Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imeamuru Watumishi wa Umma waliosimamishwa kazi kutokana na elimu yao ya darasa la saba warejeshwe kazini na walipwe mishahara yao yote katika kipindi ambacho walisimamishwa kazi.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa bungeni Mjini Dodoma leo Jumatatu Aprili 9, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ikiwa ni siku chache tangu wabunge kuitaka serikali kuwarejesha kazini watumishi hao wakati wakichangia katika taarifa ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wiki iliyopita.
Akitoa kauli hiyo Mkuchika amesema serikali imechukua hatua hiyo kutokana na maoni na ushauri mbalimbali kutoka kwa wabunge.
“Pamoja na maelekezo sahihi ya serikali yaliyotolewa mara kwa mara kumejitokeza malalamiko ya kutozingatiwa kwa maelekezo hayo wakati wa utekelezaji, malalamiko hayo yamepokelewa na ofisi yangu kutoka kwa watumishi walioathirika pamoja na vyama vya wafanyakazi.
“Aidha serikali imepokea ushauri na maoni kutoka kwa wabunge kadhaa katika mkutano wa bunge unaoendelea kutokana na hali hiyo serikali imeamua na inaagiza watumishi wote warejeshwe kazini mara moja, walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa sheria.
“Watumishi hao ni wale ambao walikuwa na ajira za kudumu au ajira za mikataba (kwa watendaji wa vijiji na Mitaa) au ajira za muda ambao walikuwa kazini kabla ya Mei 20, mwaka 2004 ulipoanza kutumika waraka wa utumishi namba moja wa mwaka 2004.
“Pili Watumishi wa Umma 1,370 waliolegezewa masharti ya sifa za muundo kupitia barua ya Katibu Mkuu Utumishi yenye Kumbukumbu Na. CCB.271/431/01/P/13 ya Juni 30, mwaka 2011, warejeshwe kazini mara moja, walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa sheria.
“Uamuzi huu uliotajwa hautawahusu watumishi waliowasilisha vyeti vya kughushi katika kumbukumbu za ajira zao, watumishi waliokuwapo katika ajira kabla ya Mei 20, mwaka 2004, ambao katika kumbukumbu zao rasmi kama vile taarifa binafsi,” amesema Mkuchika.
Mmoja wa wabunge walioshinikiza kutaka watumishi hao warejeshwe kazini alikuwa Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu Musukuma (CCM), ambaye pamoja na mambo mengine alisema watumishi hao wasiporejeshwa basi hata wabunge wenye elimu ya darasa la saba akiwamo yeye wafukuzwe bungeni.
Mwingine ni Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema), ambaye alisema watumishi hao walifanya kazi kwa muda mrefu na kwa umakini wakiwamo madereva ambao wengine waliwahi kuwaendesha mawaziri wakuu na viongozi wengine wakitafuta kura wakati wa kampeni.