KAMPALALA, UGANDA
SERIKALI ya Rais Yoweri Museveni imekana madai yaliyotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa kulegalega kwa uhusiano wa nchi hizo unatokana na Uganda kusikiliza uvumi kutoka kwa Wanyarwanda waishio Afrika Kusini.
Aidha Uganda imekana kuwa uhusiano wake na utawala wa Rwanda umezorota.
Ufafanuzi huu unafuatia kile kinachotajwa kuwa mgogoro kati ya mataifa hayo jirani, huku Rwanda inaikosoa Uganda kwa kuwasaidia wapinzani wake walio chini ya vuguvugu la Rwanda National Congress (RNC) kuvuruga utulivu nchini humo.
Aidha raia wa Rwanda waishio Uganda wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na kukamatwa kiholela na vyombo vya usalama vya hapa.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na gazeti moja la Afrika Mashariki, Rais Kagame alinukuliwa akisema mgogoro kati ya nchi zao unaendelezwa kwa sababu Uganda imeamua kuamini uvumi unaosambazwa na raia wa Rwanda waliopo Afrika Kusini badala ya kuamini kile ambacho Serikali yake inakisema.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Uganda Ofwono Opondo amekanusha madai hayo.
“Ni jambo la kuchekesha kwa yeyote kusema kuwa Serikali ya Uganda, haina taasisi za kuipatia habari za kuchunguza na hivyo inategemea habari za uzushi hasa za Wanyarwanda walioko Afrika Kusini au taifa lolote.
“Kama ingelikuwa hivyo, Serikali ya Uganda ingekuwa matatani na Serikali zote duniani. Kwa sababu katika mataifa haya, kuna watu walio na midomo mibaya au wanaozungumzia vibaya Serikali ya Uganda au mataifa yao.
“Hivyo Serikali haisikilizi habari zozote za tetesi kutoka taifa lolote ambalo linatofuatiana na taifa jingine, hilo halipo,” alisema Opondo.
Madai ya kuwapo kwa mgogoro unaofukuta kati ya Uganda na Rwanda yameendelea kuripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari.
Safari hii mawaziri wa Serikali ya Rwanda na hata rais mwenyewe wamenukuliwa wakielezea masikitiko yao kuhusu kuyumba kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, kitu ambacho Uganda inakipinga.
Lakini Opondo anaeleza kuwa marais Museveni na Kagame hukutana mara kwa mara na iwapo kuna hoja zozote, wao huzisuluhisha.
“Bado tunathibitisha kwamba tuna uhusiano mzuri na Serikali ya Rwanda na raia wa Rwanda.
“Marais Museveni na Kagame walikutana katika mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, na nje ya kikao hicho walizungumza,” alisema Opondo.