TANZANIA  ya leo inaweza kuelezwa kuwa ilikuwa imeshachepuka na kuondoka katika mstari uliokuwa umedhamiriwa na waasisi wake na hususani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye Oktoba 14, itatimia miaka 17 tangu afariki.
Ni sahihi kusema kuwa kimwili hayupo nasi lakini maneno na kauli zake pamoja na mafundisho yake bado yanaishi kutokana na sababu moja kuu kwamba kauli na mafundisho yake hayo yalikuwa ni mwanga na dira  ambayo Tanzania inatakiwa kuifuata.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni wale waliopewa dhamana ya kuiongoza nchi wameonekana kushindwa kufuata mafundisho  aliyokuwa akiyatoa Mwalimu.
Hilo linadhihirishwa kwa mambo ambayo yameibuliwa na Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli. Mojawapo ni suala la kodi ambapo katika mafunzo ya Mwalimu alisema, “Nazungumza habari za kutokusanya kodi. Kutokusanya kodi ni sifa moja ya viserikali corrupt popote pale. Popote, wala usifikiri ni Tanzania peke yake…Serikali corrupt popote pale, haitozi kodi.
“Serikali corrupt inatumwa na wenye mali. Inawafanyia kazi wenye mali. Serikali corrupt itamwambieje mwenye mali, kwamba ‘utalipa, usipolipa utakiona!’ Atacheka tu huyu. Atakwambia ‘unaniambia hivyo wewe? kesho siji basi!
Wakati Serikali ilipoanza kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara na hususani waliokuwa wanapitisha bidhaa zao katika Bandari ya Dar es Salaam na ambao walikuwa hawalipii kodi bidhaa zao hapo ndipo ilionyesha ni kwa jinsi tulivyokuwa tumekengeuka.
Ilikuwa ni dhahiri kuwa Tanzania hii ilikuwa imechepuka na kuondoka katika mstari kwa kulipuuza somo kuhusu kodi alikuwa amelitoa Mwalimu Nyerere.
Hatua hiyo inaonesha kuwa kutolipwa kwa kodi kulitokana na kuchepuka katika mkondo wa kudai kodi na kuingia katika mkondo usio mnyoofu wa kula rushwa na hivyo kuikosesha jamii (Serikali) haki yake ya kupata nyenzo ya kupeleka maendeleo ya wananchi.
Katika mchepuko hatari ni ule wa kutotambua vyeo ni dhamana na vitumike kwa faida ya wote lakini vikawa ndio nyanzo vya kuvuna jasho la mvuja jasho kwani badala ya kuwajibika kwa ajili ya umma ikawa ni kuwajibika kwa ajili yao na wana wao.
Katika mtazamo wa kauli za Mwalimu aliona kuwa baadhi ya viongozi walikuwa wameshapandikiza mazingira ya kupuuza  hisia za utaifa za uzalendo, ujasiri, kujituma, kuwajibika na kwamba walikuwa wamejibadili kitaswira kama watu wanaohama kesho na hivyo kuwa na haja ya kukusanya kila walichokiona ili wakafaidi mbele ya safari.
Taswira hiyo ilionesha kuwa wao ndio waliokuwa na meno na wanajua kutafuna ndio maana leo hii linapotajwa suala kuwa walikuwapo wafanyakazi hewa ndani ya taasisi za umma na kwamba hata marehemu walikuwa wakilipwa malipo hiyo inakuwa ni fedheha ambayo Mwalimu hakuwa ameisahau katika masomo yake.
Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiwabaini kuwapo kwa kadhia ya mambo hewa kuanzia wafanyakazi hewa, malipo hewa na hata wanafunzi hewa ni dhihirisho kwamba mchepuko uliokuwa umefanyika katika enzi za uongozi wa mazoea ulikuwa ni wa kujenga kada ya wavuna jasho wachache walioifurahia keki ya Taifa na wavuja jasho wakiambulia makombo au wakiendelea kusinyaa.
Katika kuchepuka huko ambako nchi iliingia ni dhahiri waliokuwa na dhamana walikuwa wakihanikiza uendelevu wa kuvuna jasho na kuwaacha wavuja jasho wakiwa hoi ndani ya umaskini, ujinga na maradhi na wakishamirisha dhuluma. Hili Mwalimu alilionyea katika masomo yake.
Wavuna  jasho waliiweka kando kanuni njema katika masomo hayo ya kushirikiana na jamii kwa ujumla  kuijenga nchi, badala yake  wakaunda mtandao wao wa kushirikiana kuitafuna nchi.