MOSCOW, Urusi
URUSI na Misri zimesema zitaendelea kushirikiana katika nynja mbalimbali ili uhusiano baina ya mataifa haya mawili uweze kufika ngazi nyingine.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje wa hapa, Sergey Lavrov kupitia ujumbe aliouandika katika jarida la Time-Tested Friendship na kuchapishwa katika tovuti ya gazeti la Al-Ahram la Misri.
Lavrov alisema uhusiano wa siasa kati ya nchi hii na Misri unazidi kukua na biashara baina ya mataifa haya mawili inazidi kuchanua tangu ilipofikia wastani wa dola bilioni 6.5 kwa mwaka.
“Ushirikiano katika nyanja za jeshi unawezesha vikosi vya Misri na utekelezaji wa sheria kupinga vitisho vya ugaidi kwa ufanisi zaidi,” alisema waziri huyo.
“Aina mpya za ushirikiano katika nyanja hii zinajaribiwa kwa ufanisi.
“Oktoba 2016 katika mkutano uliofanyika katika ardhi ya Misri na Septemba 2017 katika mkutano uliofanyika Urusi kwa pamoja tulikubaliana kupambana dhidi ya ugaidi na katika mkutano wa utetezi wa urafiki uliofanyika mwaka 2016 na mwaka 2017 ambao ulivihusisha vikosi vya anga vya mataifa haya mawili,”aliongeza waziri huyo.
Alisema Urusi na Misri zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika kutatua migogoro mbalimbali duniani kujenga umoja miongoni mwa jamii.