24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA LOWASSA, NJOLAY WAMVAA KIGANGWALLA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ametoa tuhuma nzito kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na Balozi Daniel ole Njolay, huku watuhumiwa hao wakidai anakurupuka.

Kigwangalla amedai Lowassa, akishirikiana na Njolay, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, walipanga njama za kukata eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), lililopo Arusha na kuligawa kwa wananchi.

Alisema viongozi hao walishirikiana na watumishi wa zamani wa NCAA, Halmashauri ya (Manispaa) sasa ya Jiji la Arusha na Bodi ya Utalii (TTB).

Hata hivyo, kauli hiyo ya Kigwangalla, imejibiwa vikali na Balozi Njolay na mtoto wa Lowassa, Fredrick ambaye ni msemaji wa familia, ambao wamedai waziri huyo anakurupuka.

Wakati Kigwangalla akitoa tuhuma hizo jana, wiki iliyopita, alitoa ilani ya siku 30 kwa watu waliojenga nyumba eneo hilo kuhama, wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu.

Jana akiwa jijini Arusha, alisema Balozi Njolay akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Lowassa, walipanga mbinu za kuvamia ekari 20 kati ya 40 mali ya NCAA.

Akizindua Bodi mpya ya NCAA, Dk. Kigwangalla mbali ya kuwatembeza wajumbe wa bodi hiyo kwenye kiwanja hicho, aliwataka kuhakikisha wanaanza jukumu la kukirejesha mikononi mwa NCAA.

“Hapa hakuna mgogoro, wakazi 83 waliouziwa viwanja na kujenga warudi kwa aliyewauzia, atajua hati alizowapa alikozitoa, huwezi kutoa hati juu ya hati. Ni hati moja tu iliyopo kwa Kamishna wa Ardhi,” alisema Dk. Kigwangalla na kuongeza:

“NCAA walinunua ekari 40 kwa bilioni 1.8/-, hawa wavamizi wamechukua ekari 20, wajumbe wa bodi hakikisheni mnasimamia hili, kila kitu kipo wazi, hawa ni wavamizi,” alisema.

 

NJOLAY AMJIBU

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu mjini hapa jana, Balozi Njolay alipinga kitendo cha Dk. Kigwangalla kuwaita wakazi hao 83 waliomilikilishwa maeneo hayo kisheria kuwa ni wavamizi.

“Ametudhalilisha, kuvamia ni kuingia eneo kwa nguvu bila ruhusa. Sisi hatukuingia hapa kwa kuvamia. Eneo hili limepangwa, likagawiwa na kumilikishwa na mamlaka kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Namheshimu sana waziri, lakini kufikia kutuita sisi ni wavamizi, nadhani hakutumia busara, nadhani busara zaidi ingemtuma kuziita pande zote; NCAA, wakazi 83 wenye hati zao na Jiji wakazungumza.

“Au angeunda kikosi kazi ili kichunguze ilikuwaje eneo hilo likagawanywa, sasa iweje leo aibuke tu na kutudhalilisha? Nimekuwa mfanyakazi serikalini kwa miaka 16, nimefanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu.

“Waziri si eneo la kusema chochote anachotaka, nimpe ushauri wa bure aunde ‘task force’, haiwezekani watu wote 83 wakaingia kwenye eneo hilo bila kufuata sheria.

“Taratibu za Serikali zisichanganywe na siasa, tukienda kihuni namna hiyo hatutakuwa tunamsaidia Rais Dk. John Magufuli. Ninaamini kila mtu ana haki ya kupata na kumiliki ardhi katika nchi hii.

“Ukimilikishwa ardhi huwezi kunyang’anywa eti kwa sababu ya tofauti za kiitikadi za kisiasa.

“Lakini pia kuna mambo mengi ya kufanya ni kwanini asishughulike na kuzuia ujangili, nilikuwa namheshimu,” alisema Balozi Njolay.

Eneo linalodaiwa kuvamiwa lilikuwa likimilikiwa na TTB kabla ya Serikali kulichukua na kuliuza ambapo NCAA walifanikiwa kulinunua tangu mwaka 2006.

Aidha wakati NCAA wakinunua eneo hilo mwaka 2006, tayari iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha mwaka 1996 ilikuwa imekwishakumega ekari 20 na kuziuza kwa watu walioomba kumilikishwa ardhi kisheria.

Na NCAA walipokuwa tayari kuendeleza eneo hilo mwaka 2007, ndipo walibaini ekari 20 kati ya 40 walizolipia Sh bilioni 1.8 zilikuwa zimevamiwa na kujengwa nyumba za makazi, shule na makanisa.

Hata hivyo, Mhifadhi Mkuu wa NCAA na Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi, Dk. Freddy Manongi, aliwaeleza wajumbe wa bodi kwamba katika majadiliano kuhusu eneo hilo, Halmashauri ya Jiji la Arusha iliomba kuwatafutia eneo jingine kama fidia.

 

KAULI YA LOWASSA

Kwa upande wake, mtoto wa Lowassa, Fredrick, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema: “Nimesikia taarifa za Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla akitaja jina la Lowassa kama mmoja ya watu eti walioshiriki kupora ardhi Arusha.

“Nimesikitishwa sana na matamshi hayo kutoka kwa waziri ambaye kwa mtu mwenye wadhifa wake, kutoa kauli zisizo na msingi wowote na kulaghai umma.

“Nimemfahamu Mhe Kigwangalla kwa miaka mingi, tangu wakati anavurugana na mbunge mwenzake wa Nzega na rafiki yangu Mhe Hussein Bashe kule Nzega.

“Kwa maoni na mawazo yangu, nimekuwa nikiamini kwamba Kigwangalla atakuwa mtu aliyebadilika na kujifunza kutokana na makosa yake ya nyuma.

“Kauli yake ya leo ni ushahidi kwamba bado ana matatizo yale yale ya kukurupuka.

“Ni wazi hata baada ya mambo mengi kubadilika na pengine nyakati za kuchafua watu kukoma, ndugu huyu bado anaishi nyakati zile zile.

“Ni wazi Kigwangalla anatumia vibaya dhamana aliyopewa na Rais Magufuli, kwa mambo ambayo Wizara ya Ardhi ina wataalamu na uwezo wa kuchukua hatua stahiki kwenye mgogoro wowote.

“Nikiwa kama msemaji wa familia, ninazo katika kiganja cha mikono yangu taarifa zote za umiliki wowote unaomgusa Lowassa.

“Ninaweza kuuhakikishia umma kwamba yote aliyosema Waziri Kigwangalla hayapo, na kama anayo basi sisi tuko tayari afanye lolote lililo chini ya mamlaka yake badala ya kurejea kule tulikopita, ambako yeye na wenzake kadhaa walifanya bila mafanikio kuchafua heshima za wote anaowataja bila sababu.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles