Lakini bila ya kukiuka masharti ya Katiba ambayo wewe Mheshimiwa Rais umeapa kuilinda na sisi wananchi tunawajibu wa kusimamia na kuitetea.

Hivyo, ujumbe wangu usitafsiri hata kwa nukta kuwa mimi ni mpinzani wa jambo hili kuwa mikononi mwa Zanzibar. La hasha!

Mheshimiwa Rais, kwa heshima naomba nikueleze kuwa jaribio la Serikali yako na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na hatua yako ya kuweka saini muswada huo ili uwe sheria, ni uvunjaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo wewe umeapa kuilinda, lakini pia ni kinyume na maelekezo ya Sheria inayorejewa kama ndio chanzo cha mamlaka ya Zanzibar kutunga sheria yake. Nitaueleza ukweli huu hapa chini.

Mheshimiwa Rais, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nyongeza ya kwanza inataja suala la Mafuta na Gesi kama jambo la Muungano. Hivyo usimamizi wake pamoja na utungiwaji wake sheria kwa mujibu wa katiba zote mbili upo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Rais, hakuna mahali duniani kote ambapo suala lenye misingi yake kikatiba linaondolewa kwa “makubaliano ya viongozi wa wakuu wa Serikali”.

Ambacho viongozi wakuu wanaweza kufanya ni kuwa na wazo la kuliondoa jambo kutoka kwenye katiba lakini utekelezaji wake lazima ufanywe kwa utaratibu uliowekwa na katiba yenyewe wa kuibadilisha ama kwa Bunge kufanya marekebisho ya Katiba au wananchi kupiga kura juu ya kuwapo au kuondolewa jambo hilo kwenye katiba.

Kwa suala la mafuta na gesi kuondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano, nakubaliana na viongozi wakuu kukubaliana juu ya wazo hilo, lakini utekelezaji wake lazima uwe kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Rais, hoja inayotolewa ya kifungu cha 2 kifungu kidogo cha 2 cha Sheria ya Mafuta iliyopitishwa na Bunge kama ndio mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi kutunga sheria inayohusu mafuta nayo ni dhaifu sana na inakosa misingi ya kikatiba. Nitajaribu kufafanua kwa kutumia sheria yenyewe tajwa, Katiba ya Muungano na sheria nyingine tulizozitunga wenyewe.

Mheshimiwa Rais, Kwenye sheria hii, kifungu cha 2 kifungu kidogo cha 2 kinasomeka

2 (2). “The regulations of petroleum upstream operation, midstream and downstream activities and
matter incidental thereto to which this Act apply shall

  • …………………………….
  • Where such operations or activates are undertaken within Tanzania Zanzibar, be governed and administered by institutions in accordance with the laws of Tanzania Zanzibar ”

Mheshimiwa Rais, laiti Serikali yako ingetafakari zaidi juu ya kifungu hiki, basi ingegundua wazi kuwa hakiipa mamlaka ya kutunga sheria ya masuala ya Mafuta na Gesi bali ni kuzipa taasisi zilizopo Zanzibar kuwa wasimamizi wa kanuni (Regulations) zinazotokana na sheria hiyo na sio kutunga sheria yetu nyingine ambayo ni kama pacha wa sheria iliyotungwa na Bunge. Na ndio maana ukisoma kifungu kidogo cha 1 cha kifungu hicho hicho cha 2 kinasema sheria hiyo itatumika kote Bara na Zanzibar. Kwa hiyo kimsingi Sheria ni moja tu. Kinachojaribu kuelezwa kwenye kifungu kidogo cha pili ni usimamizi wa kanuni zinazotokana na Sheria hiyo.

Mheshimiwa Rais, kama ambavyo unafahamu na kama umeelezwa hivyo na washauri wako au la, kwamba mamlaka ya kutunga sheria kwa Bunge la Muungano yanatokana na Ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano. Bunge letu limepewa mamlaka ya kutunga sheria zote zinazohusu Muungano na zile zisizohusu Muungano ambazo zinatumika Tanzania Bara.

Katika Ibara hiyo ya 64, Ibara ndogo ya 3 imetoa katazo kwa Baraza la Wawakilishi kutunga sheria yoyote inayohusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge na Katiba ikatamka wazi ikiwa jambo hilo litafanyika basi sheria hiyo iliyotungwa itakuwa batili.

Mheshimiwa Rais, ipo hoja inajengwa na baadhi ya watu hasa wasaidizi wako kuwa kifungu cha 2 kifungu kidogo cha 2 ndio kimetoa mamlaka yake kwa SMZ kutunga sheria. Hoja hii haina mashiko na ni upotoshaji mkubwa wa mamlaka ya Bunge.

Nakubaliana na hoja ya kuwa Bunge linaweza kukasimu madaraka yake kwa mamlaka nyingine isiyokuwa Bunge lakini kamwe mamlaka hayo hayawezi kuwa ya kutunga sheria isipokuwa kutunga kanuni. Na hili limeelezwa wazi kwenye Ibara ya 97 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo naomba nikinukuu hapa.

Ibara ya 97(5) “ Masharti yaliyomo katika ibara hii au katika ibara ya 64 ya katiba hii hayatalizuia Bunge kutunga sheria na kuweka masharti ambayo yaweza kukabidhi kwa mtu yeyote au kwa idara yoyote ya Serikali madaraka ya kuweka kanuni zenye nguvu kisheria au kuzipa nguvu ya kisheria kanuni zote zilizowekwa na mtu yeyote wa idara yoyote ya Serikali”

Mheshimiwa Rais, maelezo hayo ya Ibara ya 97(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano yapo wazi na wala hayahitaji utaalamu mkubwa kuyatafsiri kujua maana yake. Ni wazi kuwa Bunge limetunga kifungu cha 2 (2) (b) kuipa mamlaka idara ya Serikali ya SMZ aidha kusimamia kanuni au kutunga kanuni za kuipa nguvu sheria ya Mafuta namba 21 ya mwaka 2015 na sio kutunga sheria nyingine.

Mheshimiwa Rais, natamani ningeandika mengi sana ila kwa sasa naomba niishie hapa nikiwa na matumaini kuwa ujumbe huu utakufika na kuzingatia nasaha zangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles