26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Siri kifo cha Dk. Didas Masaburi yafichuka

masaburiVERONICA ROMWALD NA MAULI MUYENJWA –  DAR ES SALAAM

SIRI ya kifo cha Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi (56),  imefichuliwa ambapo imebainika kuwa kiongozi huyo amefariki dunia kwa ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis B).

Dk. Masaburi alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  (MNH) na anatarajiwa kuzikwa Jumatatu Oktoba 17, mwaka huu Chanika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jna,  msemaji wa familia, Otieno Igogo alisema wakati wa uhai wake Dk. Masaburi alikuwa akisumbuliwa na homa ya ini  ambayo ilimsumbua kwa miezi kadhaa hadi mauti yanamkuta.

“Dk. Masaburi alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa homa ya ini kwa muda mrefu, alikuwa India tangu Februari hadi Agosti, mwaka huu ambako alikuwa akipatiwa matibabu na hali yake ilipokuwa nzuri alirejea nchini, ” alisema.

Alisema madaktari wake walimtaka kurudi tena India Novemba, mwaka huu kufanyiwa uchunguzi zaidi wa afya yake kujua anavyoendelea.

“Lakini kabla Novemba haijafika hali yake ilibadilika ghafla ndipo akapelekwa Hospitali ya Regence kupatiwa matibabu. Ilipofika Oktoba 2, mwaka huu alihamishiwa Muhimbili.

“Alihamishiwa Muhimbili awe karibu na madaktari bingwa kwa uangalizi zaidi.  Madaktari walijitahidi kwa nafasi yao lakini ilipofika usiku wa juzi usiku (jana) Mungu alimpenda zaidi, ” alisema.

Alisema marehemu ameacha wake watatu, watoto 20 na wajukuu kadhaa.

“Dk. Masaburi aliacha wosia kwa familia kwamba atakapofariki dunia mazishi yake yafanyike hapa Chanika katika Chuo chake cha Ununuzi na Ugavi hivyo tutafuata wosia huo na atazikwa hapa Jumatatu ijayo, ” alisema.

Naye mjane mkubwa wa marehemu, Ashura Masaburi alisema kifo hicho kimempa majonzi mazito.

“Najisikia vibaya kufiwa na mume, sikuchoka kuwa na mume wangu…  Ni baba wa watoto wangu, mume wa ujana wangu nasikia uchungu mzito,” alisema.

Katika salamu zake, Rais Dk. John Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dk. Didas Masaburi kwa mshituko na masikitiko makubwa na anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.

“Poleni sana familia ya Dk. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu kwenu, lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa na msiba huu kwa kuwa tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini,” alisema Rais Magufuli.

Dk. Magufuli amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumpoteza mwana CCM mwenzao pamoja na viongozi na watumishi wa Jiji la Dar es Salaam ambao walifanya naye kazi alipokuwa Meya wa Jiji.

Masaburi ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), alifariki jana saa 3:30 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii kuanzia saa 4 usiku na baadaye kuthibitishwa na wanafamilia.

Wasifu wake

Mwaka 1995, Dk. Masaburi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar e Salaam .

Mbali na hilo pia alibahatika kuwa na Shahada ya Juu ya Masuala ya Ugavi  iliyotolewa na Bodi ya Uhasibu ya Taifa (NBAA), huku kwa miaka kadhaa akifanikiwa kuwa mfanyakazi wa Kiwanda cha vinywaji cha Chibuku.

Pia amefanyakazi Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo kupitia mradi maalumu wa Benki ya Dunia (WB)  na amekuwa akimiliki Shule ya Sekondari ya Dk. Didas Masaburi iliyopo Mbagala jijini Dar es Salaam pamoja na anamiliki Chuo cha Ugavi na Manunuzi kilichopo Chanika.

Dk. Masaburi alikuwa akiishi na figo moja kwa tangu mwanzoni mwa miaka 2000 hadi mauti yanamkuta.

Maisha yake kisiasa

Mwaka 2015, marehemu Dk. Didas Masaburi, alijitosa katika kunyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)  ambapo alishindwa na  aliyekuwa mgombea wa Chadema, Saed Kubenea ambaye alitangazwa kuwa mbunge hilo kwa kura 87,666  huku  Masaburi akipata kura 59,514.

Mwaka 2010, Dk. Masaburi alichanguliwa kuwa Diwaniwa wa Kata ya Kivukoni na Desemba 23, akachaguliwa kwa Meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo aliwashinda wapinzani wake, Diwani wa Kata ya Tandale, Amir Mbunju (CUF).

Meya huyo wa zamani alichaguliwa kwa kura 125  huku wajumbe wanne kati yao hawakupiga kura na 9 ziliharibika.

Mbali na kushika wadhifa huo pia alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) ambapo aliongoza nafasi hiyo kwa miaka mitano kabla ya kung’atua mwaka 2015.

Agosti 6, 2011, Dk. Masaburi aliingia katika malumbano ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walimtaka ajiuzulu kutokana na kukiuka taratibu katika uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles