25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 17 Kifo cha Mwalimu Nyerere, kiongozi yupi wa kufananishwa naye?

julius_nyerere
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

 

Na MWANDISHI MAALUMU,

“KIFO kwanini unatusumbua, tumezaliwa kwa sababu ya kuishi, ulimwengu bila watu si ulimwengu tena, kifo wee! Kifo wee kifo kifo hakina huruma.’’ Haya ni maneno aliwahi kuimba nguli wa muziki marehemu Ramazani Mtoro Ongala kwa jina maarufu Dk. Remmy Ongala.

Ilikuwa majira ya saa sita kasoro dakika tano mchana siku ya Alhamis Oktoba 14, 1999 ghafla redio na runinga zilibadilisha programu zake za kila siku na kuanza kupiga wimbo wa taifa hali iliyopelekea mioyo ya watu kugutuka na kujiuliza nini kulikoni maana leo si siku ya Uhuru au Muungano.

Baada ya wimbo, Rais Benjamin Mkapa alijitokeza kwenye vyombo vya habari huku akibubujikwa machozi yaliyotiririkia ndani ya tumbo ili asionekane mwanaume jina, kisha akawatangazia watanzania kuwa  baba yetu hatunaye tena.

Miaka kumi na saba  tangu baba yetu Nyerere apumzishwe ndani ya nyumba yake ya milele ni kipimo tosha kuelewa kama watanzania wanamuenzi kwa kicheko kwamba aliwaacha kwenye mikono salama ya mrithi au wanaendelea kuwa yatima kutokana na kusulubiwa na baba mdogo aliyeachiwa mkuki.

Julius Kambarage Nyerere akiwa mwalimu kitaaluma huku akiwa anapendelea vilevile  kuitwa mwalimu  kuliko  mheshimiwa au mtukufu anachukuliwa kama miongoni mwa wanafalsafa kutokana  na alivyoliongoza taifa ndani ya mfumo wa ujamaa.

Pamoja na sera ya ujamaa ya kiongozi huyu  kukosolewa na baadhi ya watu ndani na nje ya nchi wakiwamo wasomi, waandishi wa habari  na wanasiasa kuwa ni ya kinadharia  kuliko kuleta maendeleo chanya bado anaendelea kuwa nembo ya kukumbukwa.

Ndugu Lane katika kitabu chake cha ‘‘The New Republic’’ cha mwaka 1999 katika ukrasa wa 16 anasema kuwa Rais mstaafu wa Tanzania ndiye alipelekea kuharibu uchumi wa taifa lenye utajiri mwingi wa rasilimali.

Wakosoaji wanaendelea kudai kuwa ujamaa ulikuwa na changamoto nyingi kutokana na ukweli kwamba ili ulete matokeo chanya, utekelezaji wake ulitakiwa uende sambamba na sera za shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia.

Ikumbukwe kuwa sera za IMF na benki ya dunia ni za masharti katika uendeshaji wake na ndiyo maana inasemekana katika miaka ya themanini mwalimu alipata wakati mgumu kuzikubali kutokana na mfumo wake wa sera ya ujamaa.

Hata hivyo baadhi ya wadadisi wanaona ilikuwa ni vigumu kuleta ustaarabu wa kimaendeleo kwa kuukumbatia mfumo huu maana mwaka 1960 Tanzania na Kenya zilikuwa na maendeleo yanayokaribiana japo Kenya ilikuwa inatuzidi kama asilimia kumi.

Mambo yalikuja kuharibika zaidi mwaka 1967 wakati Tanzania ilipoanzisha Azimio la Arusha ikisisitiza sera ya Ujamaa na Kujitegemea huku Kenya ikiendelea na mfumo wake wenye kufuata soko huru na ubinafsishaji.

(Nnoli, 1978:375) anaonyesha kuwa kutokana na sera tofauti katika mataifa haya mwaka 1973 baada ya miaka sita Tanzania kuanzisha Azimio la Arusha, Kenya ilituzidi kiuchumi kwa asilimia 50 na asilimia 30 ndani ya muongo mmoja kati ya mwaka 1974 na 1984.

Hata hivyo pamoja na ukosoaji huo kitaifa na kimataifa mwalimu Nyerere alijitetea katika kitabu chake cha ‘‘The ideal society’’ cha mwaka 1967 katika ukrasa wa 16 kuwa Ujamaa ulikuwa ni msingi wa kifalsafa wa maendeleo ambao ulikuwa na misingi mitatu ya Uhuru, Usawa na Umoja.

