27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Shigela anadi fursa za GGML zinazoipaisha Geita katika kongamano la madini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAKATI Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania 2023 likifikia tamati Oktoba 26, mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela amebainisha fursa zinazotokana na uwepo wa kampuni kubwa ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kuwa chanzo cha kupaisha mkoa huo kiuchumi.

Mbali na GGML, pia zipo kampuni za kati na wachimbaji wadogo ambao wametajwa kusisimua uchumi wa mkoa huo ambao unazalisha asilimia 60 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela (katikati) ambaye alitembelea banda la GGML kwenye kongamano la Kimataifa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Jamii wa GGML, Doreen Dennis akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Mwandamizi Mahusiano ya Jamii –  GGML, Gilbert Mworia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika kongamano hilo lililofungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Shigela alisema wamekuja kushiriki ili kuona mwelekeo wa sekta ya madini, teknolojia mpya inayotumika na namna wachimbaji wadogo wanavyowea kuitumia.

Alisema GGML ni miongoni mwa makampuni makubwa ambayo yanaongoza kwa kulipa kodi nchini lakini pia yanaongoza kwenye uzalishaji wa dhahabu.

Alisema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia sheria, sera, miongozo ambayo inamtaka waziri wa madini kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki katika uchimbaji kwa kupewa leseni za umiliki, zimezidi kuipaisha sekta hiyo.

Alitoa mfano kuwa karibu asilimia 30 ya ya dhababu inayozalishwa mkoani Geita inatoka kwa wachimbaji wadogo huku asilimia 70 ikitoka kwa wachimbaji wakubwa.

“Maana yake ni kwamba rasilimali ya madini iliyopo katika mkoa wetu wa Geita inawafaidisha watanzania wote ikiwamo wenye mtaji na wasio na mtaji ambao pia wanataka kuingia kwenye sekta ya madini na mkoa pekee ambao wanaweza kuchimba kwa uhakika ni Geita.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia wamezalisha dhahabu zaidi ya tani 47 zenye thamani ya Sh trilioni sita na katika hizo tani 11 zinatokana na wachimbaji wadogo na 36 ni kwa wachimbaji wakubwa. 

Aidha, alisema uzoefu ambao wameupata kwenye sekta ya madini, ni pamoja na kupata fedha za kigeni kwa sababu ya kuuza dhahabu,

“Kwenye suala la ajira, mathalani kwa GGML peke yake imetengeneza ajira kwa watanzania zaidi ya 6000.

“Wananchi wanafanya biashara, manunuzi peke yake ya GGML kwa mwaka yanafikia zaidi ya Sh trilioni moja. Wananunua chakula, mavazi kwa ajili ya shughuli za uchimbaji, wananunua mafuta, wanatumia magari kusafirisha bidhaa, wanatumia malori na mabasi kusafirisha wafanyakazi zote hizi ni huduma ambazo zinapatikana Geita kupitia GGML,” alisema  na kuongeza;

“Lakini wapo wafanyabiashara ambao wanafanya biashara za hoteli wapo wafanyakazi ambao wanakuja kwenye mgodi, wapo wafanyabiashara wanakuja kununua dhahabu,” alisema.

Alisema mbali na Geita kuwa na soko la dhahabu, pia eneo la tatu ni faida itokanayo na mahusiano kati ya migodi na wananchi ambapo mkoa huo unafaidika na mpango wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kutoka GGML peke yake wenye thamani ya Sh bilioni tisa kila mwaka. 

Alisema Halmashauri ya Mji wa Geita na wilaya ya Geita hupanga bajeti ili fedha hizo zirudishe huduma kwa jamii ikiwamo kugusa sekta ya maji, elimu, afya na sekta za uzalishaji.

Katika uzalishaji alitoa mfano shughuli za kilimo pamoja na wafanyabiashara ndogondogo ambao wanawezeshwa na GGML kupitia jitihada hizo za uzalishaji na kukuza sekta ya madini.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa wanazozipata kutokaja na uwepo wa rasilimali hizo kwa kuweka akiba na kufungua biashara mbalimbali.

Pia aliwataka wamiliki wa migodi ambao hawajanza kutekeleza mpango huo wa CSR kushirikiana na jamii inayowazunguka lakini pia kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles