25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Simbachawene: Kuna ufinyu wa viongozi wanawake

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema wanawake wanapaswa kuendelea kujengewa uwezo wa kiuongozi ili kuweza kukabiliana na changamoto iliyopo ya ufinyu wa jinsia hiyo katika nafasi za uongozi.

Mwenyekiti wa Chama cha wanahabari wanawake Tanzania(TAMWA) ambaye pia ni Mhariri Mkuu wa Clouds Media Group, Joyce Shebe wa kwanza kushoto, akiwa miongoni mwa wanawake viongozi, waliohitimu programu ya mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake, ambayo yametolewa na chuo cha Uongozi Institute cha hapa nchini.

Simbachawene alitoa kauli hiyo katika mahafali ya sita ya Taasisi ya Uongozi nchini ambapo miongoni mwa wahitimu wamo wa wahitimu wa programu maalum ya wanawake.

Alisema programu ya viongozi wanawake ambayo ni muhimu katika kujenga usawa wa kijinsia na kuwa na maendeleo endelevu.

“Bado kuna changamoto ya ufinyu wa wanawake katika nafasi za uongozi, hivyo ni lazima kuendelea kujengewa uwezo na pindi viongozi na wanawake wanapohitimu waende wakasaidiane na viongozi wanaume ili maarifa waliyoyapata yakalete suluhu na maendeleo ya nchi yetu,jambo hili kwa sasa si hiyari bali ni lazima,”alisema Simbachawene.

Alisema serikali inapaswa kuendelea kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa viongozi wanawake.

“Lakini katika hili wanawake mnaopata uongozi nawaasa mkachape kazi na lazima tufanye kazi kwakushirikiana,kuwawezesha kiuchumo isiwe sababu yakuleta jeuri katika jamii,”alisema Simbachawene.

Mbali na hilo Simbachawene aliwataka wahitimu wa masomo ya uongozi kuepuka vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha katika utendaji wao wa kazi.

Alisema ni vizuri viongozi wakajiepusha na vitendo vibaya ili kuitumikia jamii kwa maadili yaliyomema kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

Alisema uwepo wa mafunzo mbalimbali ikiwemo yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi ni chachu ya kuboredha utendaji kazi wa viongozi mbalimbali nchini hivyo ni muhimu kila anayepata nafsi kuweza kushiriki mafunzo hayo.

“Mtakubaliana nami kuandaa na kuendeleza viongozi sio jambo rahisi, kuna kila haja ya kuandaa viongozi kwa mafunzo mbalimbali ili kuwa na viongozi bora,Mwalimu Nyerere alisema nchi inahitaji watu, ardhi, siasa safi na Uongozi bora , hivyo ni muhimu kuandaa viongozi kwa kupatiwa mafunzo ya uongozi.

“Tunahimiza kuandaa viongozi bora ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, sensa inaonesha kuna watu milioni 61, kwa wingi huu tunahitaji kuandaa viongozi ambao watasimamia rasimali watu, hivyo ni jukumu letu kama taifa kuhakikisha tunajenga uongozi bora katika kusimamia rasilimali watu na kuleta maendeleo endelevu,”alisema Simbachawene.

Pia alisema ili kufikia malengo ya uchumi ushirikiano wa sekta za umma na binafsi ni muhimu sana, hivyo ametoa mwito kwa Taasisi ya Uongozi kuangalia namna ya kujenga ushawishi kwa viongozi wa sekta binafsi kushiriki kwenye mafunzo hayo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ikulu, Mululi Mahende alisema ni muhimu kwa serikali kuendelea kuwajengea uwezo viongozi wake na kwamba imekuwa ikiongeza bajeti kwa taasisi hiyo kila mwaka ili iwe na uwezo wa kuendelea kutoa mafunzo hayo.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo alitumia nafasi hiyo kueleza kwamba kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu 2023 jumla ya viongozi 15,000 wamapata mafunzo ya kozi mbalimbali kwenye taasisi hiyo na matarajio yao ni kuona viongozi wengi zaidi wanajiunga na kupata mafunzo.

Pia alisema programu 200 tofauti zimetolewa kwa viongozi wa kada mbalimbali ambao wamepita kwenye taasisi hiyo lakini viongozi 8,000 wameshiriki shughuli za taasisi kwa nyakati tofauti.

Pamoja na hayo alisema wameona kuna haja ya kuwa na programu maalum ya kozi kwa Viongozi wanawake huku akifafanua programu hiyo inakwenda kuwajengea uwezo viongozi hao na hatimaye kutoa fursa ya kushiriki kwenye nafasi za uongozi.

“Takwimu zinaonesha duniani ni asilimia 22 ya viongozi wanawake walioko kwenye nafasi za maamuzi na ili kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za uongozi itafikiwa ifikapo mwaka 2050, hivyo uwepo wa programu hii ya viongozi wanawake ni muhimu,”alisema Singo.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zainab Said aliipongeza Taasisi ya Uongozi kwa kuandaa programu ya viongozi wanawake kwani inakwenda kupanua wigo wa kukua na kusonga mbele katika uongozi wao ikiwemo katika nafasi za maamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles