23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DPP ASUBIRI FAILI LA LOWASSA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, amesema anasubiri Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imalize uchunguzi wake dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, alihojiwa juzi kwa DCI kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi na kuandika maelezo ya onyo.

Alijidhamini mwenyewe na leo anatakiwa kurudi tena katika ofisi hizo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mganga alisema kwa sasa hawezi kusema lolote kwa sababu DCI bado anaendelea na uchunguzi wa suala hilo.

Alikuwa akijibu swali aliloulizwa na MTANZANIA kuhusu uchunguzi unaoendelea dhidi ya Lowassa na kama atafikishwa mahakamani iwapo itabainika kuna jinai.

Mganga alisema kuwa hawezi kufanya kazi kwa hisia ila anasubiri kuona nini kitatokea katika suala hilo.

“Huwa sifanyi kazi kwenye assumption (hisia), tusubiri tuone kama litatokea,” alisema Mganga.

Wakati DPP akieleza hayo, leo Lowassa ametakiwa kurejea tena katika Ofisi ya DCI kujua hatima yake kama ana kesi ama la.

Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Ijumaa iliyopita wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ni jambo la fedheha kwa nchi kuwaweka mahabusu masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara Zanzibar (Jumuki) maarufu Uamsho kwa miaka minne bila kesi kuamuriwa.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kutoka polisi, Lowassa alisema baadhi ya watu waliitafsiri kauli aliyoitoa wakati wa futari hiyo kwamba ni ya uchochezi.

Alisema kwa mtazamo wake hakuna kosa alilofanya na kwamba alikuwa anatekeleza sera ya chama chake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika mahojiano yaliyofanyika katika ofisi ya DCI Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam, mwanasheria wa Lowassa, Peter Kibatala, alisema mteja wake alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi kuhusu matamshi aliyoyatoa wakati wa futari hiyo.

“Lowassa alipokea wito kutoka ofisi ya DCI kwamba aripoti leo (juzi) saa 4.00 asubuhi. Mahojiano yalijikita katika kile kinachodaiwa kwamba ni kauli za uchochezi.

“Amechukuliwa maelezo yake ya onyo na amejidhamini mwenyewe, atatakiwa kurudi tena polisi kesho (leo),” alisema Kibatala.

Lowassa aliwasili polisi juzi saa 3:58 asubuhi akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji na wanasheria kadhaa.

Hata hivyo aliingia ndani na Wakili Kibatala huku watu wengine akiwamo Dk. Mashinji wakizuiliwa getini.

Alitoka saa 8:05 mchana na kwenda nyumbani kwake Masaki.

Taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA kuwa katika mahojiano hayo, Lowassa aliwekewa mikanda ya video mbalimbali kuhusu matamshi aliyotoa wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 yanayohusu ahadi yake ya kuwatoa kizuini masheikh wa Uamsho.

Baada ya kuwekewa video hizo, alitakiwa kueleza kwa kina kauli zake hizo zilikuwa na maana gani kwa usalama wa nchi.

Pamoja na hali hiyo, inaelezwa kuwa bado Lowassa alisimamia msimamo wake wa kuona hakuna sehemu aliyotamka uchochezi.

Hata hivyo ilipotimu saa 8:53 mchana, Lowassa alizungumza na wanahabari nyumbani kwake Masaki akiwataka wanachama wa Chadema wasiwe na hofu kwa sababu alikuwa anatekeleza sera ya chama chake.

“Nilikwenda polisi na kuhojiwa juu ya hotuba niliyoitoa kwa Waitara wakati wa futari, kuna watu wameitafsiri kwamba ni uchochezi. Polisi wana shaka, hivyo wana haki ya kunihoji.

“Niwahakikishie wanachama wenzangu hatujafanya kosa lolote, tulikuwa tunatekeleza sera ya chama chetu, wakae salama wasubiri taratibu zifuatwe,” alisema Lowassa.

Hata hivyo, hakuwa tayari kujibu maswali zaidi ya waandishi wa habari kwa kile alichodai kuwa atakuwa anaingilia kesi hiyo.

“Siwezi kutoa ‘details’ za mazungumzo kwa sasa, nitakuwa nje ya utaratibu na nitaonekana naingilia kesi, tusubiri wakati mwingine nitaongea zaidi,” alisema.

Mwaka 2011 viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki), wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kusababisha uharibifu wa mali za watu na Serikali na kuhatarisha usalama wa taifa.

Mara kadhaa wamekuwa wakifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto, wakishtakiwa kwa ugaidi.

Mbali na kina Sheikh Farid, kesi za ugaidi zaidi ya 20 zinaendelea mahakamani zikiwahusisha washtakiwa zaidi ya 60.

Viongozi wengine wa Uamsho walioshtakiwa pamoja na Sheikh Farid ni Msellem Ali Msellem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48) na Suleiman Juma Suleiman (66).

Wengine ni Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakar Suleiman (39), Gharib Ahmad Omar (39), Abdallah Said Ali (48) na Fikirini Majaliwa Fikirini (48), wote kutoka Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles