27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI GHALI AFRIKA, AMBAO NASA HAIJAONESHA UHALISIA HUO

KENYA inasemekana inatarajia kuendesha uchaguzi ghali zaidi, ambao gharama zake hazijawahi kushuhudiwa si tu nchini humo bali pia katika Bara la Afrika.

Na unaaminika kuwa miongoni mwa uchaguzi ghali kabisa duniani, ukikadiriwa kugharimu Dola bilioni moja sawa na Sh. trilioni 2.2 za Tanzania.

Mfano mdogo wa ughali wake barani Afrika; kwa mujibu wa tathimini, kwa wapiga kura milioni 19 na kitu waliojiandikisha, kila mmoja atagharimu kiasi cha dola 25 sawa na Sh.56,000 za Tanzania.

Agosti 4, Rwanda itatumia Dola milioni 6.5 kuendesha uchaguzi wake mkuu wa tatu wa vyama vingi ukishirikisha wapiga kura milioni 6.8, ikiwa chini ya dola kwa kila mpiga kura.

Uchaguzi Mkuu wa Ghana 2016, ulikuwa na wapiga kura milioni 15.7 na Serikali ilitumia dola 12 kwa kila mpiga kura wakati nchini Tanzania, ikiwa na idadi kubwa ya watu  kuliko Kenya ilitumia Dola milioni 300 katika uchaguzi wake wa 2015.

Kwa msingi huo, kampeni za uchaguzi nchini Kenya si lelemama linapokuja suala la ngawira.

Kwamba wagombea wake wanachomoka fedha nyingi mno kwa ajili ya matangazo, utawala na uratibu, usafiri ukiwamo wa helikopta zinazopishana angani mithili ya daladala.

Unapofikiria ukubwa huo wa gharama, utajiwa na wazo namna gani vyama vikuu vya Jubilee chini ya mgombea wake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto na NASA chini ya mgombea Raila Odinga na mwenza wake Kalonzo Musyoka vitakavyoshindana kwa kampeni za kufa mtu zilivyojaa kila aina ya mbwembwe na madoidoi kupita zile za 2007 na 2013.

Hilo linahusisha uvaaji wa sare rasmi za chama kuanzia kofia, fulana, vitenge, majaketi, vipeperushi, majukwaa yaliyopambika na utitiri wa vipeperushi na mabango barabarani hadi vichochoroni.

Hata hivyo, wakati hali hiyo ikiwa hivyo kwa Jubilee katika kampeni za mwaka huu, ni tofauiti kwa upande wa NASA.

Maswali mengi yamegubika juu ya mwelekeo huo mpya wa kampeni za upinzani, licha ya kuwa vinara wake watano wameonekana huku na kule wakiwinda kura. Kampeni zao zimekosa mbwembwe hizo zilizozoeleka kwa Wakenya.

Kufikia katikati ya mwezi huu, NASA haikuwa bado imenunua kofia, fulana, majaketi vipeperushi na mabango.

Timu ya Raila Odinga pia ilikuwa haijaanza kununua matangazo katika vyombo vya habari kuanzia magazeti hadi televisheni na kuzua wasiwasi wapinzani hawa wana ukata.

Hakuna mabango ya picha za Raila yaliyotapakaa nchi nzima kama 2007 na 2013.

Picha zake zinazoonekana tu katika mabango ya kampeni ni zile za wagombea mbalimbali wa NASA wakiwamo magavana, maseneta, wabunge na wagombea wa mabunge ya Kaunti (MCA).

Tangazo pekee kubwa ni lile linaloonesha vinara watano wa Nasa, likiwa na kauli mbiu ya mabadiliko.

Aidha kampeni ya Raila pia bado haijashuhudia msururu wa magari ya kampeni yenye picha yake na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka.

Ni tofauti na kampeni za wapinzani wao  wa Jubilee

Kwa fikira za haraka za wafuatiliaji wa siasa za taifa hilo wanarudisha nyuma kumbukumbu namna Serikali ya Jubilee ilivyokuwa ikihaha kujaribu kuziba mianya ya uwezekano wa wapinzani kuvuna fedha kutoka nje hasa Mataifa ya Magharibi huku Afrika, Tanzania ikimulikwa zaidi.

Hatua hizo ziliifanya NASA ilie kwa hujuma za mipango yake hiyo ya kupata fedha kutoka kwa marafiki wa kigeni.

Mei mwaka huu kikao cha taasisi za Serikali chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wafanyakazi na Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua  kilikubaliana kufuatilia kwa chati mawasiliano baina ya vyama vya siasa na wafadhili wa kigeni, Nasa ikiwa mlengwa namba moja.

Hicho ni kipindi, ambacho Raila alikuwa amepanga kukutana na baadhi ya wafadhili pembezoni mwa ziara yake mjini Yerusalem, Israel.

Kamati hiyo iliyohusisha maofisa kutoka Hazina, Usalama wa Taifa (NIS), Kurugenzi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato (KRA) kwa chache.

Baada ya safari ya Yerusalem, Odinga anadaiwa alienda Dubai kabla ya kurudi na kutua moja kwa moja kwenye mkutano wa hadhara wa NASA kule Nakuru.

Kwa mujibu wa vyanzo ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Harambee, Tanzania ilikuwa moja ya mataifa yaliyojadiliwa na kumulikwa zaidi.

Wasiwasi dhidi ya Tanzania ulikuja tangu Kenyatta na Ruto wapitishwe kuwa wagombea wa Jubilee katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ambapo kiongozi wa wengi bungeni, Aden Duale alidai Serikali ya Rais John Magufuli imeruhusu kuanzishwa kwa kituo cha kutangaza matokeo ya kura. Hata hivyo, hakutoa ushahidi.

