Khamis Sharif, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeandaa mpango maalumu wa kuhifadhi chakula cha akiba kwa ajili ya kukabiliana na majanga yote yanayoweza kujitokeza visiwani humo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dk. Makame Ali Usi aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo mwa mji wa Z’bar wakati akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, Suleiman Saharan Said aliyetaka kujua mpango wa serikali kuweka chakula cha akiba.
Alisema katika kutekeleza lengo hilo, SMZ kwa mara ya kwanza imeweza kuhifadhi jumla ya tani 338 za mchele unaotoka nchini Pakistani katika ghala la hifadhi Malindi.
Aidha alisema lengo la mpango huo ni kuhifadhi mpunga utakaonunuliwa kutoka kwa wakulima wa Zanzibar.
“Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, hivi sasa inatekeleza mradi wa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji kwa kuongeza eneo la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 1,524,” aliongeza.
Alieleza kuwa mpango huo unatekelezwa kupitia benki ya EXIM ya Korea, ili kuongeza uzalishaji wa mpunga na kupunguza utegemezi wa chakula nchini.
Katika kutekeleza mpango wa hifadhi ya chakula cha akiba, alisema iliamuliwa kwamba maghala yatakayotumika ni ghala la Malindi lililopo Unguja na ghala la Tibirinzi kisiwani Pemba.
Kuhusu ghala la Malindi alisema lina uwezo wa kuhifadhi tani 500 na tayari limekwishakarabatiwa na linatumika kuhifadhia mchele na ghala la Tibirinzi Pemba bado halijakarabaitiwa na kwamba taratibu zinaendelea.
Katika hatua nyingine alisema wizara ipo katika matayarisho ya ujenzi wa maghala mawili ya kuhifadhia mpunga katika eneo la Cheju Unguja na Dodeani- Ole kisiwani Pemba.