Na BRIGHITER MASAKI.
MREMBO aliyewahi kushiriki shindano la Miss Tanzania mwaka 2014 na kushinda kisha kupokwa taji hilo, Sitti Mtemvu (Sitti), ameibuka na kuweka wazi kwamba alikuwa kimya muda mrefu kwa kuwa alirudi masomoni nchini Marekani kwa ajili ya kusaka cheti.
Sitti alisema wakati Rais Magufuli alivyoagiza wasio na vyeti wachunguzwe, aliamua kurudi chuoni nchini Marekani kwa ajili ya masomo na kupata vyeti kwa ajili ya kumsaidia kuendesha harakati alizokuwa amezianzisha baada ya kupokwa taji la Miss Tanzania kwa madai ya kudanganya umri mwaka 2014.
Sitti, ambaye alifanikiwa kushinda taji hilo kisha ushindi wake kutenguliwa na kupewa aliyekuwa mshindi wa pili, Lilian Kamazima, ameliambia MTANZANIA kuwa, kimya chake cha muda mrefu kitafikia kikomo hivi karibuni, atakapoendeleza harakati zake, ikiwamo uandishi wa kitabu chake cha Chozi la Sitti ni Kampuni yake.
“Kimya changu kwa muda mrefu ni kutokana na kurudi masomoni Marekani kisha kupata vyeti, lakini kwa sasa nimeshamaliza na mambo mbalimbali yataendelea, ikiwamo uzinduzi wa taasisi yangu ya Sitti,” alisema Sitti.