Tuhuma hizo zimerudi kwa nguvu katika wiki za karibuni katika majukwaa ya kampeni ya Jubilee na mgombea mmoja binafsi wa urais. Hata hivyo Tanzania kupitia Ofisi ya Msemaji wa Ikulu pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kikanda Tanzania imekana.

Licha ya mkanusho huo, wasiwasi wa utawala wa Jubilee unatokana si tu urafiki binafsi uliopo kati ya Raila na Rais Magufuli bali pia madai ya karibuni yanayodaiwa kutoka chanzo cha habari ambacho hakikutajwa ndani ya NASA kuwa vituo vyake vya kutangazia matokeo ya urais nchini Kenya, Tanzania na Ujerumani vimekamilika kwa asilimia 100.

Awali Mei mwaka huu, Mhazina wa ODM na Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire, ambaye anasimamia timu ya utafutaji rasilimali, alisema wanategemea kupata msaada kutoka nje wa asilimia zaidi ya 30 ya Bajeti nzima ya kampeni, ambayo hakuwa tayari kuitaja.

“Tutapokea msaada kutoka marafiki zetu nje ya nchi kwa kadiri itakavyotolewa kwa mujibu wa sheria za nchi. Iwe misaada hiyo itakuja au la, tuna uhakika wa kuendesha kampeni zilizojitosheleza kifedha na kusimamiwa vyema zaidi katika dunia hii,” alisema.

Lakini utawala wa Kenyatta uliripotiwa kutoa agizo kali kwa taasisi za fedha ikiwamo benki zote kuwa macho na miamala yoyote inayoingia kutoka nje.

Benki Kuu ya Kenya pia iliweka sheria kali za kuweka na kutoa fedha, huku wanaotoa fedha kuanzia Sh milioni moja za Kenya sawa na Sh. milioni 20 za Tanzania wakitakiwa kutoa maelezo ya walikozitoa na lengo la matumizi.

Aidha kuna minong’ono nchini humo kuwa Jubilee ilimzibia riziki Odinga na kuwapora baadhi ya marafiki zake tajiri kutoka Magharibi mwa Afrika hasa Nigeria mwaka 2013.

Hilo lilianzia wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa Nigeria na ujumbe wake kipindi hicho, Goodluck Jonathan.

Ni pamoja na tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote, ambaye alisemekana alikuwa na nia ya kujenga kiwanda cha saruji kabla ya mpango huo kufutwa baadaye.

Jubilee haikuwahi kuficha kukerwa kwake na uwezekano wa upinzani kupata fedha kutoka nje kufadhili kampeni.

Mwaka jana Ruto alimshambulia Odinga kwa kujaribu kutembeza bakuli kwa mataifa ya Magharibi yasaidie wapinzani katika mataifa yaliyoendelea.

“Mwaka 2013, watu hawa waliwaomba marafiki zao wa Magharibi wajaribu kuingilia chaguzi zetu kwa kufungua kesi dhidi yangu na Rais katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, lakini Wakenya waliona njama hizo wakazikataa.

“Hivyo hivyo mwaka 2017, ni Wakenya watakaoamua wenyewe. Si Magharibi wala fedha zao,” alisema.

Ruto alikuwa akiitikia mwito wa Odinga kwa mataifa ya kigeni kusaidia vyama vya upinzani katika nchi zinazoendelea akieleza namna zinavyopata shida kukabiliana na vyama vilivyo madarakani alivyosema vinatumia fursa hiyo kujinufaisha.

Mwito huo aliutoa katika mkutano wa kimataifa wa kilele wa siasa mjini London, Uingereza Oktoba mwaka jana.

Je, ufuatiliaji huo wa Serikali ni sababu ya NASA kuonekana kana kwamba ina ukata, ambao umeshuhudia kampeni zake kukosa mbwembwe zilizoeleka?

Miezi saba baada ya Raila kutajwa kama mgombea urais wa upinzani na tangazo la timu yake ya kampeni inayoongozwa na Musalia Mudavadi, NASA imeshindwa kuonesha msuli wake, ambao inaweza dalili ya ukata au sehemu ya mkakati kama inavyodai.

Lakini mshauri wa Raila, Salim Lone anadai kwamba wamechelewa kurudi katika utamaduni wao wa kampeni kwa sababu za kimkakati.

Kwa mujibu wa mshauri huyo, kipaumbele cha NASA ni kuwekeza nguvu katika kile alichokieleza rasilimali kubwa zinazohitajika kulinda kura zao.

“Tunajua mahesabu yetu na tunajua mafanikio tuliyofikia katika zile ziitwazo ngome za Jubilee. Tumewekeza nguvu katika kulinda kura kwa vile tulipata somo katika chaguzi mbili zilizopita. Tumewekeza katika mawakala na kuwafunza kulinda kura zetu,” anasema Lone.

Hivyo, anasema wafuasi wa NASA muda si mrefu wataona msuli wao wa kampeni wakati watakapopomika rasilimali kulinda kura zao.

Zaidi ya wasiwasi wa ukata, vyanzo vya ndani vya habari vinasisitiza ukosefu wa rangi zilizozoeleka katika kampeni zao unalenga kutoa picha kuwa wapiga kura wameshaamua na matangazo au malighafi za kampeni hayawezi kuongeza idadi ya kura.

Kwa hili wanasema ni uamuzi wa makusudi kuelekeza fedha za kampeni katika mahali patakaposaidia kulinda kura na kuhamasisha wafuasi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles