31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yabaini matumizi bandia Sh bilioni 1.4 ujenzi stendi mpya Dar

CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala, imefanya uchunguzi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi Louis, Dar es Salaam na kubaini ubabaishaji wa zaidi ya Sh bilioni 1.4.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Elizabeth Mokiwa, akitoa taarifa ya Aprili hadi Juni jana, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ubabaishaji huo ulisababisha mradi huo kusuasua baada ya baadhi ya mahitaji kupandikiziwa.

Alisema Takukuru kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji, Spora Liana, walibaini upotevu wa fedha hizo na kusababisha mradi kushindwa kuendelea kwa kasi iliyokusudiwa.

Alisema thamani ya mradi huo ilikuwa ni Sh bilioni 50.9 na hivi sasa unaendelea vizuri kama ilivyokusudiwa.

“Baada ya kuona mradi unasuasua, Takukuru iliingilia kati na kufanya uchunguzi ambapo tulibaini kuna baadhi ya vifaa vimewekewa fedha zaidi tofauti na madai halisi,” alisema Elizabeth.

Aliongeza kuwa Takukuru pia inaendelea kufanya uchunguzi wa mgawanyo wa fedha Sh milioni 77.5 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa lengo la kupambana na virusi vya corona kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Alisema watafuatilia fedha hizo za mradi wa Water Sanitation and Hygiene (WASH) endapo umefika kwa walengwa kama ilivyopangwa.

“Takukuru tunaendelea kufuatilia fedha hizo kama kweli zimetumika kwa matumizi hayo,” alisema Elizabeth.

Wakati huohuo, Takukuru Ilala inaendelea kuchunguza tuhuma za ubadhilifu wa fedha Sh bilioni 1.6 uliofanywa na Chama cha Ushirika cha Talgwu.

Elizabeth alisema ubadhilifu huo ulifanywa kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 na uchunguzi wa jambo hilo upo hatua za mwisho kukamilika.

Aidha alisema Takukuru Ilala inaendelea kufanyia kazi mgogoro wa ardhi katika Mtaa wa Mbondole, Kata ya Msongola kuhusu ufunguaji wa mipaka ya viwanja vilivyotajwa kuwa ni vya walimu.

“Takukuru imeamua kuingilia kati suala hilo ili haki iweze kutendeka,” alisema Elizabeth.

Elizabeth alisisitiza kuwa katika kipindi cha utendaji kazi wao cha Aprili hadi Juni wamefungua kesi mpya tano na mashauri 22 yanaendelea mahakamani.

“Pia katika kipindi hicho cha robo mwaka tumefanikiwa kushinda kesi tatu, kutoa elimu kwa wanafunzi na umma pia,” alisema Elizabeth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles