Mwandishi Wetu -Dar es salaam
MATOKEO ya kidato cha nne kwa mwaka 2019 yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yameonyesha kuwa shule mbili tu kati ya zile kumi bora kitaifa ndizo wanafunzi wake wote wamepata daraja la kwanza.
Shule hizo kwa mujibu wa matokeo hayo ni Kemebos kutoka mkoani Kagera na St. Francis Girls kutoka mkoani Mbeya.
Matokeo yanaonyesha kuwa Kemebos ambayo imeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya shule kumi bora kitaifa, wanafunzi wake wote 70 wamepata daraja la kwanza.
Katika orodha hiyo, mwanafunzi aliyeonekana kushika nafasi ya mwisho ni yule aliyepata daraja la kwanza na pointi 11 huku 37 wakipata daraja la kwanza na pointi 7 na 33 ni wale waliiopata daraja hilo kwa pointi kati ya 8 na 11.
Kwa upande wa Shule ya St. Francis Girls ambayo katika orodha ya kumi bora kitaifa imeshika nafasi ya pili, matokeo yanaonyesha kuwa wanafunzi wake wote 91 wamepata daraja la kwanza.
Wanafunzi 56 wamepata daraja la kwanza na pointi 7 huku 34 wakipata daraja la kwanza na pointi kati ya 8-17.
Katika shule hiyo matokeo yanaonyesha mwanafunzi aliyeshika nafasi ya mwisho ni mmoja tu aliyepata daraja la kwanza na pointi 17.
Aidha shule nyingine ambazo nazo zimeingia katika orodha ya shule kumi bora kitaifa na kupata madaraja mengi ya kwanza lakini pia zimepata daraja la pili ni Feza Boy’s – Dar es Salaam, Cannosa – Dar es Salaam, Anwarite Girls – Kilimanjaro, Precious Blood – Arusha, Marian Boy’s – Pwani, St Augustine Tagaste – Dar es Salaam, Maua Seminary -Kilimanjaro na Musabe Boy’s – Mwanza.
Kwa upande wake Feza Boy’s ambayo katika orodha ya kumi bora kitaifa imeshika nafasi ya tatu jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 70, waliopata daraja la kwanza 72 na daraja la pili ni wawili.
Shule ya Sekondari Cannosa ambayo imeshika nafasi ya nne kitaifa, matokeo yanaonyesha waliopata daraja la kwanza ni 103 na mmoja tu ndiye aliyepata daraja la pili.
Anwarite Girls ambayo kitaifa imeshika nafasi ya tano, kati ya wanafunzi 53 waliopata daraja la kwanza ni 52 na mmoja tu ndiye aliyepata daraja la pili.
Kwa upande wa Shule ya Sekondari ya Precious Blood ambayo imeshika nafasi ya sita kitaifa ikiwa na jumla ya wanafunzi 91 waliopata daraja la kwanza ni 87 huku wanne tu wakipata daraja la pili.
Marian Boy’s ambayo inafuatia nyuma ya Precious Blood ikiwa na wanafunzi 108, waliopata daraja la kwanza ni 105 huku waliopata daraja la pili wakiwa ni watatu.
Aidha Shule ya Sekondari St Augustine Tagaste ambayo imeshika nafasi ya nane kitaifa, matokeo yanaonyesha kati ya wanafunzi wake 110 waliopata daraja la kwanza ni 105 na watano ndio waliopata daraja la pili.
Shule ya sekondari Maua Seminary ambayo imeshika nafasi ya tisa kitaifa wanafunzi wake 50 kati ya 52 waliofanya mtihani huo ndio waliopata daraja la kwanza na daraja la pili ni wawili.
Shule ambayo imefunga dimba katika orodha hiyo ya kumi bora kitaifa ya Musabe Boy’s yenyewe kati ya wanafunzi wake 118 waliopata daraja la kwanza ni 108 na daraja la pili ni kumi.
Uchambuzi wa jumla unaonyesha kuwa shule hizo zote 10 bora zimeonyesha kuchuana kwa ukaribu kwa kupata madaraja mengi ya kwanza.
Juzi Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) wakati likitangaza matokeo ya kidato hayo cha nne lilieleza kuwa watahiniwa 340,914 sawa na asilimia 80.65 kati ya 422,722 wamefaulu.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema kutokana na matokeo hayo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.38 ikilinganishwa na mwaka 2018 ambao ulikuwa asilimia 79.27.
UBORA WA UFAULU
Dk. Msonde alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, unaonyesha waliopata ufaulu mzuri wa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 135,301 sawa na asilimia 32.01.
Alisema kati yao, wasichana ni 58,542 sawa na asilimia 26.54 na wavulana 76,759 sawa na asilimia 37.97.
“Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.25 ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi tatu walikuwa 113,825 sawa na asilimia 31.76,” alisema Dk. Msonde.
Alisema waliofaulu kwa daraja la nne ni watahiniwa 205,613 sawa na asilimia 48.64.
Dk. Msonde alisema kati ya hao, wasichana ni 116,754 sawa na asilimia 52.92 na wavulana 88,859 sawa na asilimia 43.96.
Waliopata sifuri ni watahiniwa 81,808 sawa na asilimia 19.35, ambao kati yao wasichana ni 43,311 sawa na asilimia 20.54 na wavulana 36,497 sawa na asilimia 18.06.
UFAULU WA MASOMO
Dk. Msonde alisema takwimu zinaonyesha watahiniwa hao wamefanya vizuri zaidi katika masomo ya msingi ambapo ufaulu uko juu ya wastani kati ya asilimia 51.25 na 91.31.
Pamoja na hilo, alisema watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo ya Fizikia na Hisabati, ingawa kwa upande wa Fizikia ufaulu umeendelea kuimarika kutoka asilimia 45.50 kwa mwaka 2018 hadi asilimia 48.38 kwa mwaka 2019.