27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wanasa mtandao mpya wa ujambazi

*siroWadaiwa kujificha katika pori la Dondwe

* RC aomba Mkoa Pwani uwe kanda maalumu

HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM na TUNU NASSOR, MKURANGA

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limenasa mtandao mpya wa ujambazi katika pori la Dondwe lililopo eneo la Chanika.

Hatua hiyo, imekuja baada ya jeshi hilo kupambana vikali na watu wanaodaiwa kuwa majambazi wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi wanne katika Benki ya CRDB Mbande, Mbagala wilayani Temeke.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu, baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambapo lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja anayesadikiwa kuwa jambazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na wenzake saba.

“Baada ya kumkamata jambazi huyo, alikiri kuhusika katika tukio lile na kuwapeleka askari wetu sehemu walipo wenzake katika pori la Dondwe wanapofanyia mazoezi ya kivita.

“Walipofika eneo hilo, ghafla majambazi hao walianza kufyatua risasi kuelekea  kwa askari, askari walilala chini na mtuhumiwa aliyewaongoza alikimbia.

“Akari walijibu mashambulizi ndipo mapambano yalianza na askari walifanikiwa kuwajeruhi majambazi wanne na kufanikiwa kupata bunduki ya kijeshi aina ya Sub Machine Gun (SMG) iliyofutwa namba za usajili, ikiwa na risasi 22,”alisema Kamishina Sirro.

Alisema majeruhi hao wakiwa mahututi, walikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wakati wanapatiwa matibabu walifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi.

Alisema baada ya uchunguzi wa awali, walibaini bunduki hiyo ndiyo iliporwa wakati askari wakibadilishana lindo katika Benki ya CRDB Mbande.

Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema jeshi hilo limewakamata vijana 15 wanaojiita ‘panya road’kutoka maeneo ya Mbagala, Kijichi, Kongowe  na Mzinga.

“Jeshi la Polisi lilifanya msako maalumu na kufanikiwa kukamata vijana wanaojiita panya road sita katika maeneo ya Kijichi, wawili kutoka Mbagala Saba Saba na wengine, baada ya kuhojiwa wote walikiri kujihusisha na vitendo vya ukabaji na uporaji katika maeneo mbalimbali ya jiji,”alisema.

Alisema pia watuhumiwa hao walikiri baadhi ya matukio waliowahi kuyafanya, ni tukio la kumkaba Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) na kumsababishia majeraha mbalimbali katika mwili wake katika eneo la Mbagala Mianzini kwa Mmponda.

Kamanda Sirro, alitaja majina ya viongozi wa vikundi hivyo kuwa ni Elias Gerald(18), mkazi wa Kijichi, Mustapha Shabani(18), mkazi wa Kijichi, Afis Mpango (30) na Frank Jumanne maarufu kama chura(18), wote wakazi wa Mbagala Kingugi.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa huku msako mkali ukiendelea kufanywa kutokana na kuendelea kuteja majina ya wengine na baada ya upelelezi kukamilika watapelekwa mahakamani.

RC PWANI

Katika hatua nyingine, Mkoa wa Pwani, unatarajiwa kuundiwa kanda maalumu ya kipolisi ili kukabiliana na matukio ya uhalifu.

Taarifa hiyo, ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alipozungumza wakati wa mazishi ya Bakari Sinkole aliyeuawa kwa risasi katika Kijiji cha Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga.

“Marehemu huyu ni mtu wa tano kuuawa kwa risasi katika staili hii hii. Kwa kweli, hatuwezi kuvumilia hali hii, mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, nimekaa na kamati yangu pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, tumekubaliana kuunda kanda maalum ya kipolisi ili  kukabiliana na wimbi la mauaji…tunategemea kuwa na ma-RPC wawili.

“Tumeamua kufanya hivyo ili kudhibiti matukio haya ya kihalifu kwani bila kufanya hivyo, hali itazidi kuwa mbaya,” alisema Ndikilo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, aliliambia MTANZANIA kwa simu juzi, kwamba watu wanaohusika na uhalifu huo ni majambazi wanaotumia silaha.

“Wahalifu hao ni majambazi wanaotumia silaha na wana pikipiki. Kwa mfano, inasemekana hivi karibuni walivamia ofisi za kijiji wakijaribu kupora fedha, hawakufanikiwa kwa kuwa hakukuwa na fedha ofisini hapo,” alisema Kamanda Mushongi.

Alipoulizwa kuhusu matumizi ya silaha wanazotumia wahalifu hao, alisema risasi zilizotumika zinafananishwa na za bunduki ya SMG ingawa haijathibitishwa.

Katika matukio hayo ya mauaji ya hivi karibuni Sinkole ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM kijijini hapo, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Katika tukio hilo la Oktoba 6, mwaka huu, Sinkole alipigwa risasi kifuani na kufariki papo hapo, huku Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Omary Mfilisi, akipigwa risasi begani na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Kabla ya mauaji hayo, watu wawili waliovalia kofia ngumu (helmet) na kuficha sura zao kwa vitambaa, walivamia ofisi hiyo wakiwa na pikipiki aina ya Boxer.

Walipofika ofisini hapo, waliwataka watu waliokuwa mahali hapo, walale kisha wakampiga risasi Sinkole.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu waliokataa kutaja majina yao, zinasema mauaji hayo yanatekelezwa na kundi la vijana wanaopinga kufungiwa nyumba yao ya ibada kijijini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles