Na ANDREW MSECHU
KATIKA Utafiti uliotolewa na kuchapishwa kupitia kituo cha Associated Press Juni 14 mwaka huu, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Colombia nchini Marekani wameeleza kuwa wamebaini wanyama hasa Simba wamekuwa na tabia mpya ya kufanya mawindo yao usiku kuliko mchana, kwa kukwepa kukutana na binadamu ambao wamekuwa wakiingia kwenye maeneo ya hifadhi kwa shughuli zao.
Wanasayansi hao wanasema wamebaini kuwa shughuli za binadamu katika maeneo ya jirani au maeneo ya hifadhi za wanyama zimekuwa zikivuruga asili ya maeneo hayo, hivyo kuwafanya wanyama hao hasa Simba kwa Tanzania, badala ya kujishughulisha na mawindo yao kwa ajili ya chakula, kukimbilia maeneo ya ndani zaidi kujificha au kujikuta wakizungukazunguka kuwakwepa binadamu.
Utafiti huo unaeleza kubaini kuwa hata shughuli za safari za mbugani ai uwekaji wa kambi katika maeneo ya mbuga unaweza kuwatia hofu wanyama na kuwafanya wabadilia tabia zao za asili kwa kufanya uwindaji wao kwa uhakika zaidi nyakati za usiku, muda ambao hakuna shughuli za binadamu.
“Tulijaribu kuingia kwa kujificha katika maeneo ya wanyama na kuhakikisha kwamba tunafanya hivyo bila wao kujua. Lakini tulibaini kuwa uwepo wetu katika maeneo hayo ulisababisha shida kwa wanyama hasa wanaowinda,” anasema muikolojia Kaitlyn Gaynor kutoka Chuyo Kikuu cha California, Berkeley huko Marekani.
Ufafanuzi
Katika ufafanuzi wake kuhusu namna binadamu wanavyoingia katika hifadhi za wanyama na kusababisha wanyama kutotulia katika maeneo yao ya asili, kupitia kipindi cha dakika 45 cha ITV Mkurugenzi Mtendaji wa Hifadhi za Taifa, Allan Kijazi alisema suala hilo limewaingiza katika gharama ambazo hawakuzitegemea katika mipaka ya hifadhi za taifa ila wamekuwa wakichukua hatua za kukabiliana nalo.
Anasema wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa vijiji vinavyozunguka maeneo ya hifadhi yaliyoainishwa na hata kutumia mahakama kuchukua hatua kwa wanaokiuka taratibu, ambapo wengi wao ni wafugaji na wapo waliokubali na kupunguza kasi ya kuingiza mifugo hifadhini lakini pia wapo ambao wameendelea kwa njia za ujanja ujanja.
“Tumeendelea kukutana na wananchi hao lakini usipokuwepo mbadala hii itaendelea kuwa tatizo. Katika ngazi ya kitaifa tayari makubaliano yameshafikiwa baina ya Wizara ya Utalii, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na mifugo kuwe na mkakati wa kitaifa wa kuboresha malisho ya mifugo nje ya hifadhi,” anasema
Anasema katika kutatua tatizo hilo pia wanahitaji kushirikiana kuendeleza hayo maeneo kwa maana ya kujenga mabwawa na kuwezesha wafugaji kupata maji kwa ajili ya mifugo yao lakini pia wanahitaji kutoa elimu zaidi kwa wafugaji kupunguza idadi ya mifugo na kutumia mbinu za ufugaji wa kisasa ili wawe na mifugo michache ambayo wataweza kuihifadhi.
Anasema katika kukabiliana na tatizo hilo angalau wamejaribu kutenga bajeti kwa mwaka ujao wa fedha kuchimba mabwawa kwa ajili ya wafugaji katika maeneo yao na kupata maeneo ya kulisha mifugo yao.
Dk Kijazi anafafanua kuwa mtawanyiko wa wanyama katika hifadjhi imekuwa ni mkubwa zaid ya ilivyowekwa na mipaka ya kiutawala, ambayo ni hifadhi za taifa lakini wanyama hao hawatambui mipaka hiyo.
“Pale ambapo wanaona kuna malisho na kuna maji wanahama kufuata maeneo hayo na wanahama kutoka eneo moja kwenda jingine katika kuboresha mwingiliano wa jenetiki katika familia zao mbalilmbali kwa hiyo shiroba nyingi zimevamiwa kwa kuwa hakukuwa na sheria maalumu zinazowezesha kuzilinda,” anasema.
Anaeleza kuwa katika Sheria ya Ngorongoro na ya TANAPA zote zinatambua uwepo wa shoroba (maeneo maalumu ya asili ya wanyama) lakini hakukuwa na miongozo ya namna ya kusimamia shoroba hizo kwa hiyo zimevamiwa na wananchi wamejenga, wanalima, wanachimba madini na kuibua migogoro ya muingiliano baina ya wanyama pori na shughuli za binadamu.
Anasema maeneo mengi yenye migogoro yamekuwa yakitumiwa na wanyama pori kwa muda mrefu lakini wananchi wamevamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu kwa ajili ya maendeleo, suala linalohitaji kusimamiwa upya na kuwepo na utaratibu mzuri kujua maeneo gani ni muhimu sana kwa shughuli za kibinadamu na yapi ni muhimu sana kwa shughuli za wanyama na kuyatenganisha.
Katika utafiti huo, watafiti hao wa Chuo Kikuu cha Columbia walieleza pia kwamba waliangalia kufanya uwiano wa muda ambao wanyama hao hutumia kikamilifu usiku hasa kutokana na mwingiliano wa shughuli nyingi za uwindaji, shughuli za binadamu mbugani na kilimo.
Dk Gaynor anasema kwa wastani kikosi chake kilibaini kwamba uwepo wa binadamu katika maeneo ya mbuga unachangia kwa zaidi ya asilimia 20 tabia ya wanyama kufanya uwindaji wao usiku hata kwa wanyama ambao kiasili hawakuumbwa kufanya shughuli zao usiku.
Muikolojia katika Chuo Kikuu cha Goethe huko Frankfurt, Ujerumani ambaye hakuwa sehemu ya waliofanya utafiti huo, Marlee Tucker naye anaeleza kushangazwa kwake na namna matokeo hayo yanavyoonyesha shughuli za binadamu katika maeneo ya wanyama zinavyoweza kuwatisha.
“Inatisha kidogo. Hata kaka watu wanafikiri kwamba katika hali ya kawaida hatuwezi kuwa na athari za vitisho kw awanyama, kumbe tumekuwa tukiwasababishia hofu bila sisi kujua,” anasema.
Gaynor anasema wanyama ambao hawawezi kukabili kwa urahisi mazingira ya giza ndio watakaoathirika zaidi lakini inaonekana kuna mabadiliko ya kitabia yanayowafanya wanyama kujiepusha na mapambano ya moja kwa moja na binadamu.
Uchimbaji wa madini
Akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu maeneo yanayosababisha usumbufu kwa wanyama katika Hifadhi za Taifa Dk Kijazi anasema uchimbaji madini nao ni tatizo ambalo wamejaribu kulidhibiti na katika baadhi ya maeneo ya hifadhi ya Serengeti wametumia sheria kuweka nguvu ya ziada kuzuia wananchi kuingia katika maeneo hayo.
Anasema ni rahisi kulidhibiti tatizo hilo kwa kuwa mtu hawezi kuingia na kutoka, atalazimika kuingia na kukaa kwa muda hata wa siku nzima, ambapo tayari kwa hali ya ulinzi inatoa tahadhari kwa wananchi kuingia hifadhini kuchimba madini.
“Tatizo kubwa la hivi karibuni lilikuwa kwenye Hifadhi ya Ziwa Manyara katika eneo la msitu wa Maran lililounganishwa na Hifadhi za Taifa hivi karibuni, ambalo wapo wachimbaji wadogo waliopewa vibali vya kuchimba madini kwenye eneo hilo, tumeendelea kuwaelimisha kutokana na sheria ndogondogo na tumetumia mahakama kuweka zuio la uchuimbaji madini katika eneo hilo,” anasema.
Ujangili
Anasema katika kukabiliana na tishio la ujangili kwa wanyama adimu hasa tembo na faru wameanzisha pamoja na ulinzi wa jumla kupitia kitengo maalumu cha wanyama adimu kwa ajili ya kuweza kufahamu na kufuatilia mienendo yao katika maeneo yote.
Anasema kwa sasa kimeanzishwa kikosi maalumu baada ya kufahamu maeneo muhimu wanayopenda kuwepo katika kila hifadhi na kuanzisha vikosi maalumu ambavyo vinahakikisha katika maeneo hayo yanakuwa na usalama wa kutosha, ikihusisha uwepo wa kutosha wa vifaa na wataalamu na kuchukua hatua kwa haraka pale inapoonekana kuna tatizo.