23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

HATUA HIZI ZA WAZIRI LUKUVI NI ZA KUIGWA

NA MASYENENE DAMIAN

MOJA ya changamoto kubwa katika ukuaji wa miji, majiji yetu mikubwa nchini ni migogoro ya ardhi.

Hii ni kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu na uboreshaji makazi unaowaacha baadhi ya wananchi wakiwa wamechukuliwa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za maendeleo bila kuwalipa fidia inayostahili.

Wakati nchi yetu ikiwa imezungukwa na migogoro ya ardhi kila kona na kusababisha kuibuka kwa malalamiko mengi yasiyoisha, mamlaka za Serikali zimekuwa zikijitahidi kuweka mikakati mbalimbali ya kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo bila mafanikio.

Hata hivyo, baadhi ya mikakati hiyo ni kampeni maalumu iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya Waziri wake, William Lukuvi, iliyopewa jina la ‘funguka kwa waziri’.

Lukuvi anatumia mkakati huo kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi juu ya kero ya migogoro ya ardhi na kuitafutia majawabu.

Jiji la Mwanza linaloundwa na wilaya za Nyamagana na Manispaa ya Ilemela ni moja ya majiji yanayokua kwa kasi nchini.

Jiji hilo linakadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi ya 700,000. Ongezeko hilo limesababisha kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika jiji hilo, hali iliyomlazimu Waziri Lukuvi kufanya ziara za mara kwa mara ili kutafuta ufumbuzi.

Hivi karibuni, Waziri huyo alitembelea Jiji la Mwanza kutafuta ufumbuzi wa migogoro mbalimbali iliyodumu kwa muda mrefu.

Mojawapo ya migogoro hiyo ni baina ya wananchi na taasisi za Serikali hususan Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi katika maeneo ya Kigoto, Uwanja wa Ndege pamoja na Nyambiti.

Ili kumaliza migogoro hiyo, Lukuvi alizisisitiza taasisi zote za Serikali kupima maeneo yao na kuyachukulia hati ili kuepusha migogoro na uvamizi wa wananchi kila mara.

Pia alizishauri taasisi hizo kuweka mipaka mipya kwa kuyawekea uzio unaonekana kirahisi ili kuepuka uvamizi mpya kwenye maeneo hayo  yanayomilikiwa kihalali na Serikali.

Waziri Lukuvi alisema amechoka kusikia migogoro kati ya wananchi na taasisi za Serikali, uvamizi katika maeneo hayo  huku akisisitiza maeneo hayo yalipimwa lakini yana migogoro yahakikiwe upya yakiwamo ya shule, hifadhi za wanyama, misitu, ranchi za Taifa, zahanati, vituo vya afya na maeneo yote mengine yapimwe na yamilikishwe na kila wizara imiliki maeneo yake.

Uamuzi mwingine alioufanya Waziri Lukuvi ni kuupatia ufumbuzi mgogoro uliodumu kwa muda mrefu baina ya wananchi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) wanaosimamia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Aidha, katika maagizo hayo, Waziri aliwataka TAA kuwatumia wapimaji na wapangaji wake kutengeneza ramani ya mwisho ya uwanja huo pamoja na mipaka mipya ifikapo Aprili, mwaka huu.

Sambamba na hilo, alitaka mipaka mipya ya uwanja huo iwe imepatikana na kuandikiwa hati ya kiwanja hicho na mamlaka hiyo iwe na jukumu la kuilinda mipaka ya uwanja huo, huku wananchi waliojenga nyumba zaidi ya 1,000 ndani ya mipaka ya uwanja huo wakiamriwa kuondoka kwani ni wavamizi.

Pia iliamriwa kufutwa kwa viwanja vyote vilivyopimwa kwa ajili ya makazi katika eneo la Nyashana wilayani Ilemela yalipo mapitio ya ndege za jeshi, huku akiagiza wale waliolipa na kupewa hati za viwanja hivyo kupewa viwanja vingine ili eneo hilo likabidhiwe kwa jeshi.

Pamoja na kumpongeza Waziri Lukuvi, nimkumbushe kwamba si Mwanza pekee penye migogoro baina ya taasisi za Serikali na wananchi.

Kwa hiyo busara iliyotumika kwa wananchi wa Nyambiti inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mengine yenye migogoro ya namna hiyo ili kuepusha dhuluma.

Juhudi na hatua hizi zinazochukuliwa na Waziri Lukuvi zinapaswa kuungwa mkono ili Serikali isiendelee kulaumiwa kila siku na wananchi wake.

Maendeleo ya miji, majiji na hata miji midogo hayatakuwa na maana endapo Tanzania itaendelea kuwa na maeneo holela yasiyopimwa na kumilikishwa kisheria.

Turasimishe maeneo hayo ili suala la migogoro isiyoisha lifiki tamati. Bravo Waziri Lukuvi umejaribu kuutafuna mfupa uliowashinda wengi. Dawa ya mfupa ni kuutafuna si kuupapasa!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles