27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Shule ya Sekondari Salawe ilivyopambana na mimba kwa Watoto wa kike

Na Damian Masyenene, Shinyanga

TAKRIBANI miaka minne nyuma, hali ilikuwa mbaya katika shule ya Sekondari Salawe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, ikiwa inakabiliwa na changamoto kubwa ya wanafunzi wa kike kukatisha masomo kwa kupata mimba.

Wanafunzi wa Pambana Fema Club ya Shule ya Sekondari Salawe wilayani Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa shule hiyo, Faraja Mbilinyi (mwanamke) na mwalimu mlezi wa klabu, Daniel Masri

Tatizo hilo lilipelekea hatua mbalimbali kuchukuliwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, kufuatia kuchukizwa na hali hiyo na kutoa maagizo kadhaa ili kurejesha taswira nzuri.

Shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha nne ina wanafunzi 746 ikiwa na Bweni kwa wasichana pekee lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 35 tu. Shule hii ipo katika kijiji chya Azimio kata ya Salawe katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, imetajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya mimba kwa wanafunzi iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Inaelezwa kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ilikuwa inapoteza wanafunzi wengi kwa kupata mimba, ambapo inatajwa kuwa kwa mwaka takribani wanafunzi 20 wa kike walikuwa wanaacha masomo kutokana na ujauzito.

Akizungumza na www.mtanzania.co.tz shuleni hapo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Salawe, Faraja Mbilinyi, anasema kuwa alihamishiwa shuleni hapo mwaka 2019 na kukuta kesi 19 za mimba kwa wanafunzi, lakini kutokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa hali imepungua na kufikia wasichana watatu wanaopata ujauzito kwa mwaka jana.

Mwalimu Mbilinyi alieleza kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuanzisha klabu ya wanafunzi ya kuelimisha juu ya tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya afya, inayoitwa ‘Pambana Fema Club’ ambayo sasa ina wanachama 88 wanaotoa elimu ya jinsia, kutokomeza ukatili kwa wanafunzi na watoto na kuelimisha rika kupitia kupitia mikutano na vikundi.

“Hali ilikuwa siyo nzuri sana lakini tunashukuru sasa hali inakwenda vizuri kadri siku zinavyokwenda, nawashukuru walimu, kikundi cha FEMA na waelimishaji rika kutoka maeneo mbalimbali. Lengo letu ni kutokuwa na mimba kabisa,” alisema.

Mwalimu huyo alisistiza kuwa tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na kulega kwa malezi katika familia kwani amefanya ufuatiliaji kwa baadhi ya wanafunzi wanaopata mimba wazazi huwa hawafahamu lolote, ambapo ameshauri kuwa ili kukomesha kabisa na kuhakikisha hali inaendelea kuwa vizuri, ni vyema wazazi wasiwaache watoto na kuwapa uhuru uliopitiliza bila kufanya ufuatiliaji.

Baadhi ya wanafunzi wa kike ambao ni wanachama wa klabu hiyo walieleza kuwa Pambana Fema Club imekuwa msaada kwa wanafunzi wengi, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kwani kupitia elimu wanayoitoa imeweza kubadilisha fikra na kuwakomboa watoto wa kike.

Mmoja wa wanafunzi hao, Paulina Fabian wa kidato cha nne, alisema kuwa klabu yao imekuwa ikitoa ushauri, elimu ya jinsia na hutoa msaada kwa wanafunzi wa kike wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwashauri na kutoa taarifa kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo polisi na taasisi zingine ili kuwanusuru na vijana waharibifu.

Naye Agness Mwininga wa kidato cha tatu alieleza kuwa kupitia shughuli zinazofanywa na klabu hiyo ameweza kupata elimu ya vishawishi mbalimbali wanavyokutana navyo wasichana wengi hususani kutoka kwa wanaume katika kata hiyo wakiwemo waendesha pikipiki na kujiingiza kwenye mahusiano katika umri mdogo.

Kwa upande wake, Mwalimu Mlezi wa klabu hiyo, Daniel Masri alisema kuwa mwaka 2018 ziliripotiwa mimba zaidi ya 20, mimba 8 mwaka 2019 na tatu mwaka jana na kwamba klabu hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupitia majarida wanayoyapata, kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule jirani na shule za msingi na mitaani kupitia mikutano.

“Kulikuwa na tatizo kubwa la mimba, kwahiyo kushirikiana na wadau wa masuala ya kijinsia na afya wakaona itafutwe namna ya kukomesha ukatili huu kwa wanawake na watoto ndipo ikaundwa hii klabu mwaka 2017 na sasa ina wanachama 88 wakiwemo wavulana 40 na wasichana 48,” alisema.

Upande wa Serikali ya kijiji na Kata nao haukuwa nyuma kuhakikisha watoto wa kike wanasalimika na tatizo la mimba za utotoni, ambapo Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu alisema kuwa walilazimika kukaa pamoja viongozi wa serikali za mitaa na kupitisha mikakati ikiwemo kuwakamata wahusika na kuwawajibisha kupitia Sungusungu ikiwemo kuwatenga kwenye kijiji.

Alisisitiza kuwa wazazi wengi wa watoto waliokuwa wanakutwa na tatizo hilo walikuwa hawajitokezi kusaidia mamlaka kuchukua hatua, ambapo hadi sasa ni watu zaidi ya 10 waliokamatwa na kuchukuliwa hatua.

“Hapo nyuma tatizo lilikuwa kubwa, kwahiyo tulikaa tukaelewana viongozi tukapitisha kwamba sungusungu watusaidie kupambana na vita hii, imetusaidia kutujenga na kutubadilisha na pia tukatoa elimu kwa wanafunzi na wananchi, kwahiyo naweza kusema imepungua kutoka asilimia 100 hadi 40,” alibainisha.

Akieleza hali ilivyokuwa katika kata ya Salawe juu ya mimba kwa wanafunzi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko alisema kuwa alikasirishwa na matukio hayo kwani yalikithiri katika shule hiyo na kuleta aibu, lakini sasa anaridhishwa na juhudi inazofanyika kutokomeza mimba kwa wanafunzi.

DC Mboneko aliwataka wananchi kutafuta wanawake wa rika lao na kuwaacha wanafunzi wasome, huku akiagiza mkuu wa shule kuhakikisha kuwa mwaka huu hakuna mwanafunzi wa kike atakayepata mimba shuleni hapo.

“Tafuteni saizi yenu, niachieni watoto wangu wa shule, ogopeni kabisa sketi za wanafunzi msiwasumbue kabisa na wazazi tusaidiane kulea, tuwafuatilie watoto wetu na tusiwaachie uhuru uliopitiliza. Mwaka huu nisisikie kuhusu mimba hapa, wanafunzi waelimishwe na kushauriwa kuepuka mimba,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles