Mwandishi Wetu- MAELEZO
MKUTANO wa kujadili hatima ya wakimbizi unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu kwa kuzijumuisha nchi za Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).
Kutokana na hali hiyo, mkutano huo utajadili namna ya kuwarejesha nchini mwao wakimbizi hao kwa kuzingatia sheria za kimataifa zinazohusu wakimbizi.
Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi Idara ya Huduma za Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke, ambapo alisema tangu ulipotolewa wito wa kuwataka wakimbizi wa Burundi kurejea nchini mwao kwa kuwataka wajiorodheshe wengi wameonyesha nia ya kurejea nyumbani kwao.
Agizo hilo la Rais Dk. John Magufuli, alilitoa hivi karibuni, ambapo alisema hadi kufikia Agosti mosi (juzi) jumla ya wakimbizi 6,700 ambao ni raia wa Burundi wameshajiorodhesha kurejea nchini mwao kwa hiari.
Kwa mujibu wa Mseke, hivi sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 276,692 kati ya wakimbizi 348,019 walioko nchini. Wengine ni wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 70,840, Wasomali 150 na wengine (mchanganyiko) 337.
Alifafanua kuwa kati ya idadi hiyo ya wakimbizi raia wa Burundi 242,340 waliingia nchini baada ya Aprili, 2015 kufuatia machafuko ya kisiasa nchini humo.
Akizungumzia mwendo wa uingiaji wakimbizi kutoka Burundi, alieleza kuwa kwa sasa kasi imepungua kutoka wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kati ya Agosti hadi Desemba, 2016 hadi wastani wa wakimbizi kumi kwa siku katika miezi ya hivi karibuni.
“Januari mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifuta tamko la Primafacie alilolitoa mwezi Mei, 2015 ambalo linataka wakimbizi wanaokimbia machafuko nchini kwao waruhusiwe kuingia kwa makundi bila ya utambuzi,” alisema Mseke.
“Kwa wastani wa wakimbizi 1,000 kwa siku kuanzia Januari, 2017, tungekuwa tunapokea wastani wa wakimbizi 30,000 kwa mwezi na hadi kufikia sasa tungekuwa tumepokea wakimbizi wapatao 240,000,” alisema.
Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza imekuwa ikiwapatia uraia wakimbizi kutokana na hali halisi ambapo mwaka 1983 wakimbizi 32,000 raia wa Rwanda walipewa uraia.