26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UJENZI MADARASA YA MATEMBE BUSARA INAHITAJIKA

JUZI Serikali kupitia Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo, aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini, kuhakikisha wanaondoa madarasa ya tembe, nyasi na udongo katika maeneo yao.

Kauli hiyo ya Jafo imekuja ikiwa ni siku chache tangu MTANZANIA iliporipoti taarifa ya madarasa ya udongo yaliyoezekwa kwa makuti katika Shule ya Msingi Mitambo, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, kubomolewa kwa amri ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Omary Kipanga, baada ya picha za shule hiyo kusambaa katika mitandao ya kijamii.

Agizo hilo hilo la Waziri Jafo alilitoa mjini Dodoma alipokuwa akifungua awamu ya nne ya semina elekezi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Pwani na Mtwara, mjini hapa.

Jafo alisema hataki kusikia habari ya madarasa ya tembe na udongo katika shule mbalimbali bali anataka madarasa yenye ubora ili mwanafunzi aweze kusoma vizuri.

Licha ya Mkoa wa Mtwara kupata mapato kupitia zao la korosho, ndio unaongoza kwa kuwa na majengo ya nyasi na tembe.

Hata hivyo kabla ya agizo hilo la Serikali kwanza viongozi wetu walitakiwa kupima kwa kujiuliza kwa nini wazazi wamechukua uamuzi wa kujenga madarasa hayo.

Ni wazi kabisa huenda wazazi walikuwa na nia njema hasa baada ya watoto wao kusomea chini ya mti na kujikuta wakinyeshewa na mvua pamoja na kupigwa na jua kali.

Hatua hiyo ya ujenzi huo wa madarasa hayo ya muda  ambayo alibomolewa baada ya agizo la mkurugenzi sasa wanafunzi hao wanasomea chini ya mti.

Sisi MTANZANIA tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu katika kuinua elimu kupitia mpango wa elimu bure, ambapo Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 100 kwa ajili ya kugharimia elimu nchini sambamba na ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa.

Pamoja na mpango huo wa Serikali wenye nia njema kwa Taifa lakini kilichotakiwa kwa wananchi waliojenga madarasa ya tembe kwanza yasingebomolewa wakati ikiandaliwa mipango ya kujenga majengo ya kisasa.

Kwa kipindi kirefu elimu yetu imekuwa ikikabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo suala la lugha ya kufundishia na tafsiri ya elimu bure inavyoleta mkanganyiko huku baadhi ya maeneo ikichangia jamii kujitoa katika suala zima la uboreshaji wa elimu kiujumla.

Hata hivyo MTANZANIA tunashauri elimu zaidi itolewe kwa jamii ili kuweza kujua umuhimu wa elimu kwani wapo wazazi wanajiondoa katika kuchangia mafanikio ya elimu kwa kutojua umuhimu huo.

Tunajua wazi kwamba mfumo wa sasa elimu bure umeleta mafanikio na changamoto, kwani wazazi wamejiondoa kabisa kuchangia hata masuala ya msingi kwenye elimu ya watoto wao ambayo Serikali haiwezi kufanya yote kwa asilimia 100.

Sisi MTANZANIA tunasema jambo hili ni hatari kwani wazazi wapo tayari kuchangia sherehe za mahafali lakini si ujenzi wa choo shuleni.

Hivyo pamoja na mikakati mizuri ya Serikali hasa katika kuzuia ujenzi wa madarasa ya matembe bado busara inahitajika ili kutafuta ufumbuzi wa pamoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles