23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TAWALA ZA KISIASA ZINAPOKUWA MBOVU

Na ALOYCE NDELEIO

KATIKA Jiji la Dar es Salaam ipo spishu ngeni vamizi ya kunguru weusi ambao wanadaiwa kuwa ni kero kubwa katika makazi ya watu kwa kuwa huvizia hata vyakula vinavyopikwa na kunyakua vitoweo wanachokiona.

Wameshazoeleka kama wanyama wa kufugwa. Wanaongezeka idadi kwa kiwango cha kutisha na kuteketeza ndege wa jamii nyingine katika mazingira waliyoshamiri. Hawa hawakuwapo katika  karne moja iliyopita.

Lakini kilichosababisha au kuendelea kusababisha kuwapo kwa spishu hizo ni uchafu na mizoga ambayo  kimsingi inakuwa imesambaa hovyo kutokana na udhibiti usiokidhi wa taka.

Hivyo ndivyo yalivyo maisha ya kunguru kwamba palipo na mzoga  ndio sehemu ambayo huonekana, lakini kama eneo likiwa safi ni nadra kuwaona wanaspishi hao wageni na wavamizi.

Kiuhalisia kuwapo kwao katika maeneo yaliyo na mizoga haiwezi kuelezwa kuwa ni wavamizi bali wanakuwa tayari wamealikwa kwenye karamu ya kula ‘vinono’ hivyo vichafu ili kuweka mazingira safi.

Taswira za kisiasa nazo zinabeba picha hiyo kwamba pale ambako hakuna usimamizi mzuri wa mipango inayoihusu jamii lazima kuwapo na kitu kinachotoa msukumo kuwa usimamizi huo ni mbovu na kuna haja ya kuondokana nao.

Tawala za kisiasa zinazokuwa mbovu  zikiwa zinakandamiza, kuzinyima jamii haki na kudhoofisha ustawi wa jamii hukutana na matukio ambayo yanakuwa ni mageni kwake  ambayo yanakuwa ni matokeo ya kuchoshwa na tabia onevu za utawala.

Zimbabwe ambayo ilipata uhuru wake mwaka 1980 kutoka kwa utawala wa Uingereza  katika hatua za awali  ilionekana kuwa utawala wake upo katika ule mkondo wa utawala wa watu kwa ajili ya watu.

Hata hivyo utawala huo chini ya Rais Robert Mugabe uliiingia katika  mkanganyiko ambao ulisababisha kuwapo kutofautiana na nchi za Magharibi kutokana na wageni wa nchi hizo waliokuwa nchini humo kunyang’anywa rasilimali ya ardhi ambayo ilidaiwa kupewa wazawa  wengi wakiwa ni wale maveterani wa vita ya kupigania uhuru.

Hapo ndipo sekeseke lilipoanza baada ya kinachodaiwa kuwa ardhi hiyo  iligawiwa kwa kuwabagua wanachama wa vyama vingine vya upinzani na hivyo kuhodhiwa na wanachama wa chama tawala peke yake.

Kwa upande mwingine Mugabe aligeuka na kuwa sio msikivu na uchumi wa nchi ukawa unaporomoka ikizingatiwa kuwa vikwazo vya nchi za Magharibi vilichangia kwa kiwango kikubwa.

Hali hiyo inamaanisha kuwa tofauti za kisiasa ndani ya nchi pamoja na vikwazo kutoka nje  vikawa vinaitifua jamii nchini humo.

Lakini baya zaidi ni kutokubaliana na mabadiliko kwa kuwapo ung’ang’anizi wa madaraka na kutokubaliana na mabadiliko ambayo yalikuwa yanahitajika ndani ya nchi.

Taswira ya kuonesha kuwa utawala ulikuwa ni wa kiimla ndio uliongeza mtafaruku  na hususani ubabe wa Mke wa Rais Grace ulioonesha kuwa  anataka kuurithi uongozi wa mumewe.

Hii ikimaanisha kuwa kuingilia kwa jeshi ambako kumefanyika kwa kumweka kizuizini Mugabe  sio  kumetokana na ile dhana ya kizamani ya wanajeshi kuingia madarakani bali inatokana na uozo ambao umekuwa ndani ya jamii na ukiongeza kero ya ugumu wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles