28.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Wakulima kupewa vitambulisho

MWANDISHI WETU -DODOMA

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga amewaagiza wakurugenzi wa bodi za mazao kuanza mara moja kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini ili waweze kupewa vitambusho vya kuwatambua.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote nchini. Desemba 10, mwaka jana Rais Dk. John Magufuli alitoa vitambulisho kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini – wamachinga, ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Waziri Hasunga alitoa agizo la kuanza kutambuliwa kwa wakulima wote nchini jijini hapa jana, wakati akizungumza na wenyeviti na wakurugenzi wa bodi za mazao.

Alisema ili kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote, ni vyema kuwatambua wakulima wote nchini.

Hasunga alisema wakulima wa zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa wizara yake kufanya jambo kama hilo katika mazao mengine nchini. Wiki tatu zilizopita, Hasunga aliiagiza Bodi ya Korosho kuandaa daftari maalumu la kuwatambua wakulima wa korosho kote nchini.

Taarifa ambazo zitajumuishwa katika daftari hilo ni pamoja na jina kamili la mkulima, mkoa, wilaya, kata na tarafa anayotoka. Mambo mengine ni pamoja na kitongoji, mtaa au jina la kijiji anakotoka, mahali lilipo shamba lake na ukubwa wake.

Hasunga alisema ili kuwa na mipango sahihi ya kuwaendeleza wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko, ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.

Hasunga alishauri matumizi ya TEHAMA na ya mfumo wa GPS ili kuboresha daftari hilo kwa lengo la kuboresha uwekaji wa taarifa za wakulima na maeneo wanayotoka kwa usahihi zaidi. “Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa rahisi.

“Kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka mwezi Machi 2019 na bodi za mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari walishafanya hivyo, kukamilisha mwezi Juni 2019,” alisema Hasunga.

MALIPO WAKULIMA KOROSHO Akizungumzia malipo kwa wakulima wa korosho, Hasunga alisema wapo baadhi wameshindwa kulipwa fedha kutokana na taarifa zao za kibenki kuwa na mkanganyiko. “Serikali inaendelea na zoezi la uhakiki wa wakulima wa zao hilo na kuwaondoa wale waliofanya udanganyifu,” alisema.

Alisema hadi sasa Serikali imekusanya zaidi ya tani laki moja kutoka kwa wakulima wa zao hilo. UHAKIKI WA VYAMA VYA MSINGI Hasunga alisema hadi sasa wamefanya uhakiki wa vyama vya msingi 466 huku akiwahakikishia wakulima wote kulipwa fedha zao mara baada ya kukamilika kwa kazi hiyo.

Pia aliwataka wale wote wanaodaiwa katika vyama vya ushirika kulipa mikopo yao ili kuhakikisha vyama hivyo vinajizatiti katika kuendelea kuwakopesha wanachama wake.

Hasunga aliitisha kikao hicho maalumu na viongozi wa bodi za mazao, wakala na taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuboresha mikakati na kuongeza ufanisi katika utendaji wa wizara pamoja na kujitathmini kabla ya kufikia nusu mwaka ya utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya wizara ya mwaka 2018/2019 ili kujipanga kwa utekelezaji wa bajeti ya mwaka ujao wa 2019/2020.

Bodi za mazao zilizoshiriki ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Mkonge, Bodi ya Pareto, Bodi ya Chai, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Sukari.

Wakala zilizoshiriki ni pamoja na Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA). Washiriki wengine ni Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki (TPRI) na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF).

Wengine ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) na Bodi ya Leseni za Maghala. VITAMBULISHO VYA WAMACHINGA Desemba 10, mwaka jana Rais Dk. John Magufuli, alitoa vitambulisho 670,000 kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini ili kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Rais alitoa vitambulisho hivyo kwenye mkutano wake na watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakuu wa mikoa yote nchini kujadili namna ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji mapato.

Alisema kwa muda mrefu amekuwa akiiagiza TRA pamoja na halmashauri kutowatoza kodi wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi Sh milioni 4, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.

Kila mkoa utapewa vitambulisho 25,000 na kila mjasiriamali mdogo atalipia Sh 20,000 na fedha hiyo kupelekwa TRA. Kwa malipo hayo, kila mkuu wa mkoa atakusanya Sh milioni 500 na ikilazimu aagize vitambulisho vingine kwa ajili ya watakaovihitaji.

Rais Magufuli alisema hajaridhishwa na utaratibu wa kuunganisha kitambulisho cha TRA na kile cha Taifa kuwatambua wafanyabiashara wadogo akibainisha baadhi yao kutozwa kodi nje ya maagizo. Mwisho

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,663FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles