Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
BEKI wa Simba, Mohamed Hussein, ‘Tshabalala’, amesema amethibitisha kufanya mazungumzo na waajiri wake hao, lakini anatarajia kukalizana nao baada ya michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon).
Tshabalala ni miongoni mwa wachezaji 39 wa kikosi cha awali cha timu ya Taifa, Taifa Stars walioko kambini katika Hoteli ya WhiteSands wakijinoa kwa Afcon, ambayo inatarajia kuanza Juni 21 na kumalizika Julai 10, nchini Misri.
Beki huyo wa kushoto pamoja na Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na makipa Aishi Manula na Said Mohammed ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliomaliza mikataba yao msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulipofikia tamati. .
Akizungumza na MTANZANIA jana, Tshabalala alisema tayari ameanza mazungumzo na klabu hiyo kuangalia uwezekano wa kuongeza mkataba mwingine lakini zoezi rasmi la kuanguka saini anatarajia kulifanya baada ya Afcon.
“Nimeshafanya mazungumzo na viongozi, kila kitu kitakuwa wazi baada ya Afcon kumalizika,” alisema Tshabalala ambaye pia mchezaji wa zamani wa Kagera Sugar.
Tshabalala ni moja ya mabeki wanaotegemewa katika kikosi cha Simba chenye makao yake makuu Msimbazi , Dar es Salaam.
Msimu iliopita alikuwa katika kiwango bora kilichoisaidian Simba kutete ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kufika robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.