Polisi wajipanga ikishuhudia uchaguzi wa kwanza Serikali za Mitaa 2019

0
855

Raphael Okello -Bunda

WAKATI Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019 ukiwa ni wa kwanza katika Halmashauri ya mji wa Bunda   tangu ilipotengwa rasmi, vyombo vya dola vimeeleza bayana kuanza kujipanga kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi huo unatawaliwa na amani.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Bunda mkoani Mara, Hamisi Waryoba amesema atahakikisha Uchaguzi  wa Serikali  za Mitaa mwaka huu wilayani Bunda unakuwa huru  na haki.

Alisema hatamwonea mtu yeyote hivyo amewataka wote watakaojihusisha katika masuala ya uchaguzi  kufuata sheria, kanuni na taratibu zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 kama zilivyoanishwa katika mwongozo.

Waryoba  alisema hayo juzi alipokuwa akijitambulisha  kwa madiwani  nawatendaji  katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda ambapo alisema  uchaguzi ni shughuli nyeti inayowaletea wananchi viongozi  bora waliowachagua wao wenyewe  hivyo ni vyema ufanyike katika mazingira huru na haki.

Alisema anao uzoefu wa kutosha  katika historia ya wilaya ya Bunda hivyo wakazi  wa eneo hilo wasiwe na hofu na kwamba yeye ni muumini wa polisi shirikishi (polisi jamii) na  ameomba ushirikiano mkubwa toka kwa jamii.

Tayari msimamizi wa Uchaguzi  wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya  Bunda, Wiliam  Wakili  ametangaza jumla ya mitaa 88 katika kata 14 za Halmashauri  ya  Mji wa Bunda ambayo wananchi wake watashiriki  katika uchaguzi  kupata viongozi wa serikali za mitaa yao.

Awali Mbunge wa kitaifa kutoka Mkoa wa Mara, Amina Makilagi aliwataka wanawake wenye sifa  kuwania nafasi  hizo za uongozi katika serikali za mitaa.

Alisema  nafasi hizo ziko wazi kwa raia yeyote wa Tanzania mwenye sifa kugombea bila kujali jinsia, rangi, dini au kabila huku akisema akina mama wanayo nafasi kubwa kuchaguliwa kwa kuwa wana nguvu kubwa katika jamii.

Uchaguzi  wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 unakuwa ni uchaguzi wa kwanza katika halmashauri ya mji wa Bunda  tangu  halmashauri hiyo itengwe rasmi kutoka halmashauri mama ya Wilaya ya Bunda na kupata madiwani  na mbunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Mwaka 2016 wenyeviti  wa vitongoji waliochaguliwa katika uchaguzi  waserikali za mitaa mwaka 2014 walisitishwa kufanyakazi kwa mujibu wa sheria za Serikali za Mitaa na Halmashauri ya miji  huku usimamizi  wa shughuli zote  za kiuwakilishi  zikiachwa  kwa madiwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here