Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa amesema alimpenda Rais Dk. John Magufuli tangu akiwa Mbunge wa Karatu.
Dk. Slaa ambaye alitangaza kuachana na siasa mwaka 2015 kwa kutofautiana na chama chake katika kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, alitoa kauli hiyo jana alipokutana na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Novemba 22 mwaka jana, Rais Dk.Magufuli alimteua Dk. Slaa kuwa balozi siku chache baada ya gazeti hili kuripoti taarifa za kiongozi huyo zamani wa Chadema, kuajiriwa katika duka kubwa la bidhaa za majumbani (Supermarket) la Costco lililopo Oakville, Toronto nchini Canada.
Dk. Slaa aliongoza jimbo hilo kwa vipindi vitatu mfululizo kuanzia mwaka 1995 hadi 2010, baada ya kuteuliwa na Chadema kuwania urais.
Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine Dk. Slaa alisema huwa wapinzani wanawekwa pembeni lakini yeye hakuwahi kuwekwa kando na Rais Magufuli wakati huo akiwa waziri.
“Ni kweli kukupenda (Rais Magufuli) haikuanza leo ni tangu ukiwa waziri tukiwa bungeni ulifika Karatu hukuniweka pembeni nadhani si kawaida kwa sababu wapinzani huwa wanawekwa pembeni mara nyingi lakini mimi hukuniweka pembeni,” alisema Dk. Slaa.
Alisema akiwa upinzani alipiga kelele kwa sababu kulikuwa na upungufu lakini kwa sasa ana furaha kwani yale ambayo alikuwa akiyapigia kelele yametekelezwa.
“Wakati ule nilipiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kwamba kuna upungufu, leo nina furahi yale ambayo nilikuwa nayapigia kelele yanatekelezwa kwa sababu nimeyaona…sasa kitu kikubwa ni macho.
“Ushabiki katika maendeleo hauna tija, ushabiki katika siasa nao hauna tija. Kama nilivyoeleza huko nyuma siasa ni sayansi wapo wanaofikiri kuwa siasa ni upotoshaji.
“Sasa siasa kama ni sayansi ina misingi yake ambayo inahitaji kusimamiwa, utendaji wa Rais una mambo kadhaa ya msingi ambapo jambo la kwanza; ni mtu mwenye maono au hapana, nafiriki Rais ana mtazamo kwa sababu huwezi kubuni mengi ya mambo haya yaliyofanyika kwa muda mfupi kama huna mtazamo.
“La pili ni uthubutu; si watu wengi sana wanaweza kufikiria kufanya jambo na ndani ya muda mfupi, akaweza kutafuta njia ya kukitekeleza jambo hilo, unapokuwa jasiri unachukua hatua kwa sababu unaamini unachofanya ni kwa ajili ya manufaa ya nchi yako,”alisema Dk. Slaa.
Kwa upande wake, Rais Dk. Magufuli alimpongeza Dk. Slaa kwa moyo wake wa kizalendo huku akisema alimteua kuwa balozi kwa kuwa anatambua ataweza kupigania masilahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.
“Dk. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo (jana), tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi.
“Dk. Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Uamuzi wa Dk. Magufuli kumsifu Dk. Slaa kwa mara ya kwanza alimsifu kiongozi huyo wakati wa kampeni za Uchaguz Mkuu wa mwaka 2015, alipokuwa akiomba kura wilayani Karatu ambapo alimsifu kutokana na msimamo wake wa kizalendo ikiwemo kukataa kukumbatia ufisadi.
Alisema kama Dk. Slaa, angekuwa anagombea ubunge angemnadi bila kujali chama chake anachotoka.
Wakati huohuo, Rais Magufuli aliagana jana na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wamestaafu baada ya kutimiza umri.
Walioagana na Rais ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa (JWTZ) na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa, Brigedia Jenerali William Kivuyo, Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.