27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 50 ya Bakwata itumike kujitathmini

Na CLARA MATIMO

DESEMBA 17, mwaka jana Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), lilifanya maadhimisho ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Maadhimisho hayo ya kitaifa ambayo yalifanyika jijini Dar es Salaam ni ya kwanza tangu baraza hilo lilipoanzishwa  Desemba 17, 1968 mkoani Iringa.

Bakwata lilianzishwa kwa lengo la kuwaunganisha Waislamu wapate chombo cha kuwasemea, kuwaendeleza kielimu, kutoa malezi na maadili mema kwa vijana, kuratibu shughuli zote za taasisi za Kiislamu nchini, kulinda na kusimamia mali za baraza hilo.

Tangu lilipoanzishwa baraza hilo limeongozwa kwa awamu tatu, ambapo Sheikh Hemed Jumaa aliongoza kwa mara ya kwanza hadi mwaka 2002 akafuatiwa na Issa Simba aliyedumu hadi 2015 na Sheikh Abubakar Zubeir wa sasa.

Naamini kila uongozi uliopita unayo mambo mazuri uliyoyafanya kwa masilahi ya Waislamu wote nchini hususan awamu ya sasa chini ya Mufti Sheikh Zubeir ambaye tangu aingie madarakani amejipambanua kwa kauli mbiu ya ‘Jitambue, Badilika acha Mazoea’.

Kauli mbiu hiyo imelenga kuleta mageuzi makubwa ndani ya baraza hilo kwa kumhimiza kila Mwislamu kuishi katika misingi mizuri ya dini na viongozi wa Bakwata kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kurejesha imani iliyokuwa imeanza kutoweka.

Kutokana na baadhi ya viongozi wa baraza hilo kutoka nje ya mstari kulizua maswali kwa waumini walioanza kuitupia lawama Bakwata kwa kushindwa kutoa malezi na maadili mema kwa vijana, kuratibu shughuli zote za taasisi za Kiislamu nchini, kulinda na kusimamia mali za baraza hilo.

Hali hii pia ilithibitishwa na Mjumbe  wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Mkoa wa Mwanza, Rajabu Rajabu, ambaye anaamini kuwa Bakwata ililala na kushindwa kusimamia majukumu yake ikiwemo malezi hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema kuwapa mafundisho mabaya na kusababisha baadhi ya vijana kujihusisha na masuala ya ugaidi.

Hivyo basi kutokana na udhaifu huo nakubaliana na hoja ya Katibu wa Msikiti wa Ijumaa uliopo jijini Mwanza, Abdallah Sheikh Amin, aliyeitaka Bakwata kuangalia namna bora ya kupata viongozi wake na kuepuka kuwapa nafasi ya kutoa elimu katika misikiti masheikh na maimamu ambao hawajulikani.

Hii itasaidia vijana kutopata mafundisho ambayo hayaendani na maadili ya dini ya Kiislamu maana kijana wa Kiislamu kujihusisha na vitendo vya ugaidi ni kuutukanisha Uislamu kwa kuwa  mafundisho ya dini hiyo hayaruhusu muumini yeyote kutenda mambo mabaya katika jamii. 

Rai yangu kwa viongozi na Waislamu wote nchini wahakikishe wanatumia maadhimisho hayo kwa kujitathmini na kuyafanyia marekebisho pamoja na kuondoa kasoro zinazoweza kuleta msuguano na kusababisha kushindwa kutimiza matakwa ya waumini wa dini hiyo pamoja na kuratibu shughuli zote za taasisi za Kiislamu nchini.

Kama ambavyo tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa Bakwata wakisimamishwa uongozi kwa madai mbalimbali ikiwemo kushindwa kusimamia vyema mali za baraza hilo zilizopo katika mikoa yao jambo lililosababisha mali za Waislamu kuhujumiwa.

Katika kuhakikisha baraza hilo linarudi kwenye misingi yake na malengo mahususi, Mufti Abubakar Zubeir, aliunda tume kufuatilia mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na mali za baraza na taasisi zake nchi zima na kuona uhalali wa umiliki huo pamoja na hali ya usajili wa mali hizo.

 Pia katiba ya Bakwata imefanyiwa marekebisho katika kipengele cha uongozi na sasa masheikh wa mikoa na wilaya watapatikana kwa kuteuliwa na wajumbe wa baraza la ulamaa la Bakwata taifa.

Mabadiliko haya ya Katiba yamewafurahisha Waislamu wengi akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu Bakwata Mkoa wa Mwanza, Mohamed Ngonyoke, anayeamini kwamba mfumo huo utaleta ufanisi ndani ya Bakwata kwa kuwa viongozi hao wanaelewa wasipowajibika uteuzi wao utatenguliwa tofauti na ule wa awali uliokuwa unawalinda hadi kifo.

Ni wazi kwamba tangu kufanyika mabadiliko haya mpaka sasa mikoa yote haina masheikh wakuu bali wapo makaimu ambao wanasubiria uteuzi, ni imani yangu kuwa wale watakaopata nafasi za uongozi watawajibika ipasavyo kwa masilahi ya Waislamu na miaka hii 50 iwe sehemu ya wao kujitathmini na kujifunza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles