MANCHESTER United hawana mpango wa kumfuta kazi kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer, licha ya kupoteza mechi tatu kati ya nne za hivi karibuni.
Solskjaer anakabiliwa na presha kubwa ya kuipa mataji timu hiyo, hasa baada ya mkwanja mrefu aliotumia kuimarisha kikosi, ikiwamo kuwasajili Raphael Varane, Jadon Sancho na Cristiano Ronaldo.
Hata hivyo, suala la kutimuliwa katika siku za hivi karibuni halionekani kuwapo kwani mabosi wa Man United wanaamini bado Solskjaer mwenye umri wa miaka 48 anawafaa.
Kwa mujibu wa taarifa, anayeshilia msimamo wa kocha huyo kuendelea kupewa muda ni Makamu Mwenyekiti wa Mashetani Wekundu hao, Ed Woodward, ambaye alimpa mkataba wa miaka mitatu miezi michache tu iliyopita.