AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
KATIKA kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti duniani, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Maguha Stephano, amewashauri wanawake kuwanyonyesha watoto kama inavyoshauriwa na wataalamu wa lishe kwani hali hiyo si tu inamsaidia mtoto, lakini pia ni kinga kwa ugonjwa wa saratani ya matiti.
Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, Dk. Maguha alisema kuwa wanawake ambao hawajazaa wala kunyonyonyesha wako katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti.
“Hatari ipo kubwa kwa wale wanawake ambao hawajazaa na kwa wale wanaozaa, lakini hawataki kunyonyesha. Kitaalamu kwa kadiri unavyonyonyesha, mfano kunyonyesha mtoto mpaka miezi sita au hata miaka miwili, hapo uwezekano wa kupata saratani unakuwa mdogo.
“Kwahiyo kunyonyesha ni moja ya kinga ya ugonjwa wa saratani ya matiti kwa wanawake, wale ambao wanakwepa kunyonyesha nawashauri wanyonyeshe ipasavyo ili waweze pia kujikinga na saratani ya matiti,” alishauri Dk. Maguha.
Alisema mambo mengine yanayosababisha saratani ya matiti ni matumizi ya muda mrefu ya dawa za uzazi wa mpango ambazo zina kiambata kinga cha estrogen, hivyo amewashauri wanawake kupunguza matumizi ya dawa za uzazi wa mpnago zenye hivyo viambata.
“Mtumizi ya dawa hizo kwa mfano mwanamke anatumia dawa za uzazi kwa miaka 15 hadi 20, hii inaweza kuleta madhara kwa kumsababibishia saratani ya matiti, sababu nyingine ni ile ya unene uliopitiliza husababisha mafuta kuwa mengi mwilini.
“Kuna zile sababu za kurithi, kwa mfano kama kuna mtu kwenye ukoo wako alishawahi kupata saratani ya matiti ambayo inatokana na vinasaba, pia inaweza kurithiwa.
“Pia nawashauri, hasa wanawake waachane na matumizi ya vilevi na sigara kwani hata hivi husababisha saratani ya matiti,” alisema Dk Maguha.