Ni katika fikra ya kuamini uhuru wa mtu au taifa mwalimu hakupenda kuona mtu anaonewa kimabavu au kwa kutumia nguvu ya pesa. Pamoja na kiongozi huyu kuchambuliwa na wadadisi wa masuala ya kisiasa kama mtu aliyeongoza nchi kiimra bado ni anachorwa kama mtetezi wa wanyonge.

Wanaomkosoa mwalimu na kumuona dikteta ambaye aliukandamiza uhuru wa kutoa maoni wanadai kuwa hakupenda kupata ushauri na waliomkosoa walikipata cha moto ikiwemo kupotea kisiasa au kuihama nchi. Ni kiongozi pekee aliyeingilia uhuru wa vyombo vya habari hadi kuwa mhariri mkuu wa magazeti kwa hofu ya wananchi kung’amuka.

Akiwa kiongozi shupavu kwa kutetea uhuru kimaneno alitamka waziwazi kuwa Tanzania haitakuwa huru hadi nchi zote za Afrika zitakapokuwa huru. Mwalimu aliyatimiza maneno kwa vitendo alipoamua kuzipigania kijeshi nchi za Afrika hususan za kusini mwa Afrika.

La kujiuliza katika miaka 17 ya mauti ya baba yetu, ni kiongozi yupi katika nchi yetu au Afrika mwenye moyo kama huo iwapo ndugu Mohamari Ghadafi alivamiwa na nchi za magharibi na kuuawa kama kuku huku viongozi wetu wakiogopa ili wasipoteze mkate wa kuombaomba?

Akionekana kiongozi mwenye sauti ya mamlaka na matumaini katika shida,  wakati wa kumtwanga Nduli Idd Amin wa Uganda alipovamia mipaka mwaka 1978 ili kuchezea uhuru wetu, Mwalimu alisema  sababu, nia na uwezo wa kumpiga tunao. Hata kama vita hiyo inasemekana palikuwepo na jambo nyuma ya pazia.

Je, viongozi wetu wa sasa wanao moyo wa kujenga matumaini mapya ya wananchi wanapokumbwa na matatizo ya ghafla au wanajiweka kando na kutumia lugha za kuvunja moyo kwa kuwaambia wananchi waliowapigia kura wajitafutie ufumbuzi maana serikali haijasababisha majanga?

Kwa namna baba wa taifa alivyoamua kuacha raha za Ikulu na kuvaa sare za kijeshi na kukimbilia Kagera ili kuwatia moyo wapiganaji huku akiwahamasisha wananchi wachangie chakula cha askari, sina uhakika kama viongozi wa kileo wako tayari kufanya hivyo ndani ya muda mfupi baada ya kutokea maafa!

Katika usawa mwalimu hakuwa mbabaishaji kwani pamoja na sera yake ya ujamaa kukosolewa kuwa ni chanzo cha umasikini, lakini alijitahidi ili rasilimali zilizopo zigawiwe kwa kila mtanzania kulingana na jasho lake.

Ni kweli wapo wakosoaji wanaomuona mwalimu kama kiongozi aliyetumia mabavu kusimika ujamaa wakati mataifa mengi ya Afrika aliyotaka yawe na usawa yamejaa rushwa na ufisadi, lakini ikumbukwe kuwa ni kiongozi huyu aliyeonyesha mfano kwa kuwabana wahujumu uchumi katika miaka ya themanini huku wapokeaji na wala rushwa wakitamani ardhi ipasuke.

Pamoja na jitihada zilizopo kwa viongozi wa sasa katika kumuenzi shujaa huyu bado ni vigumu kutambua kama usawa upo endapo nafasi za juu za uongozi katika vyama au serikali zilizo nyingi hazitolewi kitaaluma bali ni kwa kujuana kama si kujipendekeza kiumbea kwa bwana mkubwa.

Je, viongozi wa vyama na serikali wanapokula mkate wa taifa na familia zao mpaka wananawiri huku wakiwaambia wananchi wakalime kwa jasho tena juani ili wajitafutie riziki vinginevyo hawatapatiwa msaada wa chakula bila kuweka mifumo ya umwagiliaji katika sehemu kame, kuwapatia pembejeo na wataalamu wanamuenzi mwalimu?

Ni viongozi wepi wanaoongoza kwa vitendo huku wakiziacha ofisi zao na kwenda kulima kwa jembe la mkono tena maeneo ambayo ni makame na hayana rutuba ili kujua ugumu ulivyo kama mwalimu alivyokuwa akilima Butiama?

Nyerere katika kitabu chake fulani cha mwaka 1968 anasema kuwa alitaka kujenga jamii yenye furaha ambayo haina migogoro kati ya mtu na mtu. Ni katika muktadha huu mwanasiasa huyu alionekana anataka umoja.

Mwalimu aliamini kuwa watu wakiwa na umoja wataweza kuwa na maendeleo. Imani yake ya umoja ilikuja kudhihirika waziwazi alipohakikisha Tanganyika na Zanzibar zinaungana mwaka 1964 japo kuna malalamiko ya kuwa muungano huo haukuwashirikisha watu wengi ndio maana una kero zisizoisha.

Mwalimu ni kiongozi pekee ambaye katika enzi za uhai wake aliutetea na kuulinda muungano kwa tahadhari kubwa huku akijihadhari kutumia kauli ambazo zinaweza kuwasha moto badala ya kuzima. Nani hakumbuki kuwa Nyerere alikuwa akitumia mafumbo ili kuzima nguvu ya Uzanzibari na Uzanzibara?

Kimataifa alihakikisha Tanzania inaungana na taasisi nyingine za kimataifa mfano umoja wa nchi huru za Afrika siku hizi ni umoja wa Afrika AU, Umoja wa nchi za kusini mwa Afrika SADC, nchi za Afrika Mashariki, umoja usiofungamana na upande wowote na Umoja wa Mataifa.

Je, viongozi wetu baada ya kifo cha mkombozi huyu, mbali na kuendelea kubaki katika jumuiya hizi wanaitetea nchi kimataifa ili ipate maendeleo? Je, safari nyingi nje ya nchi zenye kutumia pesa za walipa kodi ni za manufaa au anasa?

Je, viongozi wetu wakiamua kujitenga na kuamua kukaa ndani ya nchi bila kushirikiana na wenzao si watajikuta wakisusiwa na hatimaye kukosa fursa ambazo hatuwezi kuzipata hapa nchini mfano teknolojia ya viwanda na ulinzi?

Mwalimu Nyerere kutokana na kupenda umoja wa watu hata baada ya kung’atuka madarakani aliendelea kushughulikia migogoro ya kimataifa mfano Burundi. Ni kiongozi huyu aliyemshauri rafiki yake Keneth Kaunda wa Zambia kuachana na kung’ang’ania madarakani ili nchi isiingie kwenye migogoro.

Ni kiongozi yupi ndani au nje ya taifa letu ambaye yuko tayari kushughulikia migogoro kwa uwazi bila kuoneana aibu kama si kulindana kwa hofu ya siku moja kutenda makosa yaleyale? Migogoro ya ulafi wa madaraka inayoendelea Burundi na DRC huku viongozi wa kikanda wakiweka magego nje ni ushahidi tosha.

Kitendo cha mwalimu kung’atuka hapo mwaka 1985 ili wengine waongoze hata kama baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wanadai ni baada ya kuona sera yake ya Ujamaa haiwezi kuendelea kuwa hai, ni cha ushujaa kuliko akina Robert Mugabe, Paul Kagame, Edward Dos Santos na wengine wengi wanaotaka kufia madarakani au kuona nchi ikiwaka moto.

Ni mfumo huu wa kuachiana madaraka unaichora Tanzania katika ramani ya dunia kuwa ina viongozi wastaarabu japo baadhi ya wakosoaji wakiona kama kiini macho cha demokrasia maana hakuna kubadilishana kati ya chama na chama.

Baba yetu wakati amelala kitandani katika hospitali ya mtakatifu Thomas jijini London huko Uingereza, alipoona amezidiwa na matumaini ya kupona hayapo alisema kwa huzuni kuwa watanzania anawapenda ila hana jinsi kifo lazima kitamchukua,  atakachofanya ni kutuombea kwa Mola tubaki salama.

Maombi ya Mwalimu aliyoyaacha yalete umoja wa kitaifa ambapo watu/wanasiasa wanaweza kutofautiana katika itikadi za vyama vyao lakini wakashirikiana bila kutumika nguvu ya dola, yalete utawala wenye kuheshimu sheria na haki za binadamu, maombi yalete maridhiano katika Muungano bila kusahau katiba iliyoko mbele yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles